3159; Maokoto.

Rafiki yangu mpendwa,
Fedha ndiyo kitu ambacho huenda kina majina mengi ya utani kuliko kitu kingine chochote.
Fikiria majina mbalimbali ya fedha kama mshiko, mapene, ngawira, fuba au shekeli.
Yote hayo ni majina ya fedha yamekuwa yakitumika katika nyakati mbalimbali.

Na kwa wakati wa sasa, jina maarufu la fedha ni maokoto.
Binafsi nimelipenda jina hili kwa sababu lina mtazamo chanya na sahihi kabisa kuhusu fedha.

Watu wengi wamekuwa wanatumia kauli ambazo zinaashiria mtazamo hasi kuhusu fedha na hivyo kujizuia kuzipata kwa wingi.
Mfano mtu anasema nikipata fedha, nita …
Kauli hiyo inaashiria kwamba kuna uwezekano wa kupata au kutokupata.
Na hivyo mtu asipopata ni sawa tu.

Kuita fedha maokoto inaashiria kwamba fedha ni kitu cha kuokota, kwa sababu kimezagaa tu.
Na huo ndiyo ukweli, fedha zimezagaa kila mahali na wale wanaokuwa nazo kwa wingi siyo kwa sababu wana chochote cha tofauti.
Bali ni kwa sababu wanaamua kuziokota.

Watu hao fedha kwao ni kama udogo au mchanga.
Ukikuta mtu ana udogo mwingi, huwezi kumuuliza ameutengenezaje, unajua ameukusanya tu kutoka kwenye ardhi.

Unaona inavyokuwa rahisi kuifikiria fedha, kwa kuipa jina la maokoto, kwa maana kwamba ni kitu unachokusanya tu, maana kimezagaa kila mahali.

Huenda bado unafikiria unaokotaje fedha, basi tuendelee kurahisisha zaidi.
Njia pekee ya kupata fedha (maokoto) ni kupitia mauzo. (Najua zipo njia nyingine kama za wizi, tushwa, ulaghai, urithi, kushinda bahati nasibu n.k. Lakini unajua mwisho wa njia hizo, hivyo hatuzihesabii kama njia).
Lazima uwauzie watu kitu ndiyo wawe tayari kukupa fedha walizonazo.
Kwa maana hiyo basi, unaokota au kukusanya fedha kupitia mauzo.

Kwenye kuokota fedha kwa mauzo kuna vipengeke vinne, ambapo fedha ndiyo kipengele cha nne, ambacho ni matokeo zaidi.

Vipengele vingine ni kama ifuatavyo.

Cha kwanza ni kuwa na kitu chenye thamani ambacho watu wengine wanakihitaji sana.
Lazima uwe na kitu cha thamani unachouza, ambacho wengine wanataka sana kuwa nacho.
Hitaji hilo la wengine ndiyo linawafanya wawe tayari kukupa fedha ili wapate thamani unayouza.

Cha pili ni watu wa kuwauzia thamani uliyonayo. Watu ambao wana uhitaji mkubwa wa thamani hiyo na wanaweza kumudu kulipia ili wawe nayo.
Wengi wanaweza kutaka thamani uliyonayo, lakini kama hawawezi kumudu kulipia, hutaweza kukusanya maokoto.
Na hatupo kwenye shughuli ya kuwasaidia wasiojiweza. Bali tupo kwenye biashara ya kubadilishana fedha kwa thamani.

Cha tatu ni kuwashawishi watu hao wakubali kununua thamani uliyonayo. Unaweza kuwa na thamani ambayo watu wanaihitaji na wanaweza kuimudu, lakini wasinunue kama huna ushawishi mzuri kwao.
Na ushawishi kwenye mauzo huwa unaanza kwa urafiki na kuaminika. Hivyo unawajibika kujenga urafiki na kuaminika na wale unaopanga kuwauzia thamani uliyonayo ili wakubali kununua.
Kumbuka njia ya mauzo ya kukusanya maokoto inahusisha watu kukubali wao wenyewe kukupa fedha zao na siyo kuzichukua kwa nguvu.

Vitu hivyo vitatu vikija pamoja ndiyo vinazalisha kitu cha nne ambacho ni maokoto.
Wengi wanakwama kukusanya maokoto kwa sababu wanaanzia mwisho badala ya kuanzia mwanzo.
Ni lazima upande kabla hujavuna.

Mahali pa wewe kukusanya maokoto.

Biashara uliyonayo sasa ndiyo mahali sahihi kwako kukusanya maokoto mengi kadiri unavyotaka.
Unachohitaji kufanya ni kuongeza thamani ya kile unachouza, kuwafikia wengi zaidi (usakaji), kuwashawishi kununua (ukamilishaji) na kuwapa huduma bora sana ambazo hawawezi kuzipata mahali pengine (uhudumiaji).

Biashara yoyote inayofanyia kazi maeneo hayo matatu kwa fokasi kubwa, kwa msimamo bila kuacha na kwa muda mrefu, lazima itakusanya maokoto mengi.
Lakini pia siyo njia rahisi, ina vikwazo na changamoto za kila aina. Hivyo lazima mtu ajitoe kisawasawa na kamwe kutokukata tamaa na kuishia njiani.

Umakini mkubwa unahitajika, maokoto huwa yana wivu, yakiona huyapi umakini yanakukimbia.
Unayapa maokoto umakini kwa kuzijua namba zako na kuzifuatilia kwa umakini mara zote.
Usilete uzembe, uvivu au mazoea kwenye kufuatilia maokoto yako.
Jua kila namba kila wakati ili uweze kuboresha kwa kukuza zaidi.

Vitu vingine unavyoweza kuuza ili kukusanya maokoto.

Moja ni fedha, ukiwa na fedha, unaweza kuzitumia kama nyenzo ya kupata fedha zaidi. Kwa mfano kwa kuziwekeza vizuri fedha, unaweza kuzalisha fedha zaidi.

Mbili ni ujuzi/uzoefu uliojijengea. Pale unapokuwa na vitu vya thamani unavyoweza kufanya ambavyo wengine hawawezi kufanya, watakuwa tayari kukulipa ili uwafanyie au uwafundishe kufanya.

Tatu ni muda. Kama huna fedha wala ujuzi/uzoefu, unakuwa na muda mwingi. Unaweza kuuza muda huo kwa wengine wenye uhitaji nao na katika kufanya hilo ukajenga ujuzi/uzoefu ambao utaweza kuuza kwa thamani kubwa zaidi na kupata fedha ambazo pia utauza kwa kuwekeza.

Naamini unapata picha hapo jinsi mambo yanavyopaswa kwenda, nenda nayo hivyo.
Muhimu ni maokoto, na popote ulipo, tumia kile ulichonacho kuongeza maokoto zaidi.

Pamoja na kwamba mauzo ndiyo njia bora ya kukusanya maokoto, bado mauzo hayafanani.
Kuna mauzo yana maokoto makubwa na mauzo yenye maokoto madogo.
Mauzo yenye maokoto makubwa ni yale yanayotibu maumivu makubwa ambayo tayari watu wanayo na hawawezi kuyavumilia.
Watu huwa wanachukua hatua haraka sana kuondokana na maumivu wanayokuwa nayo.
Mauzo yenye maokoto madogo ni yale yanayozuia maumivu yasitokee. Kimantiki hayo yalipaswa kuwa mauzo bora, lakini ni kazi ngumu sana kumshawishi mtu kuzuia maumivu ambayo hata hana.
Hivyo wape watu kile wanachokitaka hasa, tibu maumivu yanayowanyima usingizi.

Mwisho kwenye eneo hili la maokoto, ni lazima uwe vizuri sana kwenye majadiliano.
Kwenye maisha hupati kile unachostahili, bali unapata kile unachokipambania.
Kuwa vizuri kwenye majadiliano na mapatano ili kuwashawishi watu wakupe kile unachotaka kutoka kwao.

Hapa tumekumbushana mambo yote muhimu tunayopaswa kuzingatia ili kukusanya maokoto mengi zaidi.
Tuendelee kuyafanyia kazi kwa umakini mkubwa, msimamo na kwa muda mrefu bila kuacha na ushindi utakuwa wetu kwa uhakika.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe