3084; Kila mtu anaongea, sisi tufanye.

Rafiki yangu mpendwa,
Watu wanaongea sana,
Wanaongea jinsi ambavyo wanataka kufanya makubwa.
Wanaongea jinsi ambavyo wengi siyo waaminifu wala wachapa kazi.
Wanaongea jinsi ambavyo mambo ni magumu na vikwazo vinavyowazuia.
Wanaongea jinsi walivyoshindwa kutimiza yale waliyoahidi wao wenyewe.

Lakini yote hayo wanayoongea hayana uzito kama ufanyaji.
Kuongea kunafurahisha na kuridhisha, lakini hakuzalishi matokeo yoyote.
Pamoja na hayo bado watu wengi ni waongeaji.
Kwa sababu kuongea huwa kunaleta ushindi hewa.
Kwa kuongea mtu anaona kama kuna kitu amefanikisha.
Lakini ukweli ni hakuna anachokuwa amesababisha.

Kwa kuwa sisi tunataka kuzalisha matokeo ya tofauti, tunapaswa kuwa kinyume na wengi.
Wakati wengi wanafurahia kuongea, sisi tunapaswa kuwa wafanyaji zaidi.
Tusiongee sana jinsi tunavyotaka kufanya makubwa, bali tufanye makubwa kwa kuanza hatua ndogo ndogo kwa msimamo bila kuacha.
Tusiongee sana jinsi ambavyo wengi siyo waaminifu na wachapa kazi, bali sisi tuwe waaminifu sana na tuchape kazi mno.
Tunaposhinda kutekeleza tulichoahidi, tusiongee sana nini kimetukwamisha, bali tufanye kwa ukubwa zaidi.

Maneno ni mengi, lakini hayana uzito kama matendo.
Maneno ni yale yale, ambayo ni ya kujirudia, lakini matendo huwa ni mapya na ya kipekee, hata kama yanaonekana kujirudia.

Maneno mengi ni kiashiria cha utupu wa mtu.
Kama ambavyo debe tupu huwa linavuma sana.
Ndivyo pia wanaoongea sana huwa siyo wafanyaji.
Yale ambayo watu wanakazana sana kusema, ni kinyume na vile walivyo.
Wanatumia maneno kuficha madhaifu makubwa yaliyo ndani yao.

Wewe usiwe muongeaji sana, bali fanya zaidi.
Unaweza usieleweke mwanzoni.
Unaweza usijulikane na wengi wala kusifiwa kama mafundi wa kuongea.
Lakini kadiri muda unavyokwenda, ndivyo tofauti ya maneno na ufanyaji inajidhihirisha.
Maneno yatabaki kuwa maneno, wakati matendo madogo madogo yanayoendelea, yanajikusanya na kuzalisha matokeo makubwa.

Laiti watu wangepeleka nguvu wanazotumia kuongea kwenye kufanya, matokeo ambayo yangezalishwa yangekuwa makubwa sana.
Laiti watu wangefanya chembe tu ya yale wanayosema, wangekuwa wa tofauti sana.
Lakini unajua nini,
Kuongea ni rahisi,
Kufanya ni ngumu,
Watu wengi wanapenda vitu rahisi.
Na watu wengi huwa hawafanikiwi.

Utachagua mwenyewe,
Kama utaongea sana, ujifurahishe na kuwafurahisha wengine kwa muda mfupi halafu uishie hapo.
Au kama utafanya zaidi, ukabiliane na ugumu, uchekwe, upingwe na kudharauliwa, lakini uweze kufanya makubwa zaidi baadaye.

Muda wako na nguvu zako zote unapaswa kuzipeleka kwenye kufanya.
Wacha matokeo unayozalisha yajieleze kwa nguvu kuliko maneno yako.
Unaweza kuona kama unachelewa, lakini kwenye maisha huwa hakuna kuchelewa.
Matokeo, bila ya kujali yamepatikana wakati gani, ndiyo yenye nguvu kubwa.

Jidhibiti wewe mwenyewe kwenye kuongea, fanya zaidi.
Na waepuke wale wanaoongea sana, ambatana na wanaofanya zaidi.
Ni kitu kidogo, ila chenye nguvu kubwa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe