3148; Mchezo wenye ushindi wa uhakika kwako.

Rafiki yangu mpendwa,
Watu wengi sana wamekuwa mashabiki na wafuatiliaji wa michezo.
Pale timu wanazozishabikia zinapocheza, wanakuwa tayari kuacha kila kitu ili wasikose mchezo huo.

Kinachowafanya watu kushabikia sana michezo ni kupenda ushindi.
Kila mtu anapenda kupata ushindi kwenye maisha yake.
Lakini kupata ushindi kwa mtu binafsi siyo kitu rahisi.
Inamtaka mtu kuweka kazi kwenye kitu kwa muda mrefu bila kuishia njiani.

Watu wanapokosa ushindi halisi kwenye maisha yao, ndiyo wanakimbilia kupata ushindi hewa kwenye ushabiki wa michezo.
Pale timu ambayo mtu anashabikia inashinda, anafurahi na kuona amepata ushindi yeye.
Utawasikia watu wakisema kabisa kwamba tumeshinda, kama vile naye alikuwa anacheza uwanjani.

Na watu siyo tu wanapenda ushindi, lakini pia huwa wanapenda kuonekana ni washindi.
Na hilo huwasukuma kuvaa jezi za timu zao pale zinaposhinda.
Kama timu imeshindwa, hawavai jezi hiyo.

Hayo yote yanatuonyesha jinsi ambavyo watu wanapenda ushindi kwenye maisha yao.
Na pale wanapokosa ushindi halisi, wanachukua ushindi feki.
Nauita ushindi feki kwa sababu haijalishi umefurahia kiasi gani kwa timu yako kushinda, hakuna manufaa ya moja kwa moja unayoyapata kwenye maisha yako.

Hapa napenda kukushirikisha mchezo wenye ushindi wa uhakika kwako na ambao una manufaa ya moja kwa moja.
Ni mchezo ambao utakuwa unapenda kuucheza na udhibiti wa kushinda mchezo huo upo ndani yako.
Na pale unapoweka juhudi na kushinda, manufaa unayoyapata yanakuwa na manufaa ya moja kwa moja kwako.

Mchezo ninaouzungumzia hapa ni mauzo.
Kufanya mauzo ni mchezo wenye uhakika wa ushindi.
Ushindi ambao unaweza kuuathiri moja kwa moja.
Na ushindi ambao unaingiza fedha moja kwa moja kwenye mfuko wako.

Mauzo ni mchezo unaoweza kuupenda kwa kuwa una nguvu ya kuchagua kuuza kile unachopenda au kupenda kile unachouza.

Pia ni mchezo ambao unaweza kujipa uhakika wa ushindi kwa sababu una udhibiti wa kile kinacholeta ushindi.
Njia pekee ya kupata ushindi kwenye mauzo ni kuongea na watu wengi zaidi.
Iwe ni ana kwa ana au kwa simu, kadiri unavyoongea na watu wengi, ndivyo unavyojiweka kwenye nafasi ya kupata ushindi zaidi.
Ukichagua kuongea na watu wengi zaidi, unapata ushindi mkubwa zaidi na kwa uhakika.

Na muhimu kabisa mauzo ni mchezo ambao manufaa yake ni ya moja kwa moja kwako.
Unapokamilisha mauzo, unalipwa fedha ambapo utatengeneza faida.
Ni kutoka kwenye faida unayotengeneza ndiyo unaingiza kipato moja kwa moja.
Hiyo ina maana kama utaweza kuuza kwa wengi zaidi na kutengeneza faida kubwa zaidi, utaweza kuingiza kipato kikubwa zaidi.

Waache wengine wahangaike na ushindi hewa kwenye ushabiki wa michezo.
Wewe hangaika na ushindi halisi kupitia kufanya mauzo.
Maana siyo tu wewe unayeshinda pale unapouza.
Bali hata mteja anashinda, kwa sababu unakuwa umemuuzia kitu chenye manufaa kwake.

Ushindi halisi ni mzuri na wa kufurahisha.
Ni ushindi ambao una manufaa makubwa kwako.
Ni ushindi wa mauzo.
Kuwa muuzaji bora kabisa kuwahi kutokea ili upate ushindi huo.
Utajihakikishia ushindi huo kwa kuongea na wateja wengi zaidi.
Kuwa na orodha kubwa ya wateja unaowafuatilia na wafuatilie kwa karibu na msimamo.
Kila mara utakuwa kwenye nafasi nzuri ya kupata ushindi kwa kukamilisha mauzo.

Je ni ushindi gani ambao umejitoa kwa kila namna kuweza kuupata kwenye mauzo?
Karibuni tushirikishane kwenye maoni hapo chini.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe