3132; Viwango vimeshushwa sana.

Rafiki yangu mpendwa,
Watu wengi huwa wana tabia ya kulalamikia mfumo wa elimu kwamba viwango vya ufaulu vimeshushwa sana.
Kwa ufaulu mkubwa ambao watoto wa siku hizi wanakuwa nao, mtu yeyote aliyesoma zamani anaona kama angesoma zama hizi, basi na yeye angepata ufaulu mkubwa sana.
Na hapo mtu hajaweka urahisi wa kujifunza uliopo kwenye zama hizi ukilinganisha na zamani.

Mambo hayo ambayo wengi wamekuwa wanayaona kwenye mfumo wa elimu ni ya kweli kabisa.
Lakini unajua nini kingine cha kweli?
Ni viwango ambavyo vipo kwenye kila eneo la maisha.
Viwango vilivyopo kwenye kila eneo la maisha vimeshushwa sana kiasi kwamba yeyote anayeshindwa kwenye eneo lolote ni uzembe wake tu ndiyo unakuwa umechangia.

Tuangalie eneo la biashara, unafikiri mtu aliyeishi miaka 50 iliyopita atayaonaje mazingira ya mtu kuanzisha biashara kwa sasa?
Hebu fikiria ni mahitaji kiasi gani ambayo mtu alipaswa kuwa nayo miaka 50 iliyopita ili kuweza kuanza biashara.
Kwa hakika mahitaji ni mengi sana, kuanzia eneo la uhakika, mtaji mkubwa, watu na kadhalika.

Lakini angalia leo hii, mtu yeyote anaweza kuanzisha biashara yoyote anayoitaka bila ya kuwa na hayo matakwa yaliyohitajika kipindi hicho.
Leo hii mtu anaweza kuanzisha biashara bila ya kuwa na eneo, wala mtaji, wala watu.
Yaani mtu hahitaji hata kuwa na wazo bora na la tofauti.
Viwango vya kuanzisha biashara vimeshushwa mno kiasi kwamba mtu yeyote kutokuwa na biashara zama hizi ni uzembe wake tu.

Kadhalila ni viwango vya mafanikio kwenye eneo lolote lile la maisha.
Miaka mingi ya nyuma, mafanikio ya mtu kwenye maisha yalitegemea sana amezaliwa kwenye familia ya aina gani.
Na hapo ni awe na bahati asiwe amezaliwa kwenye familia ya watumwa, maana aliendelea kuwa mtumwa maisha yake yote.
Mtu aliyezaliwa kwenye familia ya kifalme, alikuwa na uhakika wa mafanikio.
Na aliyezaliwa kwenye familia ya kimasikini, hakuwa na namna ya kutoka kwenye huo umasikini.

Lakini hebu angalia leo hii, mtu yeyote anayetaka kufanikiwa, anaweza kufanya hivyo bila ya kuzuiwa na chochote.
Na hata mafanikio yenyewe ya kumpa mtu utofauti, siyo makubwa sana.
Kwa kuwa wengi kwenye jamii hawapambani kupata mafanikio makubwa, mafanikio yoyote madogo mtu anaweza kuyapata, yatamfanya aonekane wa tofauti kabisa.

Hapo hatujaangalia eneo la kujifunza.
Tukirudi nyuma miaka michache tu, kabla ya kuja kwa mapinduzi ya mtandao wa intaneti na simu janja, kujifunza kitu chochote lilikuwa zoezi moja gumu sana.
Kusoma vitabu ilikuwa mpaka uende maktaba na hapo ni ubahatike kupata kitabu ulichotaka.
Kujifunza taaluma au ujuzi wowote ilikutaka ujiandikishe kwenye vyuo na kusoma kwa miaka mingi.
Lakini leo hii, kwa kuwa tu na simu janja unaweza kujifunza kitu chochote kwa muda wowote ukiwa popote.
Unaweza kupata na kusoma kitabu chochote unachotaka.
Na pia unaweza kujifunza taaluma au ujuzi wowote unaoutaka ndani ya muda mfupi sana.
Viwango vya kujifunza vimeshushwa sana, inashangaza kwa nini wengi hawajifunzi.

Rafiki, tunaweza kuendelea na hilo kwenye kila eneo la maisha na kuona jinsi ambavyo viwango vya kufanikia kwenye kila eneo vimeshushwa sana.
Hivyo basi, kama hujafanikiwa kwenye eneo lolote lile la maisha yako, kuna sababu moja tu ambayo ni uzembe wako binafsi.
Kama umeshindwa kujitofautisha na kundi kubwa la watu ambao hawana mafanikio makubwa, jua umejitakia wewe mwenyewe.

Kwa jinsi viwango vya mafanikio vimeshushwa sana kwenye kila eneo, ni kujidharau kwa hali ya juu sana kama tutashindwa kuyapata mafanikio makubwa tunayoyataka.
Huhitaji hata nguvu kubwa sana kufanikiwa, unachohitaji ni usiwe tu mzembe, uache kufuata mkumbo na kushika njia yako.

Mtu aliyekuwa na kiu kubwa ya mafanikio, ila akafa miaka 50 iliyopita bila ya kufanikiwa, akifufuka leo atakufa tena akiwa na sonona.
Kwa sababu atashangaa sana jinsi mafanikio yamekuwa rahisi, halafu watu wengi bado hawajafanikiwa.
Atashindwa kabisa kuelewa iweje watu wanateseka wakati mambo yamerahisishwa sana?

Tusiwe sehemu ya wale watakaomwangusha mtu wa aina hiyo.
Badala yake tuwe sehemu ya kumfanys ajivunie, kwa kuona tumeweza kutumia vizuri fursa nyingi zinazopatikana kujijengea mafanikio makubwa.

Viwango vimeshushwa sana,
Ushindani umekuwa mwepesi mno,
Lakini pia nguvu ya kuturudisha nyuma nayo imekuwa kubwa.
Tusikubali kumezwa na nayo mazoea, badala yake tutumie vizuri fursa zinazotuzunguka kufanya makubwa.
Tuishi kwenye zama tulizopo sasa, tukiwa na njaa ya mafanikio waliyokuwa nayo watu wa zama zilizopita.
Kwa namna hiyo tutaweza kufanya makubwa sana.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe