3096; Mwanzo wa anguko.

Rafiki yangu mpendwa,
Watu wengi huwa wanadhani anguko la mtu kwenye maisha linaanzia kwenye kushindwa.
Lakini huo siyo ukweli.
Anguko huwa linaanzia kwenye mafanikio na siyo kwenye kushindwa.

Huwa kuna usemi kwamba kushindwa ni mwalimu mzuri sana wa mafanikio na kushinda huwa kunazalisha uzembe.
Ni pale mtu anaposhindwa ndiyo anapata msukumo wa kujifunza na kuchukua hatua za tofauti ili kupata ushindi.
Lakini mtu anaposhinda, huwa anajiona tayari anajua kila kitu na hahitaji kujifunza tena wala kuchukua hatua za tofauti.

Baada ya ushindi, watu wengi huridhika na kuenda kwa mazoea.
Ile kiu kubwa ya mafanikio ndani yao inapoa.
Wanalegeza mkazo waliokuwa wameuweka na ukawafikisha pale walipofika.
Nidhamu kali ya kazi waliyokuwa nayo wanaiweka pembeni na kwenda kama wengine.
Matokeo yake wanakaribisha anguko ambalo linawatoa pale walipokuwa wameshafika.

Kuondokana na hali hiyo, baki na njaa na kiu ya mafanikio mara zote, bila ya kujali ni matokeo gani umeyapata.
Unapopata ushindi, usiridhike na kuona umeshamaliza kila kitu.
Badala yake weka malengo mengine makubwa zaidi ya yale ambayo tayari umeshayafikia.

Kila wakati kwenye maisha yako unapaswa kuwa na kitu kikubwa unachokipambania, bila kujali umeshafanya makubwa kiasi gani.
Ushindi uliopata jana, leo hauhesabiki. Ushindi mkubwa zaidi unaoutaka kesho ndiyo unatakiwa kukunyima usingizi leo.

Hatari nyingine ya ushindi kwenye anguko inasababishwa na watu wanaokuzunguka.
Kama wanakuwa hawana mafanikio makubwa, wanatumia mafanikio unayokuwa umeyapata kukulazimisha uridhike.
Wanapokuona unaendelea kujisukuma licha ya ushindi ambao tayari umeshaupata, wanakuambia unapaswa kuridhika na ulichopata, kwa sababu ni kikubwa sana.
Na kweli ukiwaangalia wao na ukajilinganisha na wewe, unajiona umeshafika mbali na hivyo unaweza kupunguza juhudi unazoweka.

Hiyo ni hatari kubwa sana, ambayo ni vigumu kuivuka, kwa sababu wale wanaokuzunguka wana nguvu kubwa ya ushawishi kwako.
Ndiyo maana ni muhimu sana muda wote uzungukwe na watu waliofanikiwa kuliko wewe au ambao muda wote wanapambana kupata mafanikio makubwa kuliko yale ambayo tayari wameshayapata.
Watu wa aina hiyo watakupa moyo na msukumo wa kuendelea kuweka juhudi kubwa na kutokuridhika na ushindi unaokuwa umeshaupata.

Kama upo hai, muda wote unatakiwa kuwa na malengo makubwa unayoyafanyia kazi.
Malengo makubwa ambayo hujawahi kuyafikia na yanakupa msukumo wa kujituma zaidi.
Hupaswi kuwa kwenye hali ya kuridhika wakati wowote ule.
Pale tu unapoanza kuridhika ndipo anguko linapoanzia.

Wengi wanapokuwa wanaanzia chini, huwa wanaweka lengo ambalo ni kubwa na kuona wakishalifikia basi wamemaliza kila kitu.
Lengo hilo linawasukuma wajitume kwa kupitiliza.
Wakiamini ni zoezi la muda mfupi, kwani wakishafikia lengo watapumzika.
Ni pale wanapofikia lengo ndiyo wanaona kuna malengo mengine makubwa zaidi ya kufikia.
Hilo linawataka waweke malengo mengine makubwa zaidi na juhudi waongeze zaidi.

Kwa kifupi, maisha ya mafanikio hayana mapumziko.
Kujiambia ukifikia malengo uliyojiwekea utapumzika, ni kukaribisha anguko baada ya kuwa umepiga hatua.
Ukishafikia malengo uliyokuwa umejiwekea, unatakiwa kuweka malengo mengine makubwa zaidi.

Unaweza kuwa unajiuliza vipi hali ya uchoshi (burnout) inayoletwa na kuweka juhudi kwa muda mrefu bila kupumzika?
Jibu ni hali hiyo ya uchoshi huwa inaletwa na juhudi zisizokuwa na kusudi.
Kwa mfano nikikuambia ubebe mfumo wa sementi wenye kilo 50 na ukimbie nao, utalalamika ni mzito sana.
Lakini ikitokea mtu wako wa karibu, mwenye kilo zaidi ya 50, ameumwa na kuanguka ghafla, utaweza kumbeba na kumkimbiza eneo sahihi bila ya kuchoka.
Hivyo uchoshi hautokani na kila unachofanya, bali unatokana na sababu ya kufanya.
Kama huna sababu ya msingi ya kufanya, uchoshi unakuwa mkubwa.
Lakini unapokuwa na kwa nini kubwa ya kufanya kitu, uchoshi haupati nafasi.

Hivyo basi, tunajifunza umuhimu wa kuwa na kwa nini kubwa kwenye mafanikio makubwa tunayotaka kuyafikia.
Ikiwa tunachotaka ni fedha pekee, tukishazipata tutaridhika haraka na kuacha kuweka juhudi.
Ila tunapokuwa na kusudi kubwa zaidi ya fedha, tunapata nguvu ya kuendelea kujisukuma zaidi bila ya kuridhika wala kuchoka.

Haijalishi umefika wapi na kupata nini, kama bado upo hai, unapaswa kuendelea kujisukuma zaidi.
Kamwe usiridhike na kuzoea popote ulipofika, panga kwenda mbali zaidi ya popote unapokuwa umefika.
Hali hiyo ndiyo itakupa mafanikio makubwa na kukuacha kwenye kilele cha mafanikio.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe