Rafiki yangu mpendwa,
Hakuna asiyejua umuhimu wa fedha kwenye maisha.
Huwa nasema, ukitoa hewa ambayo tunaivuta bure, kila kitu kwenye maisha kinahusisha fedha.
Na hata kwa hiyo hewa, unaipata bure ukiwa mzima wa afya, kwani ukipata maradhi makubwa, utahitajika kulipia ili uvute hewa.

Lakini pamoja na umuhimu huo mkubwa wa fedha, bado ni kitu ambacho watu wengi hawakipi uzito mkubwa kwenye maisha.

Kutokuipa fedha uzito unaostahili imepelekea watu kujiingiza kwenye matatizo ya kifedha ambayo yamewagharimu sana.

Tatizo kubwa la kifedha ambalo linawasumbua watu wengi ni madeni.
Mtu kuwa na madeni ni kiashiria cha wazi kwamba mtu huyo ana uzembe mkubwa kwenye eneo la fedha.

Najua kauli hiyo itawaumiza wengi, hasa ambao tayari wapo kwenye madeni, lakini ukweli unatakiwa kusemwa ili tiba iweze kupatikana.

Tuanze kwa kuangalia chanzo cha madeni ni nini.
Chanzo kikuu cha madeni ni matumizi kuzidi mapato.
Hapo ndipo matatizo yote ya kifedha yanapoanzia.

Kinachofanya matumizi kuzidi mapato ni kipato cha mtu kuwa chini huku matumizi yakiwa juu.

Mtu anayekuwa kwenye madeni, maana yake kuna uzembe anafanya kwenye maeneo hayo mawili; kipato ni kidogo na matumizi ni makubwa.

Kama kweli mtu yupo makini na kutaka kutoka kwenye changamoto hiyo ya kifedha, lazima aanzie maeneo hayo hayo mawili; kuongeza kipato na kudhibiti matumizi.

Lakini hivyo sivyo wengi wanavyofanya.
Wengi wakiwa kwenye madeni, wanachofanya ni kutengeneza madeni zaidi kwa kuendelea kukopa.

Na hapo ndipo ninapokupa onyo kwamba usinunue matatizo ya watu ya fedha.
Ninachomaanisha ni kwamba kama mtu anakuja kwako kukukopa fedha, tayari mtu huyo ana matatizo ya fedha.
Kama utamkopesha fedha anazotaka, usidhami umemsaidia kutatua tatizo lake, bali umelinunua tatizo lake.
Baada ya kukukopa, tatizo la fedha haliwi lake tu, linakuwa ni lako pia.
Kwani itakuwa vigumu sana kwa mtu huyo kukulipa.
Na siyo kama hataki kukulipa, ni kwamba tu hana namna ya kukulipa.

Hivyo mtu anapokuja kwako kukopa fedha, kumbuka hili, kumkopesha mtu fedha ni kuyanunua matatizo yake ya kifedha.

Kama unafanya biashara ya kukopesha na mtu anakidhi vigezo vilivyowekwa kibiashara vya kupata mkopo, hapo utampa.
Lakini kama kutoa mikopo siyo biashara yako, kaa mbali na hilo, utaishia kununua matatizo ya watu na yatakusumbua sana.

Kwa kumalizia, kama wewe ndiyo upo kwenye upande wa kuwa na madeni na kuomba mikopo kwa watu wengine, acha kulea uzembe.
Rudi kwenye msingi mkuu wa kuongeza kipato na kupunguza matumizi.
Ishi kwa gharama za chini kabisa iwezekanavyo na fanya kazi kwa muda mrefu zaidi.
Ukijitoa kweli kwenye hilo, utaweza kujijengea msingi imara sana wa kifedha.

Pata na usome kitabu cha ELIMU YA MSINGI YA FEDHA ambacho kitakupa mkakati wa kuongeza kipato, kudhibiti matumizi na kufanya uwekezaji ili uweze kujijengea uhuru wa kifedha.
Wasiliana na namba 0752 977 170 kupata nakala yako ya kitabu sasa.

Rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Muuza Matumaini,
Mwanafalsafa ya Ustoa,
Mkuu wa Chuo Cha Mauzo,
Kocha Dr. Makirita Amani
amakirita@gmail.com
http://www.amkamtanzania.com / http://www.t.me/amkamtanzania
http://www.utajiri.tz / http://www.t.me/utajiritz
http://www.mauzo.tz / http://www.t.me/chuochamauzo