3081; Mambo yasiwe mengi.

Rafiki yangu mpendwa,
Kwa kuwa tunataka sana kufanikiwa kwenye maisha yetu, huwa hatuoni kama sisi wenyewe tunaweza kuwa kikwazo kwenye mafanikio yetu.

Lakini ukweli ni kwamba sisi wenyewe huwa tunakuwa kikwazo kwa mafanikio makubwa tunayoyataka kwa sababu ya mambo kuwa mengi.

Kadiri mtu anavyokuwa na orodha ndefu ya mambo ya kufanya, ndivyo inavyokuwa vigumu kwa mambo hayo kutekelezeka.
Na siyo tu kwa sababu mambo ni mengi hivyo hayapati muda, bali ni mtazamo mzima wa mambo mengi ndiyo unaokuwa kikwazo.

Kwa mambo kuwa mengi kwenye orodha, mtu ni rahisi kuzoea mambo hayo na kudhani yatafanyika tu.
Wengi huona kitendo tu cha kuwa na orodha ndefu ya vitu vya kufanya.

Halafu kuna ile hali ya mtu kuchoka kabla hata hujaanza.
Kwa kuona orodha ikiwa ndefu, mtu unashindwa kuona wapi pa kuanzia, hivyo kukwama na kushindwa kabisa kuhama.

Kingine kinachokwamisha watu kwenye ufanyaji ni masharti yanayokuwa mengi ili mtu afanye.
Hapa mtu anajiwekea vigezo vya kutimiza ili kuweza kuchukua hatua, vigezo ambavyo kwa wingi wake ni nadra sana kukamilika.
Kwa kutokamilika kwa vigezo hivyo, mtu anakwama kuchukua hatua anazopaswa kuchukua.

Kutaka kuwa na maisha yenye mlinganyo kamili ni njia nyingine ya kuruhusu mambo mengi kuwa kikwazo kwa mtu kufanikiwa.
Kwa kuhangaika na kuangalia kama kila kitu kipo sawa, inapunguza nguvu na muda kwenye yale muhimu yanayopaswa kufanywa.

Ukiangalia watu wote ambao wameweza kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yao, kuna kipindi ambapo walipunguza sana mambo kwenye maisha yao.
Walikuwa na kipindi ambacho ratiba yao yote ilikuwa ni wao na kile wanachofanya tu.
Hawakuruhusu kitu kingine chochote kuchukua muda na nguvu zao.

Inapokuja kwenye kitu chako kikuu unachofanya, usiruhusu mambo mengi kukaa kati yako na kitu hicho.
Hakikisha mara zote kitu hicho ndiyo kipaumbele kikubwa na cha kwanza kabisa kwako.

Chukua mfano wa wanariadha wawili.
Wa kwanza utaratibu wake uko hivi; kama nikiwahi kuamka, na nikawa najisikia vizuri, huku hali ya hewa ikiwa nzuri na kuna mtu wa kuambatana nayo basi nitafanya mazoezi.
Wa pili utaratibu wake uko hivi; nawahi kuamka kisha nafanya mazoezi.
Iko dhahiri hapo ya kwamba ni rahisi sana wa kwanza kukwama na kutokufanya kutokana na mambo mengi aliyojiwekea, ni rahisi kwa moja kukwama na kuzuia mengine yote.
Lakini kwa wa pili, nafasi ya kufanya ni kubwa zaidi kwa sababu hakuna mambo mengi ya kuzingatia.

Punguza sana mambo unayohangaika nayo ili uweze kubaki na machache muhimu utakayoyafanya muda wote.
Tupo kwenye msimu wa HAPANA, ambao ukiweza kutumia vizuri neno HAPANA utaepuka mambo mengi sana yanayokukwamisha.

Kati yako na ndoto yako kuu, kupitia kile kikuu unachopaswa kufanya, pasiwe na kingine chochote kinachoweza kukukwamisha.
Ni wewe na kufanya, basi.
Kwa namna hiyo utalazimika kufanya, kwa sababu huna pa kutorokea.

Hebu jaribu kufikiria tu, kama unaamka mapema kila siku na muda wote wa siku yako unauweka kwenye kujenga biashara yako.
Kwa siku nzima unatekeleza majukumu ya kujenga mfumo, timu na kukuza mauzo.
Kwa umakini wako wote kuwa kwenye eneo hilo tu na kutosumbuliwa na mengine mengi, unajiweka kwenye nafasi ya kufanya makubwa na mazuri zaidi.

Ukishajiona kati yako na kufanya kile kinachokufikisha kwenye lengo kuu kuna mambo mengi, jua unajikwamisha mwenyewe.
Anza kutumia neno HAPANA kuondoa mambo hayo ili uweze kubaki na lile lililo kuu peke yake.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe