3133; Watu ambao hutaki kuwabadilisha.

Rafiki yangu mpendwa,
Ndiyo maisha ni magumu, lakini huwa tunazidisha ugumu wake kwa kutaka vitu ambavyo vipo nje ya uwezo wetu kuvidhibiti.
Tunajihakikishia tutaweza kukamilisha vitu hivyo.
Pale tunapojaribu kuvikamilisha na tukashindwa, tunapata sana msongo na kuona maisha ni magumu zaidi.

Moja ya eneo ambalo tumekuwa tunazidisha ugumu wa maisha na kujipa msongo ni kuwabadilisha watu.
Hii inakuja pale tunapochagua kushirikiana na watu kwenye eneo fulani, lakini wanakuwa wana tabia fulani ambazo hatuzitaki.
Tunajiambia tutawabadilisha tabia hizo ili wawe vile tunavyotaka sisi.
Na hapo ndipo tunapokaribisha matatizo na kuzidisha ugumu wa maisha.

Kwa kawaida watu huwa hawapendi kubadilika, huwa ni rahisi zaidi kwao kwenda na mazoea ambayo tayari wanayo.
Na pale watu wanapoona wanabadilishwa na wengine, ndiyo wanakuwa wagumu zaidi kubadilika.
Hivyo unapoanza zoezi lako la kuwabadili watu, ndipo mambo huwa magumu na mahusiano yenu kuwa na mivutano zaidi.

Na hiyo haijalishi nguvu yako kwenye hayo mahusiano, kuwabadili watu ni kitu kigumu.
Watu hudhani pale wanapokuwa na nguvu basi inakuwa rahisi kuwabadili watu.
Kwa mfano pale mtu anapomwajiri mfanyakazi, kwa sababu ana nguvu kwake, basi anadhani anaweza kumbadilisha.
Kitu ambacho huwa hakitokei, hata mtu afanye nini.
Hata kama mtu unamlipa, inapokuja kwenye kumbadilisha, ni kazi ngumu mno kwa upande wako.

Kama hali ndiyo hiyo, unafanyaje sasa ili kupata watu sahihi wa kushirikiana nao?
Jibu ni moja, anza na watu ambao hutaki kuwabadilisha.
Hawa ni watu ambao upo tayari kwenda nao kwa jinsi walivyo bila ya kuwabadili kwa namna yoyote ile.
Watu hao wanakuwa na tabia ambazo zina manufaa kwako kwa namna unavyotaka kushirikiana nao.
Na hapo inapaswa kuwa uhalisia wao na siyo maigizo ambayo wanaweza kukufanyia ili kukuhadaa uone wako vile unavyotaka.

Hilo linakutaka uwajue watu kwa uhalisia wao kabla hujafanya maamuzi ya kushirikiana nao kwa muda mrefu.
Lakini pia inakutaka uweke hisia zako pembeni na uwaone watu kwa uhalisia wao na siyo kwa vile unavyotaka kuwaona wewe.
Hivyo unahitaji kuwa na muda wa kumtazamia mtu kabla hujafanya maamuzi ya kuambatana naye moja kwa moja.
Hili ni kwa watu wote ambao unataka kujihusisha nao kwenye maisha yako, kuanzia maisha binafsi mpaka kwenye kazi na biashara.

Kitu kingine ambacho ni kigumu sana kwa watu ni kupokea ushauri ambao ni kinyume na walivyotaka wao.
Watu wanaweza kukuomba ushauri kwenye jambo fulani, na ukawashauri kwa namna ambayo ni bora kabisa.
Lakini wao wakaenda kutekeleza tofauti na ulivyowashauri.
Na wakati mwingine wakawa wamekosea kwa hatua walizochukua, na ushauri wako kuonekana ndiyo ungekuwa sahihi zaidi kwao.
Unaweza kusumbuliwa sana na hilo, likakuvuruga sana, kwa nini watu wakuombe ushauri halafu wakafanye tofauti?

Lakini unapojua asili ya watu, huwezi kuumizwa wala kuvurugwa na mambo kama hayo.
Unachotakiwa kujua ni kwamba watu wanapokuja kukuomba ushauri siyo kwamba hawajui nini cha kufanya.
Wanakuwa tayari wameshaamua kabisa nini wanakwenda kufanya.
Wanapokuomba ushauri ni kutaka tu kupima kama kile walichopanga kufanya unakubaliana nacho au la.
Ndiyo maana ukiwashauri watu kile kinachoendana na wanavyotaka kufanya wao, wanasema una ushauri mzuri.
Na ukiwashauri kitu ambacho ni tofauti na wanavyotaka wao, wanasema una ushauri mbaya na kuendelea na mpango wao.

Hilo halimaanishi usitoe ushauri kabisa.
Kwanza ni usitoe ushauri kwa mtu ambaye hajakuomba umshauri.
Siyo tu hatafanyia kazi ushauri wako, bali atakuchukia kabisa kwa huo ushauri unaokuwa umempa. Inashangaza sana lakini ndiyo uhalisia ulivyo.
Na pili, pale mtu anapokuomba ushauri una machaguo mawili;
Chaguo la kwanza ni kumuuliza yeye amepanga kufanya nini, kisha kumshauri namna bora ya kwenda na hicho alichochagua.
Chaguo la pili ni kumpa ushauri unaoona ni sahihi kwake, lakini jua kwa sehemu kubwa hataufanyia kazi, hivyo hilo lisikuumize.

Kwa sehemu kubwa sana, mafanikio yetu yanategemea sana watu ambao tunashirikiana nao.
Watu tunaowaoa au kuolewa nao.
Watu tunaoshirikiana nao kwenye biashara.
Wafanyakazi tunaowaajiri.
Wateja tunaowauzia.
Marafiki tunaoambatana nao.
Na watu wengine wengi.
Kuyarahisisha maisha yako, chagua kushirikiana na kuambatana na wale ambao tayari wana tabia unazozitaka, ambao huhitaji kuwabadilisha kwa namna unavyotaka wewe.
Hilo litakupunguzia msongo mkubwa sana kwenye maisha yako.

Na inapokuja kwenye eneo la kuwashauri watu, jua kabisa ni kitu ambacho huwa hakifanyi kazi, hivyo usikipe uzito ambao utakuumiza.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe