3114; Viwango na mipaka.

Rafiki yangu mpendwa,
Maisha huwa ni magumu, lakini huwa tunayafanya kuwa magumu zaidi kwa kutaka kudhibiti mambo ambayo yapo nje ya uwezo wetu.

Moja ya vitu ambavyo huwa tunapenda sana kufanya ni kuwabadili watu.
Watu mbalimbali ambao tunachagua kushirikiana nao kwenye maeneo mbalimbali, wanakuwa na tabia ambazo ni kikwazo kwa kile tunachotegemea kwao, lakini tunajiambia tutawabadilisha hizo tabia zao.
Na hapo tunakuwa tumeingia kwenye mateso makali ya kujitakia.
Kadiri tunavyokazana kuwabadili watu hao, ndivyo wanavyokuwa wagumu kubadilika.

Ukweli ni kwamba, watu huwa hawapendi mabadiliko, hata kama mabadiliko hayo ni kwa manufaa yao wenyewe.
Na pale unapowalazimisha kubadilika, ndiyo unakutana na ukinzani mkali zaidi, wanafanya kila namna kuhakikisha juhudi zako za kuwabadilisha zinakwama.

Baadhi ya watu huwa wanaamua kubadilika wao wenyewe, hasa pale wanapokuwa wanataka sana kupata kitu fulani.
Hivyo siyo kwamba mabadiliko kwa watu hayawezekani kabisa, yanawezekana kama yataanzia ndani yao wenyewe na wakawa tayari kulipa gharama kubwa ya mabadiliko.

Rafiki, ukitaka kuyafanya maisha yako kuwa rahisi kwa kuepuka zoezi la kuwabadilisha watu lakini kupata matokeo unayoyataka, unapaswa kuweka viwango na mipaka.
Unatakiwa kuweka viwango ambavyo mtu anapaswa kuvifikia katika utendaji wake ili uweze kupata matokeo ambayo unayataka.
Na pia unatakiwa kujiwekea mipaka ambayo mtu hapaswi kuivuka katika utekelezaji wa majukumu yake.

Viwango vinaonyesha kipimo cha chini cha utendaji ambacho mtu anategemewa kukifikia ili aweze kuendelea kupata nafasi aliyonayo.
Kama mtu atafanya chini ya kipimo hicho, anakuwa ameshindwa kuendana na matakwa ya nafasi aliyonayo.
Ili kuhakikisha viwango vinafikiwa, lazima kuwe na namba za kupima na namba hizo kupimwa na kutathminiwa mara kwa mara.
Bila kupima, kutathmini na kuchukua hatua, viwango unavyokuwa umeweka vitabaki kuwa matamanio hewa, kwani hakuna atakayekazana kuvifikia.

Mipaka ni utenganisho kati ya yanayokubalika na yasiyokubalika.
Ni mstari ulio wazi wa nini kinakubalika kufanyika na nini ambacho hakikubaliki kufanyika.
Mtu anapovuka mipaka iliyo wazi, anakuwa amechagua mwenyewe kwenda kinyume na yale yanayotegemewa.
Mipaka inawaonyesha watu wigo wao wa kufanya yale wanayotegemewa kufanya.

Ili viwango na mipaka iweze kufanya kazi na kukupa matokeo unayoyataka, lazima kuwe na madhara yanayojulikana wazi kwa wale watakaoenda kinyume.
Lazima kuwe na madhara pale watu wanapofanya chini ya kiwango na kuvuka mipaka ambayo ipo.
Madhara yanaweza kuwa na viwango, kulingana na mwenendo wa mtu.
Mara ya kwanza mtu kukiuka anaweza kupewa onyo na kukumbushwa kuzingatia viwango na mipaka iliyopo.
Pale anapoendelea kuwa sugu kukiuka viwango na mipaka, licha ya kupewa onyo, ndipo hatua kali zaidi zinapohitajika kuchukuliwa, ikiwepo adhabu mbalimbali na/au kufukuzwa kabisa.

Yote mpaka hapo tulipofika ni rahisi na inaeleweka.
Ugumu huwa unakuja pale mtu unayejihusisha naye anakuwa wa karibu au anakuwa tegemeo kwako.
Inaweza kuwa unafanya kazi na ndugu yako wa karibu.
Inaweza kuwa ni mahusiano kati yako na mwenza wako.
Au inaweza kuwa ni mfanyakazi unayemtegemea sana.

Katika maeneo yote, bado unahitaji sana viwango na mipaka.
Na watu wanatakiwa kujua wazi viwango na mipaka hiyo.
Na kujua madhara yatakayowapata kama hawatazingatia.
Halafu basi, kuchukua hatua sahihi pale wanapokiuka.
Na muhimu, kuwa tayari kumpoteza mtu yeyote yule ambaye anakiuka viwango na mipaka uliyoweka, hata kama unamhitaji kiasi gani.

Ukileta tu upendeleo kwenye kusimamia viwango na mipaka uliyoweka, inakosa maana kwako na kwa wengine.
Watu wote watakiuka na hutakuwa na cha kuwafanya.
Kila mtu anayejihusisha na wewe anatakiwa kujua wazi viwango na mipaka iliyopo na kuzingatia.
Utajaribiwa sana na wengi kwenye viwango na mipaka yako, njia pekee ya kushinda ni kusimamia kwa uimara.

Watu huwa wanalalamika kwamba hawaheshimiwi na wengine.
Lakini watu hao hao wanakuwa hawana viwango na mipaka waliyoweka na kuwataka wengine wazingatie.
Bila kuwa na viwango na mipaka na kuvisimamia, hakuna mtu yeyote anayeweza kukuheshimu.
Na unahitajika kuwa unaishi kwenye viwango na mipaka uliyowawekea wengine.
Dunia haikupi kile unachotaka, bali kile unachokipambania kwa kukataa kilicho chini ya unachotaka.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe