3154; Tofauti itakapoanzia.

Rafiki yangu mpendwa,
Siku ya jana, mjasiriamali na mwandishi Alex Hormozi alikuwa na tukio kubwa kabisa la kuzindua kitabu chake cha pili kinachoitwa $100M Leads.

Ni kitabu cha kutengeneza wateja tarajiwa kwenye biashara, ambapo ndani yake ameeleza njia nane za uhakika za kutengeneza wateja tarajiwa wengi kwenye biashara ya aina yoyote ile.

Ili kuonyesha njia hizo alizoainisha kwenye kitabu zinafanya kazi vizuri kabisa, aliamua kuzitumia zote kwenye tukio la kuzindua kitabu hicho.
Hivyo mapema sana alitangaza tukio hilo la uzinduzi wa kitabu na kutaka watu wajiandikishe kwenye mtandao.
Mimi ni mmoja wa waliofanya hivyo.

Kwa wiki zisizopungua sita, alitumia njia zote anazofundisha kwenye kitabu na akapata wahudhuriaji zaidi ya laki 5 waliojiandikisha kwenye tukio hilo.
Kwa kweli aliweka mategemeo ya kila mtu juu sana, akiahidi kuna kitu kikubwa ambacho atakitoa kwa wale tu watakaoshiriki uzinduzi huo mubashara kwa njia ya mtandao.

Siku ikafika ambayo ilikuwa ni jana na akafanya uwasilishaji bora kabisa kuwahi kutokea, kwa dakika 90.
Alieleza dhana nzima ya kitabu na kugusia njia hizo nane kwa mifano ya jinsi zinavyofanya kazi vizuri sana.

Mwisho akashirikisha mifumo 8 aliyoandaa ya kumsaidia mtu kwa uhakika kutengeneza wateja tarajiwa wengi kwenye biashara.
Alithaminisha mifumo yote 8 atakayompa mtu na ikawa zaidi ya dola elfu 12, hiyo ni karibu milioni 30 za Kitanzania.
Na ni kweli hiyo mifumo ina thamani kubwa mno, hatanii.

Kilichofuata baada ya hapo ndiyo kilitushangaza wote.
Kwa jinsi ninavyojua masoko na uwasilishaji, nilishajua wapi anaelekea.
Nilikuwa na uhakika atatoa mifumo hiyo kwa punguzo la bei kwa kuonyesha thamani kubwa ambayo mtu unaenda kuipata kwa kuwa nayo.
Na nilijiambia kwa uhakika bei atakayotaja haitapungua dola 900 na haitazidi dola elfu 5.

Akaendelea na uwasilishaji,
Akasema thamani hiyo ya zaidi ya dola elfu 12, ataitoa kwa dola elfu 4.
Akasema hapana, ataitoa kwa dola elfu 2,
Mpaka hapo nikawa najua wapi anaenda.
Lakini akaniacha na butwaa pale aliposema gharama halisi atakayotoza ni dola 0!
Kwa kweli sikuyaamini macho yangu.
Kila aliyeshiriki tukio hilo alishangazwa na kufurahishwa kwa wakati mmoja.

Nimejifunza masoko na mauzo kwa muda mrefu na niseme wazi, sijawahi kuona kitu cha aina hii.
Ni kitu cha kipekee mno, maana wengi huwa wanakisema, ila yeye amekitekeleza kwa uhakika.
Hakukuwa na mtego wowote, ni thamani ya dola elfu 12 ambayo unaipata bure kabisa, kwa kushiriki tu.

Kuna ofa nyingine alizotoa na ambazo alizopanga vizuri kwa kutumia mbinu ya uhaba, ambayo ilifanya kazi vizuri sana.
Lakini thamani kuu aliyoahidi kutoa bure ameitoa, mara baada ya tukio alituma kweli kwenye barua pepe yangu.
Kwa kuwamegea tu, tunayo zana moja matata sana ambayo tutaenda kuifanyia kazi kwa uhakika ndani ya Bilionea Mafunzoni na tutakuwa hatari mno.

Rafiki, hayo yote ni utangulizi tu, kilichofanya nikuandikie huu ukurasa wa leo ni kile nilichoona kwa watu baada ya tukio hilo.
Nilisema hebu nione watu wengine wanasemaje kuhusu uzinduzi huo ambao kwangu umekuwa wa kipekee kabisa.
Wengi walisifia sana, wakisema Alex amepandisha sana viwango vya uzinduzi wa kitabu.

Na kama kawaida, nikakutana na wengine ambao wanasema kama kila mtu atafanyia kazi mbinu zote ambazo Alex ametoa bure, kutakuwa na ushindani mkali sana sokoni na hivyo hazitafanya kazi.
Na hapo ndipo niliposhangazwa na kupata tumaini kwa wakati mmoja.
Nilishangazwa na jinsi baadhi ya watu wasivyokuwa na shukrani, au niseme kuwa na wivu kwa jinsi tukio hilo limekwenda kwa mafanikio makubwa.

Na nilipata matumaini kwamba kuna fursa kubwa sana ya kunufaika na mbinu hizo, kwa sababu, asilimia 99 ya watu waliozipata, hawatazifanyia kazi kabisa.
Kwanza kabisa wengi hawatafanyia kazi kwa sababu tu ya uvivu. Nimechungulia mfumo aliotuma wa hizo mbinu, nimeona inahitaji angalau masaa 8 ya kuangalia video za maelekezo. Na hapo nikajua kwa uhakika, wengi hawana utulivu wala umakini wa kutenga hayo masaa 8 ya kujifunza.
Kila mtu anataka vitu vya haraka haraka.

Pili, wengi watafikiri kwamba kwa kuwa kila mtu anafanyia kazi hayo, basi hayatafanya kazi.
Hivyo kwa kiburi chao, watahangaika kufanya kwa njia ya tofauti.
Na hawatapata matokeo mazuri kama yalivyoahidiwa.

Alex ametoa bure kabisa mchakato mzima uliomwezesha kujenga biashara zake na kufikia thamani ya zaidi ya dola milioni 100.
Na wachache sana ndiyo watakaonufaika na zana hizo, huku wengi mno hawatanufaika kabisa.
Tofauti ya makundi hayo mawili inaanzia kwenye KUFANYA.
Wote tumepata maarifa sawa kabisa, lakini tutatofautishwa na ufanyaji.
Wachache sana tutakaofanya tutanufaika.
Na wengi sana ambao hawatafanya hawatanufaika.
Ni rahisi kama hivyo.

Sote tunajua falsafa yetu kuu ya KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ni kanuni; KUJIFUNZA + VITENDO = MAFANIKIO.
Hiyo ndiyo tunayoisimamia mara zote.
Na ndiyo inayotutofautisha na wengine wengi.
Tuendelee kuidumisha hiyo.
Ndiyo itakayotufikisha kwenye mafanikio makubwa tunayoyataka.

Karibuni sana kwenye ufanyaji.
Kinachotuweka pamoja hapa ni kujifunza na kufanya.
Kama hujifunzi hupati nafasi.
Na kama unajifunza na hufanyi pia hupati nafasi.
Ni kujifunza na kufanya, ndiyo kunatutofautisha na watu wengine wote.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe