3099; Usinywe tu, bali ogelea kabisa.

Rafiki yangu mpendwa,
Safari yetu ya mafanikio ni kama vita.
Unapokuwa vitani, chochote kinachoweza kukusaidia kupambana na adui kinatumika vizuri kabisa.
Iwe ni silaha, watu, taarifa, mazingira au hata hali ya hewa.
Na kadiri kitu kinavyokuwa na manufaa, ndivyo kinavyotumika kwa wingi na ukubwa.

Kwenye hii safari ya mafanikio, moja ya silaha muhimu tunazohitaji ni hamasa.
Ugumu na changamoto za hii safari vinafanya kukata tamaa kuwe rahisi sana.
Inahitajika hamasa kubwa sana kuweza kuvuka yote hayo na kubaki imara.

Kuna njia mbalimbali za kupata hamasa, ya nje na ya ndani.
Hamasa ya nje huwa inaamsha hamasa ya ndani na kumpa mtu nguvu ya kuendelea na mapambano.

Watu wengi hutania na kubeza hamasa ya nje kama dawa ya miti shamba ambayo mtu anakunywa, yenye ahadi ya kutimu mengi lakini isiyokuwa na uhakika.

Kama tutaamua kuchukulia hamasa hiyo ya nje kama dawa, wewe hupaswi tu kuinywa, bali unapaswa kuogelea ndani yake kabisa.
Yaani unapaswa kuipata kwa wingi sana ili ikupe nguvu kubwa ya kupambana.

Zungukwa na yale yanayokupa hamasa hiyo ya nje kwa wingi na mara zote.
Tumia yale yote yanayokupa hamasa ya nje ili kuchochea hamasa ya ndani na uweze kujisukuma kwa zaidi ya ilivyo kawaida.
Kama kuna vitu unasoma, kusikiliza, kuangalia au kufanya na vinakupa hamasa, fanya hivyo kwa wingi.
Kama kuna watu ukiwa nao au kuna mahali ukikaa unapata hamasa fanya hivyo.

Usijione kama una mapungufu kwa kuhitaji kupata hamasa mara kwa mara.
Kadiri safari ya mafanikio inavyokuwa kubwa, kadiri malengo yanavyokuwa makubwa, changamoto pia zinakuwa nyingi na kubwa na hivyo unahitaji hamasa kubwa zaidi.

Na kama tulivyoona hapo juu, ukiwa vitani, chochote kinachokusaidia kupambana na adui kinapaswa kutumika kwa wingi na uhakika.
Kwenye vita yako ya mafanikio, usiache kutumia silaha ya hamasa kwa wingi na uhakika.
Chochote kinachokupa hamasa, kitumie kwa wingi na ukubwa mno.

Kila unapokutana na kitu chochote ambacho kinafanya kazi, unapaswa kukitumia vizuri kwa manufaa ya hali ya juu.
Usiache kitu kwa sababu umekitumia sana na kukichoka.
Badala yake endelea kukitumia kwa uhakika kadiri kinavyoendelea kukupa matokeo mazuri.
Usikitumie kwa udogo (kunywa) bali kitumie kwa wingi sana (kuogelea) ili kiweze kukupa matokeo makubwa sana.

Unaweka juhudi ili upate matokeo.
Unapopata chochote kinachowezesha juhudi zako kuleta matokeo makubwa na mazuri, unapaswa kukitumia vyema.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe