3020; Nionyeshe orodha yako.

Rafiki yangu mpendwa,
Hakuna kipindi ambacho binadamu tumevurugwa kama nyakati tunazoishi sasa.
Tunaishi kwenye usumbufu mkubwa sana ambao unawinda umakini wetu.
Kuna mambo mengi sana ambayo yanaonekana tunapaswa kuyafanya, lakini siyo yote ni muhimu.

Njia pekee ya kutoka kwenye mtego huo wa kuwa na mambo mengi ya kufanya lakini yasiyokuwa na umuhimu ni kuwa na vipaumbele.
Vipaumbele ni kuhakikisha mambo yote yaliyo muhimu yanafanyika na hupotezi muda kwenye mambo yasiyokuwa sahihi.

Na ili kuweza kukamilisha yaliyo muhimu na kuepuka kupoteza muda kwa yasiyo muhimu, unapaswa kutumia orodha.
Kila unapoianza siku yako unapaswa kuwa na orodha isiyozidi vitu sita muhimu unavyopaswa kuvifanya kwenye siku yako.
Vitu hivyo vinapangiliwa kwa umihimu wake, namba moja ikiwa muhimu kuliko mbili, mbili muhimu kuliko tatu na kuendelea.

Kwa maana hiyo basi, siku yako inaongozwa na orodha unayokuwa umeweka.
Unafanya yale kwanza yaliyo kwenye orodha na huhangaiki na yaliyo nje ya orodha hiyo.
Kuna mengi yanayokuja kwako na kuonekana ni muhimu, lakini hupaswi kuhangaika nayo mara moja.
Badala yake unayaongeza kwenye orodha yako.

Ni muhimu sana uwe na orodha ambazo ndiyo zinakuongoza.
Unapaswa kuwa na orodha za mambo unayotaka kukamilisha kwenye siku, wiki, mwezi na mwaka.
Orodha zinakusaidia ufanye mambo kwa umuhimu na wakati wake.
Orodha zinazuia mambo yasiyo muhimu kuteka umakini wako kwa manufaa ya wengine.

Kwenye zama hizi za teknolojia, kuna njia mbalimbali za kuweka orodha kwa kutumia siku, kompyuta na programu nyingine.
Lakini njia bora kabisa ya kuweka na kufanyia kazi orodha yako ni kuandika kwa kalamu na karatasi.
Kwa kuwa na kijitabu kidogo chenye orodha yako unayofanyia kazi ni rahisi kuweka vema kwenye yale uliyokamilisha na hata kuongeza mengine yanayojitokeza, ambayo kwa sehemu kubwa yataenda kwenye siku nyingine.

Hakuna kitu kinachofurahisha na kuleta hamasa kama kuweka alama ya vema kwenye orodha yako kuashiria jukumu limekamilika.
Hiyo inakupa nguvu ya kuendelea na majukumu mengine uliyonayo kwenye orodha yako.

Watu wote wenye mafanikio na kipato kikubwa huwa wanafanya mambo yao kwa kuzingatia orodha.
Hivyo kama huna orodha, maana yake hutengenezi kipato kikubwa pia.
Kama unataka kuongeza kipato chako kwa ukubwa, anza kutumia orodha kwenye kila unachofanya.

Kwenye programu yetu ya Bilionea Mafunzoni kuna orodha mbalimbali ambazo ni lazima kuziweka na kuzifanyia kazi kila siku.
Ya kwanza ni orodha ya malengo makuu tunayofanyia kazi. Tunaandika orodha hii kila siku ili kuhakikisha hatuyasahau malengo yetu makuu.
Ya pili ni orodha ya majukumu ya kukamilisha kwenye kila siku yako. Hayo ni yale ambayo unapaswa kuwakamilisha kwenye siku husika ili kuyafikia malengo yako.
Na ya tatu ni orodha ya mpangilio wa masaa yako yote ya kazi kwa siku nzima, tangu unapoamka mpaka unaporudi kulala. Hapa unaupangilia muda wako wote wa siku na kisha kufuta mpango huo kwa msimamo ili uweze kufanya makubwa.

Ni rahisi sana kuweza kutabiri wapi utafika na maisha yako, kwa kuangalia orodha zako.
Kama huna orodha kabisa, hujui unachofanya na hakuna makubwa utakayoweza kufanya.
Kama una orodha ila hujaiandika, au umeandika lakini huizingatii, kila siku utakuwa unachoka ila hakuna matokeo makubwa utakayokuwa unazalisha.
Kama una orodha uliyoandika na unayoifuata kwa umakini mkubwa, utafanya mambo yaliyo muhimu na kuzalisha matokeo yaliyo bora.

Nionyeshe orodha yako na nitakuambia ni wapi unakwenda na maisha yako.
Watu wote wenye mafanikio makubwa wanazo orodha wanazoziheshimu na kuzifuata kwa msimamo wa hali ya juu.
Wakati mwingine wanaweza kuonekana kama wasumbufu au wenye mawazo mgando, lakini unga’ng’anizi wao huwa unawalipa sana baadaye.

Ongozwa na orodha na simamia vizuri orodha zako, hiyo ndiyo njia pekee ya kuweza kufanya makubwa sana kwenye maisha yako.
Mambo yote muhimu yaweke kwenye orodha.
Fanya yale yaliyo kwenye orodha tu.
Likijitokeza jambo jingine linaloonekana ni muhimu sana, liongeze kwenye orodha yako kwa ajili ya baadaye au siku zinazofuata.
Kama utakuwa mfuatishaji mzuri wa orodha, utakuwa na dharura chache sana zinazovuruga orodha yako.
Hivyo hupaswi kuwa na wasiwasi kuhusu dharura zinazoweza kujitokeza.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe