3123; Chini ya kumi ni sifuri.

Rafiki yangu mpendwa,
Maisha yetu hapa duniani huwa yanaendeshwa kwa kanuni nyingi sana za asili.
Ni kwa kufuata kanuni hizo ndiyo tunapata yale tunayoyataka kwenye maisha yetu.

Moja ya kanuni muhimu sana kwenye safari ya mafanikio ni kanuni ya wastani.
Kanuni hiyo inaeleza kwamba kuna wastani wa kila kitu kwenye maisha.
Ili uweze kupata chochote unachotaka, unapaswa kwanza kuijua kanuni hiyo ya wastani na kuitimiza ndiyo uweze kupata unachotaka.

Kwa urahisi, kanuni ya wastani inaeleza uwiano wa kumi kwa moja, kati ya juhudi zinazowekwa na matokeo yanayopatikana.
Kwa mfano, ili uweze kuuza kwa mteja mmoja, inabidi uwafikie wateja wasiopungua 10 wenye uhitaji wa kile unachouza.

Kwa kanuni hiyo ya wastani, matokeo yoyote unayotaka kupata, zidisha juhudi mara 10 kisha tekeleza juhudi hizo.
Wateja unaohitaji ili biashara yako ijiendeshe vizuri, zidisha mara 10 na hiyo inakuwa idadi ya unaopaswa kuwafikia.
Ili kupata faida unayotaka, unatakiwa uuze mara 10 yake.

Tukiendelea kuirahisisha kanuni hiyo ya wastani, tunaona namba ya chini kabisa inayoweza kuleta matokeo ni 10.
Chochote kinachofanyika chini ya 10 ni sawa na hakijafanyika kabisa.
Ni vigumu sana kupata matokeo yoyote unayoyataka kama juhudi unazoweka ni chini ya namba 10.

Na hapo ndipo ninaposema kufanya chini ya 10 ni sawa na sifuri, yaani hujafanya kabisa.
Fikiria kufanya kwa viwango vya makumi na siyo mamoja.
Pia fikiria kwa kuzidisha badala ya kujumlisha.
Hivyo ndivyo unavyopaswa kuziendea namba zako ili upate kile unachotaka.

Epuka sana kufanya chochote kile kwa viwango vidogo na kukata tamaa haraka pale matokeo yanapokuwa tofauti na mategemeo uliyokuwa nayo.
Jua unapofanya mara 10 ndiyo inahesabika kama mara 1, hivyo chini ya hapo ni sawa na haijafanyika kabisa.

Utakuwa mahali pazuri sana kama kila juhudi unazopaswa kuweka utazidisha mara kumi kisha kutekeleza kweli.
Ukiweza kwenda na mpango huo, hakuna chochote kitakachoweza kukushinda kwenye maisha yako.

Fanya kwa ukubwa, wingi na msimamo chochote ulichopanga kufanya na utaweza kuzalisha matokeo makubwa sana na yanayokupa mafanikio makubwa pia.
Mara zote kumbuka kanuni ya wastani ya moja kwa kumi na fanya mara kumi ili kupata matokeo unayoyataka.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe