3078; Maji yanayoizamisha meli.

Rafiki yangu mpendwa,
Sote tunajua ya kwamba meli huwa inaelea kwenye maji.
Pamoja na uzito wake mkubwa, meli hiyo huwa inaendelea kuelea vizuri tu.
Lakini hiyo yote ni kama maji yataendelea kubaki nje ya meli.
Ni pale maji yanapoingia ndani ya meli ndiyo meli inapoanza kuzama.

Kumbe basi, maji yanayoizamisha meli ni yale yanayoingia ndani ya meli na siyo yanayobaki nje ya meli.
Na hata kwa kiwango, maji yanayoingia ndani ya meli na kuizamisha, siyo mengi kama yale yanayobaki nje.
Hivyo kiasi kidogo cha maji yanayoingia ndani ya meli huwa yana madhara makubwa sana.

Tunajifunza nini hapo?
Somo kubwa la kutoka nalo hapo ni chanzo cha wengi kushindwa kwenye maisha kinakuwa ndani ya mtu kuliko nje yake.
Kwa nje mtu anaweza kuzungukwa na vitu vingi vinavyochochea ashindwe, lakini havitakuwa na nguvu mpaka pale vinapoingia ndani.
Ni vitu vinavyoingia ndani ya watu ndiyo vinawafanya washindwe kwenye maisha.

Kuna mazingira mengi hasi ambayo mtu unakutana nayo kwenye maisha.
Lakini mazingira hayo hayawezi kuwa na madhara kwa mtu kama hajaruhusu mambo hayo hasi kuingia ndani yake.
Ni pale mtu anapoingiza fikra hasi kwenye akili yake ndiyo anapoanza kushindwa.

Kadhalika kwenye biashara, kuna changamoto nyingi sana ambazo huwa zinaathiri biashara, lakini changamoto hizo huwa hazina nguvu kama ni za nje ya biashara.
Changamoto zenye nguvu na madhara makubwa ni zile zinazoanzia au zinazoingia ndani ya biashara.

Biashara huwa inaanza kwa kushindwa ndani kwanza ndiyo baadaye kushindwa kunaoneoana dhahiri nje.
Watu wamekuwa wakiona ushindani mkali unaua biashara, lakini hilo ni kwa baadaye sana.
Biashara inafanywa kuwa dhaifu na mambo yanayokuwa yanaendelea ndani yake kiasi cha kupelekea ishindwe kuhimili mikiki mikiki ya nje.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwa mahusiano yanayovunjika.
Wengi hukimbilia kulaumu sababu za nje au upande mmoja kwenye mahusiano hayo.
Lakini ukweli ni kwamba kuna sababu za ndani ambazo zimefanya mahusiano hayo kuwa dhaifu kiasi cha kushindwa kuhimili mikiki mikiki ya nje.

Maisha hayawezi kukosa changamoto kabisa.
Kwa hakika changamoto ndiyo zinafanya maisha yawe na maana.
Kama ambavyo maji ndiyo yanafanya meli iendelee.
Changamoto zenye nguvu ya kuleta madhara kwenye maisha ya mtu ni zile ambazo zinaanzia au zinaingia ndani ya watu.
Changamoto zozote zile zilikabiliwa vizuri kwa nje, huku ndani mtu akibaki na utulivu mkubwa, ataweza kuzivuka na kuwa imara zaidi.

Kwenye maeneo yote ambayo unakwama kwenye maisha yako, jiulize ni vitu gani vya ndani yako mwenyewe vinakukwamisha kwenye maeneo hayo.
Wakati wengine wanakimbilia kulaumu mambo ya nje, wewe chimba ndani yako kupata majibu sahihi.

Tuchukue mfano wa biashara zinazoshindwa.
Huwa ni rahisi sana watu kulaumu mambo ya nje kama ushindani, uchumi mbaya, sera mbovu za serikali, wateja wagumu n.k.
Lakini hutasikia watu wakilaumu mambo ya ndani kama kukosekana kwa mfumo mzuri, kukosekana kwa timu imara na kutokuwepo kwa mchakato sahihi wa mauzo. Usimamizi wa fedha na watu kuwa mdogo pia huwa hautajwi.

Kwa mambo yote ambayo tunakwama au kukutana na ugumu, tukianza kwa kuchimba ndani yetu, tutaweza kuzuia ya ndani yasipelekee kushindwa kabisa.
Hivyo basi, kwa magumu na changamoto zozote unazopitia kwenye maisha yako, kabla hujakimbilia mambo ya nje, anza kwanza na ya ndani.
Ukiweza kuyatatua vizuri ya ndani, ya nje yanakosa nguvu ya kuleta madhara makubwa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe