3143; Kikosi cha kwanza.

Rafiki yangu mpendwa,
Kila kocha wa mchezo, huwa ana wachezaji wengi kuliko inavyohitajika.
Kwenye wachezaji hao wengi anaokuwa nao, huwa ana kikosi chake cha kwanza.

Kikosi cha kwanza huwa kinakuwa na wale wachezaji bora kabisa ambao kocha anakuwa na imani nao kwamba wanaweza kumpa ushindi mkubwa.
Hicho ndiyo kikosi ambacho kocha huwa anakipanga pale anapokuwa na mashindano makubwa na anayotaka kushinda kwa uhakika.

Wachezaji wanaokuwa kwenye kikosi cha kwanza huwa nao wanajituma sana ili kubaki kwenye kikosi hicho.
Huwa hawajisahau na kuona wameshamaliza, bali wanajua wachezaji wengine wengi waliopo na ambao pia wanapambana kupata nafasi kwenye kikosi hicho cha kwanza.

Ili kuhakikisha wanaendelea kubaki kwenye kikosi hicho cha kwanza, wachezaji huwa wanajitoa kwa kupitiliza.
Wanaweka juhudi kubwa sana ili kuleta matokeo ya tofauti kwenye timu na kuhakikisha kwamba wanategemewa kwenye timu.
Wanahakikisha kama hawapo basi pengo lao linaonekana wazi na hiyo ndiyo inakuwa njia ya kujihakikishia wanaendelea kubaki kwenye kikosi cha kwanza.

Ili kuhakikisha wanabaki kwenye kikosi cha kwanza, wachezaji bora huwa wanazingatia yafuatayo;
1. Kuwa na maandalizi bora kwa kufanya mazoezi kwa viwango vya juu kabisa.
2. Kuweka nguvu kwenye maeneo ambayo wana uimara badala ya kuhangaika na madhaifu waliyonayo.
3. Kujiwekea viwango vya juu sana na kujisukuma kuvifikia ili kuondoka kwenye mazoea.
4. Kuwa na shauku na hamasa ya hali ya juu sana muda wote kitu kinachowapa nguvu ya kuendelea kuweka juhudi.
5. Kuweka vizuri vipaumbele na kutumia muda na rasilimali nyingine kwa ufanisi mkubwa.
6. Kutunza afya ili kuweza kuwa kwenye mchezo muda wote, kuanzia afya ya mwili, akili na roho. Maana mchezo ni mkali, bila afya imara hawawezi kuhimili.
7. Kuendelea kujifunza endelevu na kukazana kuwa bora zaidi ya walivyo. Kutokuwa na kiburi cha kuona tayari wanajua kila kitu na hawana tena cha kujifunza. Kuomba maoni ya kuboresha mchezo wao na kuyafanyia kazi maono hayo.

Kuwa kwenye kikosi cha kwanza haitoshi tu mchezaji kuwa na kipaji kwenye mchezo wake, wengi wana vipaji.
Kuwa kwenye kikosi cha kwanza inahitaji mchezaji kujitoa kwa viwango vya juu sana, kwenda hatua ya ziada kuliko alivyotegemewa na kuwa na msimamo kwenye yote ambayo anayafanya.

Rafiki yangu mpendwa, una njia mbili za kutumia haya maarifa;
Moja ni kujenga kikosi cha kwanza kwenye timu unayoijenga kwenye biashara yako. Angalia wale ambao wana sifa ulizojifunza hapa na kuwaendeleza vizuri ili biashara iweze kupata mafanikio makubwa.

Mbili ni wewe kupambana ili ukae kwenye kikosi cha kwanza kwenye KISIMA CHA MAARIFA na BILIONEA MAFUNZONI.
Ni wengi sana wanaotaka kupata mafanikio makubwa kwenye maisha yao.
Lakini ni wachache pekee wanaoyapata mafanikio hayo.
Siyo kwa sababu wachache hao ndiyo wenye uwezo au bahati, bali kwa sababu ndiyo wanakuwa wamejitoa kwa hali na mali kufanikiwa.

Je wewe umejitoa kiasi gani kuhakikisha unayapata mafanikio makubwa?

Uko tayari kupambana kiasi gani ili kubaki kwenye kikosi cha kwanza?

Unamfanya Kocha wako akutegemee kwenye nini ili kila mara aendelee kukupanga kwenye kikosi cha kwanza?

Jibu maswali hayo kwa uwazi kabisa hapo chini na yafanyie kazi majibu yako ili uendelee kubaki kwenye kikosi cha kwanza cha KISIMA CHA MAARIFA NA BILIONEA MAFUNZONI.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe