3057; Kwa nini nataka uuze.

Rafiki yangu mpendwa,
Kama ambavyo nimeshakuandikia mara kwa mara, una malengo makubwa matatu kwenye biashara yako.
Malengo hayo ni kujenga mfumo wa kuiendesha biashara, kujenga timu imara na kujenga wateja waaminifu.

Ili uweze kutekeleza malengo hayo, kuna majukumu makuu mawili ambayo unapaswa kuyatekeleza. Na majukumu hayo yanakutaka uvae kofia kuu mbili.
Ya kwanza ni uwe meneja mzuri wa biashara yako ili uweze kujenga mfumo na timu. Na ya pili ni uwe muuzaji namba moja kwenye biashara yako ili utengeneze wateja waaminifu watakaokaa kwenye biashara yako kwa muda mrefu.

Kwenye ukurasa huu tunaenda kuangalia zaidi eneo la mauzo.
Ninataka sana wewe uwe muuzaji kwa sababu ndiyo eneo ambalo lina njia ya wazi ya kukuza biashara na kufikia lengo la ubilionea.

Mauzo ni mchezo wa namba na ukishazielewa namba zako na kuzifanyia kazi vizuri, unaweza kuyatabiri matokeo kabisa.

Kama ukiweza kutengeneza wateja 100 wapya kila mwezi na kila mteja akawa ananunua kwa angalau Tsh laki 1 kila mwezi, kwa miaka mitano utakuwa na wateja wasiopungua 5000 na mauzo yasiyopungua Tsh milioni 500 kwa mwezi au Tsh bilioni 5 kwa mwaka.

Huu ni mfano rahisi wa idadi ya wateja 100, ambayo kila mtu anayejitoa kweli anaweza na mauzo ya Tsh laki 1 kila mwezi, ambapo mtu akiweka juhudi kuwafikia wateja sahihi anaweza pia.

Hizo ni namba ambazo zinawezekana hata kwa mtu mmoja tu akiwa amejitoa kweli kweli kujenga biashara kupitia kujenga mauzo.
Sasa namba hizo zinaweza kuwa kubwa zaidi kama kukiwa na timu kubwa ya mauzo.

Na ili kufikia namba hizo na kuendelea kukua zaidi, kuna vitu viwili vikubwa vinatakiwa kufanyika.
Cha kwanza ni kujenga timu imara ambayo itaweza kuendelea kuwafikia wateja wengi zaidi na kufanya mauzo makubwa zaidi kwa wateja hao.
Ujengaji wa timu imara unakutaka wewe kuwa mfano bora kwenye mauzo na kuwa meneja mzuri pia.

Kitu cha pili ni uweze kutoa bidhaa na huduma bora kabisa kiasi cha wateja kutokukuacha na kwenda kwingine.
Ukishampata mteja na akanunua kwa mara ya kwanza, anatakiwa kuendelea kununua kwako kwa kipindi chote cha maisha yake.
Kama umeweza kumuuzia kwa mara ya kwanza, utaweza pia kuendelea kumuuzia kama mambo yote yatafanyika kwa usahihi.

Namba tulizoona hapa siyo mwisho, ni mwanzo tu na kuna fursa kubwa sana ya ukuaji ukishaweza kufikia namba za aina hiyo.
Lakini yote hayo yanakutaka sana wewe uwe muuzaji bora na meneja mzuri.
Unahitaji kuwa mfano bora sana kwa watu wote unaowaajiri na kuwaweka kwenye mauzo.

Unaweza kuona wewe hulazimiki kuuza kama tayari umeshaajiri watu wa mauzo.
Lakini kumbuka hakuna mtu anayeweza kuyabeba maono makubwa ya kibiashara uliyonayo.
Na hakuna mtu anayeweza kujisukuma kuliko unavyojisukuma wewe.

Watu hata wawe sahihi kiasi gani, huwa wanaathiriwa sana na mazingira yanayowazunguka.
Kwa kuwa muuzaji bora na meneja mzuri, utaweza kujenga utamaduni bora kwenye biashara yako na kuigeuza kuwa mashine ya mauzo.

Biashara ikishakuwa mashine ya mauzo, yaani inazalisha matokeo ya uhakika kupitia timu inayokuwepo, hakuna kinachoweza kuizuia biashara hiyo kukua.

Uza na simamia vizuri, kuna hazina kubwa sana ipo ndani ya biashara yako.
Lakini hazina hiyo inataka kazi kubwa ifanyike ili kuiibua.
Kazi hiyo ndiyo wajibu wako namba moja kwenye biashara yako.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe