3075; Mapenzi na pesa.

Rafiki yangu mpendwa,
Watu huwa wanasema kwamba pesa haiwezi kununua mapenzi,
Sijui kuhusu hilo kwenye mahusiano, lakini kwenye biashara, mapenzi na pesa haviwezi kutenganishwa.

Tukianzia kwenye msingi mkuu, utafanikiwa zaidi kwenye biashara ambayo unapenda kuifanya.
Ile ambayo kwako siyo kazi, bali kama mchezo, ambayo inahusisha kusudi la maisha yako na unafurahia jinsi wengine wanavyonufaika na siyo tu fedha unayopata.
Kwa kupenda unachofanya, unapata msukumo wa kufanya zaidi na hapo unapata matokeo bora zaidi yanayofanya upate fedha nyingi zaidi.
Mapenzi na pesa vinakwenda pamoja kama hivyo.

Baada ya msingi huo wa upendo kuwa msukumo wa kile unachofanya, tunakuja upande wa soko.
Soko la biashara yako linaathiriwa sana na mapenzi na pesa.
Kuna vitu vitatu muhimu vinavyopaswa kuwepo ili biashara yako iwe na soko zuri.
1. Biashara iwapende na kuwakubali wateja.
2. Wateja waipende na kuithamini biashara.
3. Wateja waweze kumudu kununua biashara inachouza.

Ni muhimu sana biashara iwapende na kuwakubali wateja ili iweze kuwahudumia kwa ubora wa hali ya juu sana, kitu kitakachowavutia wateja wengine pia.
Biashara itaweza kwenda hatua ya ziada kwenye kuwahudumia wateja pale inapowapa kipaumbele cha kwanza.

Wateja wanapaswa kuipenda na kuithamini biashara ili wakubali kununua na warudi tena kununua mara kwa mara. Pia wawe tayari kuleta wateja wengine nao wanunue.
Wateja wanaoipenda na kuithamini biashara wanakuwa mabalozi na mashabiki wazuri wa biashara hiyo, kitu kinachoipa fursa ya kukua zaidi.

Wateja wanapaswa kuweza kumudu kununua kile ambacho biashara inauza. Pia wawe tayari kulipa kulingana na bei iliyopo. Kwa kumudu kwao na kuwa tayari kulipia ndiyo wanasababisha mauzo kukamilika kwenye biashara.

Ili biashara ifanikiwe, lazima vitu vyote vitatu viwepo. Kikikosekana hata kimoja tu, biashara haiwezi kusimama imara na kufanikiwa.

Kama biashara inawapenda na kuwakubali wateja na wao wanaipenda na kuithamini biashara, ila wakawa hawawezi kumudu kulipia, biashara itashindwa kufanya mauzo mazuri, kitu kitakachofanya ikose fedha na ife kabisa

Kama wateja wanaipenda na kuithamini biashara na wanaweza kumudu kulipa ila biashara haiwapendi na kuwakubali, haitaweza kuwahudumia kwa ubora wa hali ya juu.
Matokeo yake wateja hawataridhika na hivyo kwenda kutafuta mahali pengine ambapo watapata huduma bora zaidi.

Na kama biashara inawapenda na kuwakubali wateja na wanaweza kumudu kulipa, ila hawaipendi na kuithamini biashara wanakuwa wateja wagumu sana kufanya nao kazi. Hata ufanye nini bado hawatathamini na kushukuru. Watakuwa watu wa kulalamika kwa kila kitu.
Wateja ambao inabidi uwalazimishe sana kufanya nao biashara huwa wanaishia kukusumbua wakati wa kufanya nao biashara. Watalalamikia bei japo wanaweza kuimudu na watachelewa sana kulipa.

Unahitaji kuwa na vitu vyote vitatu ili kuweza kuendesha biashara bora na yenye mafanikio makubwa.
Ukipata vyote vitatu, utakuwa na biashara ambayo unaifurahia sana, ambayo utakuwa tayari hata kuifanya usiku na mchana, kwa sababu kila kitu kinakwenda vizuri.

Kama kuna namna ambavyo biashara yako haiendi vile ulivyotaka iende, jiulize ni wapi unapokosea.
Je wewe mwenyewe unaipenda kweli biashara hiyo? Kama leo ungeshinda bahati nasibu na kupata mabilioni ya dola, je ungeendelea kufanya biashara hiyo?
Kama jibu ni hapana, basi unajua tatizo kuu linaanzia wapi.

Je biashara yako inawapenda na kuwakubali wateja? Kama wanaonekana wanaleta tu fedha kwenye biashara, hakuna cha ziada kinachofanyika na hapo inakuwa shida kupata wateja wengine wengi zaidi.
Kwa wateja kutokuhudumiwa vizuri, fursa za kuwauzia zaidi zinapotea.

Je wateja wanaipenda na kuithamini biashara yako? Kama jibu ni hapana, watakuwa wanakusumbua sana kiasi cha kushindwa kufanya biashara vizuri.

Na je wateja unaowalenga wanaweza kumudu kulipia kile unachouza? Kama uwezo wa watu kifedha ni mdogo, watashindwa tu kununua, bila kujali unahangaika nao kiasi gani.

Jikague vizuri wewe mwenyewe, biashara yako na wateja wako ili uweze kuona ni wapi unapokwama kuendesha biashara ambayo wewe mwenyewe unavutiwa nayo na kuwa kwenye nafasi nzuri ya kufanikiwa.

Ukijenga biashara yako vizuri kwa kuzingatia haya uliyojifunza hapa, utaweza kuwa na biashara bora kabisa, inayotoa thamani kubwa na ya kipekee, yenye wateja bora kabisa wanaoifurahia na inayofanya mauzo makubwa.
Hayo yote yapo ndani ya uwezo wako, ila yanakutaka ufanye kazi hasa na uache kabisa mazoea.

Huwezi kujenga biashara kubwa na bora kwa kuiendesha kwa mazoea.
Kufanya kile ambacho wengine wanafanya, utaishia kupata yale wengine wanapata.
Kufanya leo kile ambacho ulifanya jana, kesho utapata matokeo kama uliyopata leo.
Badilika kwa namna unavyoendesha biashara yako au soko litakutupa pembeni.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe