3117; Usife.

Rafiki yangu mpendwa,
Bilionea Charlie Munger, mshirika wa karibu wa Warren Buffett huwa anaishi kwa kanuni hii; “Ninachotaka kujua ni wapi nikienda nitakufa, ili nisiende hapo.”
Anaiita kanuni ya kugeuza, kuanza na matokeo fulani kisha kujiuliza nini kifanyike kwa sasa kuzuia.

Munger ana miaka 99 na ni Bilionea, hivyo hiyo kanuni yake inafanya kazi kwa uhalisia.

Rafiki, kifo ndiyo hali pekee ya kudumu kwenye maisha yetu.
Mtu unaweza kubadili kila kitu kwenye maisha yako isipokuwa kifo.

Unaweza kufanya makosa mengi kwenye maisha yako, lakini yote utaweza kuyasahihisha kama tu utaendelea kuwa hai.

Hivyo basi, kosa kuu na kubwa kwa kila mtu ni kufa.
Na hapa kufa haimaanishi tu kimaisha, bali kwa kila kitu tunachofanya.

Kwa mfano kwenye biashara unaweza kusahihisha makosa mengi unayokuwa umeyafanya, kama tu biashara bado itakuwa hai. Biashara ikishakufa, hakuna namna unaweza kuboresha chochote kile.

Tunapaswa kuhakikisha chochote tunachofanya tunaepuka makosa ambayo yatapelekea kwenye kifo kabisa.

Cheza mchezo wako wa mafanikio kwa kuangalia muda mrefu zaidi.
Kwa muda mrefu, kila aliyedhamiria kitu fulani ameweza kukipata.
Lakini sharti la kwanza ni kuwa hai na kuendelea na mapambano.

Dhana ya usife inakutaka upime kila hatari kabla hujaingia.
Wajibu wako ni kuepuka zile hatari ambazo zinaweza kukupeleka kwenye kifo ili ubaki kwenye mapambano kwa muda mrefu zaidi.

Kama bado upo hai, ni kiashiria kwamba una nafasi ya kubadili yote uliyofanya huko nyuma.
Hivyo badala ya kupoteza muda na nguvu kwenye kujutia uliyofanya huko nyuma, zitumie kuboresha zaidi.

Hitaji rahisi kabisa la kupata ushindi kwenye jambo lolote la maisha yako ni kukaa kwenye jambo hilo kwa muda mrefu zaidi.
Kwani kuna hata hali ya kukutana na bahati nzuri ambazo zinakupa manufaa.
Lakini hayo yote ni kama bado utakuwa kwenye kitu hicho.
Ikiwa umeondoka, unakuwa umefuta fursa zote za mbeleni.

Dhana hii ya usife ni muhimu sana.
Kadiri unavyokaa kwenye kitu chochote kile kwa muda mrefu zaidi, ndivyo unavyojiweka kwenye nafasi nzuri na ya uhakika ya kufanikiwa.
Jua ni wapi ukienda au nini ukifanya utakufa ili usiende au kufanya.
Wajibu wako mkubwa ni kuhakikisha unadumu kwenye mchezo wako wa mafanikio kwa muda mrefu zaidi.

Muda ni silaha nzuri ya ushindi ukiwa upande wako.
Hakikisha muda unakuwa upande wako kwa kuepuka kifo cha aina yoyote ile.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe