3049; Mambo ambayo huhitaji kukumbusha, lakini inabidi.

Rafiki yangu mpendwa,
Kuna mambo ya msingi kabisa kwenye safari ya maisha na mafanikio ambayo huhitaji kuwa unakumbushwa kila mara.
Haya ni mambo ambayo unapaswa kuwa unayaelewa kutoka ndani kabisa ya moyo wako.

Lakini kwa sababu binadamu tuna tabia ya kusahau mambo, hata yale ya msingi kabisa, inabidi turudie rudie kuambiana mambo haya ya msingi.
Cha msingi zaidi ni wewe mwenyewe kuendelea kujikumbusha mambo haya kila mara ili yakae juu kwenye fikra zako na uyatumie kufanya maamuzi sahihi.

Twende moja kwa moja kwenye mambo matano ya msingi kabisa kwenye maisha ambayo unapaswa kuyakumbuka kila mara.

1. Fanya kazi.
Hili halihitaji sana ufafanuzi, inaeleweka kabisa kwamba kila unachohitaji kwenye maisha yako, kinaanzia kwenye kazi.
Lakini ni mara ngapi umekuwa unashawishiwa kwamba kuna njia ya mkato ya kupata mafanikio isiyohusisha kazi?
Kila wakati kuna hadaa za aina hiyo unakutana nazo, ambazo kama ukijichanganya vibaya, unaweza kuamini kama ni kweli hivi.
Hivyo basi rafiki yangu, ni muhimu kujikumbusha hili kila mara.
Jiambie kabisa kwamba rafiki wa kweli ni kazi.
Haijawahi kuwepo na wala haitakuja kuwepo njia ya kujenga mafanikio makubwa na yanayodumu ambayo haihusishi kazi.
Ukiambiwa hiyo njia ni mpya na ya kweli, puuza, hakuna ukweli mpya.

2. Utashindwa.
Hii imekuja haraka na inaendana kinyume kabisa na mtazamo chanya tunaopaswa kujijengea wakati wote.
Lakini twende kwenye ukweli, tunaona watu wa kila aina wakishindwa kila siku, na wewe ni mtu, hivyo utashindwa kwenye baadhi ya mambo unayofanya.
Utashindwa mara nyingi kabla hujafanikiwa na hata ukishayapata mafanikio, bado kuna mengi utashindwa.
Mtu mmoja aliyefanikiwa sana alipoombwa kutoa ushauri kuhusu mafanikio alisema kwa ufupi; ili ufanikiwe, ongeza kasi ya kushindwa.
Ni muhimu sana kujikumbusha hili kwa sababu mbili;
Moja ni unaposhindwa siyo mwisho wa safari ya mafanikio, bali ndiyo safari yenyewe.
Mbili ni unapofanikiwa siyo kinga kwamba hutashindwa tena.

3. Huwezi kumridhisha kila mtu.
Kwa kitu chochote kile unachofanya, theluthi moja ya watu watakubaliana na wewe, theluthi moja watakupinga na theluthi moja watakupuuza, yaani watakuwa hata hawana habari kama umefanya kitu hicho.
Unajua ni theluthi ipi unatakiwa kuhangaika nayo?
Siyo yoyote kati ya hizo, mtu pekee wa kuhangaika naye ni wewe mwenyewe.
Fanya kile ambacho kinakuridhisha wewe kwanza, halafu hizo theluthi nyingine zitajipanga zenyewe.
Ukweli ni kwamba, kwa chochote unachofanya, kuna baadhi ya watu utawaridhisha, lakini kama utafanya kwa kuwaridhisha watu, wataishia kukuangusha.
Fanya kwa kujiridhisha wewe kwanza na kama kuna ambao nao wataridhika basi itakuwa kitu cha ziada kwako.
Na kama hakuna watakaoridhika, haitakuathiri kwa namna yoyote ile.
Kabla hatujaondoka hapa tukumbushane hili muhimu; kabla hujafanikiwa wengi watakudharau, ukishafanikiwa wengi watakuchukia.
Hakuna namna utaweza kubadili hali hizo, hivyo usiruhusu zikusumbue.

4. Wasiwasi hautakuisha.
Kitu kimoja ambacho sisi binadamu tunakipenda sana ni uhakika kwenye kila jambo na eneo la maisha yetu.
Uhakika ndiyo unaotupa utulivu mkubwa kwenye maisha.
Lakini ukweli wa maisha ni kwamba hakuna uhakika.
Hata mambo ambayo tunajiona tuna uhakika nayo, tunajidanganya tu, uhakika ni msamiati ambao haupo.
Na inapokuja kwenye safari ya mafanikio, mambo ndiyo tofauti zaidi, hakuna uhakika hata kidogo.
Kabla hujafanikiwa unakuwa na wasiwasi mwingi iwapo utafanikiwa.
Ukishafanikiwa unakuwa na wasiwasi mwingi kwamba utayapoteza mafanikio yako.
Jua hakuna wakati wasiwasi utakuisha kabisa, utaendelea nao kwa maisha yako yote.
Kila unapokuwa na wasiwasi jikumbushe hiyo ni sehemu ya safari na wajibu wako ni kufanya kile kilicho sahihi na bora wakati wote.

5. Utakufa.
Hili sihitaji hata kukuambia, kwa sababu ni adhabu uliyopewa siku uliyozaliwa. Kwamba siku moja utakufa, iwe utaishi mwaka mmoja, kumi au mia, kifo ni uhakika.
Unawaona watu wakiwa wanakufa kila siku na wewe ni mtu, hiyo ndiyo njia yako.
Lakini tena ubinadamu na kusahau vinaingia hapo.
Hebu jiangalie wewe mwenyewe jinsi unavyotumia muda wako wa kila siku, inaonyesha kweli una uelewa kwamba kifo kipo mbele yako?
Maana matumizi yetu ya muda ni kama vile tutaishi milele.
Mara zote ukikumbuka kwamba utakufa na ukiwa hujui kifo hicho kitakufikia lini, kila siku inakuwa ya thamani kubwa sana kwako.
Bila kusahau, kuna wale watu wanakutishia kwamba utakufa, pale unapoenda kinyume na matakwa yao binafsi, hao siyo tu uwapuuze, bali wacheke kabisa, huku ukiwatakia heri kwenye maisha yao ya milele hapa duniani.

Rafiki, yapo mengi ya kuendelea kujikumbusha kila siku ili usiyasahau kibinadamu. Haya matano ni ya msingi kabisa, ukiyazingatia, mengine mengi yataenda sawa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe