3146; Hujifunzi, una ahirisha.

Rafiki yangu mpendwa,
Tunaishi kwenye zama za maarifa na taarifa.
Hizi ni zama ambazo maarifa na taarifa zinapatikana kwa wingi na urahisi sana.
Kila mtu anaweza kujifunza chochote kile anachotaka bure kabisa au kwa gharama ndogo sana.

Tungetegemea kwenye zama kama hizi watu wajifunze kwa wingi sana na waweze kutumia maarifa waliyoyapata kupiga hatua kubwa.
Lakini hivyo sivyo ilivyo kwenye uhalisia.
Watu wengi sana hawajifunzi chochote kwenye maisha yao.
Na hao hao ndiyo wa kwanza kulalamika mambo ni magumu sana kwao.

Wengi wakiambiwa kwamba hawajifunzi huwa wanakuwa wakali.
Wanasema wanasoma vitabu na makala huku pia kusikiliza na kuangalia vipindi mbalimbali vya mafunzo.
Kwao kujifunza ni kupokea maarifa na taarifa.

Lakini kwenye uhalisia huko siyo kujifunza.
Kujifunza ni pale mtu anapochukua hatua za tofauti na kubadili hali aliyokuwa nayo.
Pale mtu anapopata maarifa na kuyatumia kuchukua hatua za tofauti ndiyo anakuwa amejifunza.

Haijalishi mtu amepata maarifa kiasi gani, kama hajayatumia kuboresha maisha yake basi hajajifunza.
Badala yake amekuwa ana ahirisha kufanya yale yaliyo ya msingi.
Yaani muda ambao aliutumia kupata maarifa ambayo hayatumii ni muda ambao aliahirisha kuchukua hatua sahihi kwenye maisha yako.

Huwa kuna usemi kwamba mtu anayejua kusoma ila hasomi vitabu hana tofauti na asiyejua kusoma kabisa, maana wote wanakosa vitu vizuri.
Kadhalika anayejifunza lakini hachukui hatua hana tofauti na ambaye hajajifunza kabisa, maana wote wako pale pale.
Zaidi ni anayesema amejifunza anakuwa ametumia muda huo kuahirisha kufanya yaliyo muhimu.

Kujifunza siyo mchezo wa kutazama.
Bali ni mchezo wa kuingia na kufanya.
Unajifunza kwa kina, kuelewa na kukumbuka kwa muda mrefu pale unapofanya kitu kuliko unapopata maarifa tu bila kuchukua hatua.

Kujifunza ni pale mazingira yanakuwa yale yale lakini hatua unazochukua zinakuwa za tofauti.
Sasa kama hatua unazochukua zinaendelea kuwa zile zile, maana yake hujajifunza. Maana huna tofauti na ambaye hakupata maarifa hayo.

Na kama utaandamana kwamba hilo haliwezekani, kwa sababu umesoma vitabu na makala nyingi sana, umesikiliza na kuangalia maarifa mengi.
Na kama utaenda mbali kabisa na kueleza vitu unavyoona umejifunza.
Nitakachokuambia ni huo muda uliotumia kupata hayo maarifa yote ni muda ambao umeahirisha kufanya yale muhimu unayopaswa kufanya.
Umejificha nyuma ya kujifunza, wakati hakuna chochote umejifunza.

Kwa kila maarifa unayoyapata, hata kwenye makala fupi kama hii, mwisho chukua dakika chache za kutafakari nini umeondoka navyo vya kwenda kufanyia kazi mara moja.
Anza kufanyia kazi vile ulivyoondoka navyo mara moja, usisubiri vipoe.

Ondoka hapa na orodha ya vitu unavyojiambia umejifunza kwa siku za karibuni ila bado hujaanza kuvifanyia kazi na nenda kavifanyie kazi sasa.

Huenda utaandamana tena, kwa kusema maarifa unayoyapata ni mengi sana kiasi kwamba huwezi kuyafanyia kazi yote.
Na hapo ndipo utakaponishangaza zaidi.
Kwa sababu ni ya nini uhangaike na maarifa hayo mengi ambayo hutayatumia?
Hapo si ni sawa na kula chakula kingi, halafu kukitapika chote hapo hapo, hupati virutubisho unavyotaka.

Ndiyo maarifa ni mengi mno kwenye zama hizi na hakuna anayeweza kumaliza kujifunza kila kitu kilichopo.
Na hapo ndipo panakuwa muhimu kuchagua vitu gani unavyojifunza na kufanyia kazi mara moja.

Kwenye programu yetu ya KISIMA CHA MAARIFA NA BILIONEA MAFUNZONI tuna vitabu vikuu viwili vya rejea; BILIONEA MAFUNZONI NA CHUO CHA MAUZO.
Hivyo ndivyo siyo tu tunapaswa kuvisoma, bali tunapaswa kuogelea humo na kufanyia kazi kila neno.
Kama hujafanyia kazi maarifa yote kwenye vitabu hivyo viwili, hustahili kujifunza kitu kingine chochote.
Chochote utakachojaribu kujifunza nje ya hivyo ni upotevu wa muda na kuahirisha kuchukua hatua ambazo kitabu kinakutaka uzichukue.

Kadhalika hizi makala za kurasa unazozipata kila siku, pamoja na za falsafa, ni za kukukumbusha mara kwa mara mambo ya kuzingatia katika kuyaishi maisha yako ya kila siku.
Unapaswa kuzifanyia kazi mara moja, kama zinavyoeleza.
Unasoma lakini huchukui hatua, jua hujajifunza.
Umepoteza tu muda ambao kama ungeutumia kutekeleza machache sana ambayo umewahi kuyapata, ungepiga hatua zaidi.

Ipo nadharia inayosema kwamba kadiri maarifa na taarifa zinavyopatikana kwa wingi na kwa urahisi, ndivyo watu wanavyozidi kuwa wajinga.
Hiyo ni kwa sababu wanatumia muda mwingi kukimbizana na kila aina ya maarifa na taarifa kiasi cha kushindwa kuchukua hatua.
Kila wakati ni kuingiza tu bila kutoa.

Wakati maarifa na taarifa vilipatikana kwa uhaba, watu walifanyia kazi kwa uhakika maarifa machache waliyoyapata na kuweza kupiga hatua kubwa.
Hawakuwa na anasa ya maarifa mengi ya kupoteza nayo muda.
Sasa maarifa yanapatikana kwa wingi sana na hakuna kitu watu wanafanya, zaidi ya kuendelea kupata maarifa mengi zaidi yanayoendelea kuwa usumbufu kwao.

Usisome kitu kingine chochote kabla hujachukua hatua kwenye kitu ambacho umejiambia umejifunza.
Maana kuchukua hatua za tofauti ndiyo maana halisi ya kujifunza.
Tofauti na hapo ni kuahirisha yale unayojua unapaswa kuyafanya, kwa kuingia kwenye usumbufu wa kupata maarifa mengi zaidi ambayo hutayatumia.

Kwa jinsi muda ulivyo wa thamani na wa uhaba mkubwa, ni jambo la kusikitisha sana kama utaupoteza kwenye usumbufu na kubaki pale pale ulipo.
Mara zote chukua hatua za tofauti kwenye yale unayojifunza ili uweze kuyaboresha maisha yako.

Na wala usihofu kwamba kwa kujifunza na kuchukua hatua mpya kila mara utakuwa mtu wa kubadilika mara kwa mara.
Bali utakuwa mtu unayeendelea kuwa bora kadiri unavyokwenda.
Maana hatua unazochukua kwenye yale unayojifunza siyo za kuanza vitu vipya kila wakati, bali ni hatua za kuboresha kile ambacho tayari unakifanya.

Pata maarifa kisha chukua hatua za tofauti kwa kutumia maarifa hayo uliyoyapata.
Hiyo ndiyo maana sahihi ya kujifunza.
Chochote tofauti na hapo siyo kujifunza, bali ni usumbufu na kuahirisha.

Kama bado utang’ang’ana kwamba unapata maarifa mengi ili usipitwe, unadhani nini kinakupita zaidi, maarifa unayoyapata au hatua ambazo huchukui?
Maana kwa wingi wa maarifa yaliyopo, tayari unapitwa, hata kama utajifunza kila siku kwa masaa 24.
Nafasi pekee uliyonayo ya kutokupitwa ni kufanyia kazi maarifa machache unayoyapata.
Hayo ndiyo yatakayoacha alama ya kudumu kwenye maisha yako.
Mengine yote utayasahau na yatakuwa yamekupita.

Je wewe umekuwa unajifunza au una ahirisha?
Ni maeneo gani umekuwa unajifunza na maeneo gani umekuwa una ahirisha?
Una ahidi nini hapa kuhusu kujifunza na kuacha ku ahirisha?
Jibu maswali hayo kwa kuweka maoni yako hapo chini.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe