Habari njema rafiki yangu mstoa mwenzangu,
Mchezo mzima maisha yetu uko hapa. Kama tukiweza kuyajua yale ambayo yako ndani ya uwezo wetu na yale ambayo yako nje ya uwezo wetu tutaweza kuishi maisha yetu kwa uhuru zaidi.
Mambo mengine yanatokea yanatupa hofu kwa nini yametokea bila kujua hata hatuwezi kuyadhibiti kutokea kwa mambo hayo.
Sisi binadamu huwa tunasumbuka na mambo mengi sana. Lakini, tukianza kuyaangalia mambo hayo, mengi tunajisumbua nayo bure kwa sababu yapo nje ya uwezo wetu, hakuna chochote tunachoweza kufanya tukayabadili au kuyaathiri. Kwa mfano, kuwaka au kutokuwaka kwa jua ni kitu ambacho kipo nje ya uwezo wetu. Huwezi kuwalalamikia watu kwamba leo jua ni kali sana, au leo joto ni kali sana kwa sababu hata ukilalamika namna gani, huwezi kuzuia joto, ila unaweza kukabiliana na joto kama vile kutumia kiyoyozi na siyo kuzuia lisitokee.
Mambo mengi yanayotokea kwenye maisha yetu tunaweza kuyagawa kwenye makundi mawili.
Moja ni yaliyo ndani ya uwezo wetu. Haya ni mambo gani?
Haya ni yale mambo ambayo tunaweza kuyaathiri, tunaweza kuyafanya kuwa bora zaidi.
Kwa mfano, mauzo ni mchakato na siyo tukio. Kitu pekee ambacho tunaweza kukiathiri kwenye mauzo ni juhudi zetu sisi tunazoweka kwenye mchakato na siyo matokeo.
Mbili ni yale ambayo yako nje ya uwezo wetu. Haya ni yale mambo ambayo hatuwezi kuyadhibiti kwa namna yoyote ile yaani kifupi, hatuna cha kufanya. Kwa mfano, unaweza kudhibiti juhudi unazoweka kwenye jambo lolote lile lakini ukashindwa kwenye matokeo mfano, mgonjwa anayeumwa, daktari anaweza kuweka juhudi zaidi kwenye kumtibu mgonjwa lakini hawezi kumzuia mgonjwa kufa kwa sababu kifo ni kitu ambacho kipo nje ya uwezo au udhibiti wake.
Kwa namna yoyote ile, hupaswi kusumbuliwa na chochote kile kwa sababu kama kitu kipo ndani ya uwezo wako basi unahitaji kuchukua hatua.
Na kama kitu kipo nje ya uwezo wako, huna hatua ya kuchukua, basi kabiliana nacho kama kilivyo au kipuuze.
Mwanafalsa wa Ustoa Epictetus aliwahi kunukuliwa akisema, Baadhi ya vitu vipo ndani ya uwezo wetu na vingine vipo nje ya uwezo wetu. Vilivyo ndani ya uwezo wetu ni maoni yetu, fikra zetu, maamuzi yetu na matendo yetu, kwa kifupi yale yote ambayo sisi tunayafanya. Vitu vilivyo nje ya uwezo wetu ni miili yetu, mali zetu, sifa zetu na nafasi nyingine tunazopewa, kwa kifupi chochote ambacho hatufanyi sisi moja kwa moja, kipo nje ya uwezo wetu. Vitu vilivyo ndani ya uwezo wetu ni bure, huru na visivyo na ukomo, vilivyo nje ya uwezo wetu ni dhaifu, visivyo huru, vyenye ukomo na visivyo vyetu.
Nukuu;
Some things are up to us and some are not up to us. Our opinions are up to us, and our impulses, desires , aversions-in short, whatever is our own doing. Our bodies are not up to us, nor are our possessions, our reputations, or our public offices , or, that is, whatever is not our own doing. The things that are up to u s are by nature free, unhindered, and unimpeded; the things that are not up to us are weak, enslaved, hindered, not our own . – Epictetus.
Kama kuna kitu ambacho kinakusumbua kwa sasa, kaa chini jiulize, je hiki ninachopitia kwa sasa kipo ndani ya uwezo wangu? Kama kipo ndani ya uwezo wako, chukua hatua kubwa, bila hofu, bila sababu.
Hatua ya kuchukua; kama kitu kipo ndani ya uwezo wako, kibadili na chukua hatua.
Kama kitu kipo nje ya uwezo wako, kabiliana nacho au kipuuze kisikusumbue na kukuharibia utulivu wako.
Lengo kuu la falsafa ya Ustoa kwenye safari ya UBILIONEA ni kutujenga tuwe na wastahimilivu ili kupata utulivu. Hakuna kitu kibaya kwenye maisha yetu kama kukosa utulivu, tukipoteza utulivu kwa sababu ya mambo madogo madogo basi tutapoteza fokasi yetu kwenye safari ya UBILIONEA. Tupate utulivu na kuweka nguvu zetu zote kwenye malengo yetu na siyo kuruhusu vitu vidogo vidogo kutuvuruga.
Rafiki na Mstoa mwenzako,
Mwl Deogratius Kessy
Utilities ndio kila kitu. Kwani utulivu ukichangaya na focus tunaweza kupata mafanikio makubwa
LikeLike
Ni hakika nimejifunza kwa kina zaidi ntakwenda kufanyia kazi ili maisha yangu yakawe bora zaidi
LikeLike
Je! Hiki ninachopitia kipo chini ya uwezo wangu ama juu ya ya uwezo wangu? Kama kipo chini ya uwezo wangu nitajitahidi kikifanye kwa ukamilifu na kama kipo chini ya uwezo wangu sitahangaika nacho kabisa.
LikeLike