2941; UKIBI

Rafiki yangu mpendwa,
Unajua kuhusu ugonjwa wa UKIMWI.
Ambao ni kifupisho cha Upungufu Wa Kinga Mwilini.
Ni ugonjwa unaosababishwa na virusi na ni hatari.

Kwa dhana hiyo hiyo kuna ugonjwa mwingine nataka tuuite UKIBI. Ambapo ni kifupisho cha Upungufu wa Kinga kwenye Biashara.
Huu ni ugonjwa hatari ambao umeua biashara nyingi sana.

Biashara zinazokufa huwa zinakosa kinga kuu tatu;

Moja ni MFUMO wa biashara.
Mfumo wa kuendesha biashara ni kinga muhimu inayohitajika sana ili biashara iweze kufanikiwa.
Mfumo ndiyo unaiwezesha biashara kujiendesha yenyewe bila kutegemea uwepo wa mmiliki.
Mfumo wa biashara unakuwa ukielezea kila kinachopaswa kufanyika kwenye biashara na namna kinavyopaswa kufanyika.
Wazo bovu la biashara, likiwekewa mfumo mzuri linafanikiwa. Lakini wazo bora kabisa, kama litakosa mfumo mzuri litashindwa.
Ijengee biashara yako kinga kwa kuwa na mfumo thabiti wa kuiendesha.

Mbili ni TIMU ya kuiendesha biashara.
Biashara ni mchezo na mafanikio kwenye mchezo wowote ule yanategemea sana timu kuliko mtu mmoja mmoja.
Timu imara inayoongozwa kwa mfumo inaleta matokeo bora kabisa kwenye biashara.
Timu imara ni ile yenye watu wanaowajibika kwenye majukumu yao na kushirikiana kwa karibu katika kuyatimiza.
Ijengee biashara yako kinga kwa kuwa na timu imara inayotekeleza majukumu yote ya kibiashara.

Tatu ni WATEJA waaminifu.
Namba kuu na ya kwanza kwenye biashara ni mauzo. Na mauzo yatafanyika kama kuna wateja kwenye biashara. Ili mauzo yawe makubwa na ya uhakika, wateja wanapaswa kuwa wengi na waaminifu kwenye biashara.
Wateja waaminifu kwenye biashara ni wale ambao wanarudi tena na tena kununua na wanawaleta wateja wengine wengi nao waje kununua kwenye biashara.
Wateja ndiyo uwekezaji unaolipa zaidi kwenye biashara, kwani wakihudumiwa na kutunzwa vizuri, wanainufaisha sana biashara.
Biashara inaweza kuwa na wateja wengi na bado ikafa, kama wateja hao wananunua mara moja na hawarudi tena.
Mafanikio ya biashara yanategemea sana ubora wa wateja ambao inayo.
Ijengee kinga biashara yako kwa kujenga wateja bora na waaminifu kwenye biashara yako.
Wapende na kuwajali sana wateja wako kiasi kwamba hawatakuwa tayari kwenda kununua pengine ila kwako.

Tumeshaona ugonjwa mkuu unaoua biashara nyingi ambao ni UKIBI. Unaotokana na kukosekana kwa kinga kuu tatu kwenye biashara ambazo ni MFUMO, TIMU na WATEJA.
Wajibu wako mkubwa kama mfanyabiashara ni kujenga kinga hizo tatu.
Pambana sana kuhakikisha biashara yako ina kinga hizo tatu na utaifurahia sana.
Hili ni jambo linalohitaji kazi na kujitoa kweli kweli. Fanya hivyo kama kweli unataka kujenga biashara yenye mafanikio makubwa na ambayo haitetereshwi na chochote.

Kama ambavyo mtu mwenye UKIMWI anasumbuliwa na magonjwa ambayo watu wasio nao hayawasumbui, ndivyo pia biashara zenye UKIBI zinavyotikiswa na mambo mbalimbali.
Ijengee biashara yako kinga na itaweza kuvuka mengi yanayozisumbua biashara dhaifu.

#NidhamuUandilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe