3160; Mafiga matatu.

Rafiki yangu mpendwa,
Hendry Ford hakuwa injinia.
Wala hakujua kitu chochote kuhusu fizikia.
Lakini alikuwa mmiliki wa kampuni ya magari.

Siku moja Ford alipata wazo.
Kwamba inawezekana injini ya gari ikawa na uwezo mkubwa zaidi.
Na hilo litawezekana kama injini itakuwa na pistoni 8 badala ya 6 zilizozoeleka.
Aliona hilo ni wazo bora kabisa.

Ford aliwaita mainjinia wake, na kuwapa hilo wazo.
Akawaambia nahitaji mtengeneze injini yenye pistoni 8 ma siyo 6 zilizozoeleka.
Mainjinia wakamjibu hilo ni jambo ambalo kifizikia haliwezekani kabisa.
Akawaambia nendeni mkatengeneze.

Baada ya muda akawaita tena mainjinia wake na kuwauliza maendeleo yao kwenye kazi aliyowapa yanaendaje.
Wakamwambia kama tulivyokueleza, haiwezekani kabisa kifizikia kuwa na injini yenye pistoni 8.
Ford aliwasikiliza kwa makini wakieleza kwa kujiamini jinsi wazo lake haliwezekani.
Walipomaliza kujieleza, aliwaambia; “Labda sijaeleweka vizuri, nataka injini yenye pistoni 8 na kama nyie hamuwezi kunipa hiyo injini nitatafuta watu wengine wa kufanya hii kazi.”

Mainjinia walitoka pale na baada ya muda wakarudi kwa Ford wakiwa na habari njema za injini yenye pistoni 8 badala ya 6.
Na hizo ndizo injini za V8 ambazo zinajulikana mpaka leo kwa uwezo wake mkubwa.

Hadithi hii ya kweli kabisa kuhusu Ford inatuonyesha mafiga makuu matatu yanayopaswa kuwepo ili biashara yoyote ile ifanikiwe.
Mafiga hayo ni WAZO, UTEKELEZAJI na MSUKUMO.
Biashara inapaswa kuwa na wazo au mawazo ya tofauti ambayo yanaitofautisha na biashara nyingine.
Mawazo hayo yanafanyiwa kazi kwa uhakika.
Na kunakuwa na msukumo kwenye pande zote, yaani wazo na utekelezaji.

Sasa basi, biashara nyingi zimekuwa zinashindwa kwa sababu mtu mmoja ndiye anayetaka kufanya mambo yote matatu.
Yaani awe na wazo, alitekeleze na yeye mwenyewe ajisukume kwenye maeneo yote mawili.
Hicho ni kitu ambacho kumekuwa hakitokei.
Inakuwa ni kama mtu kutaka kupika chakula kwenye jiko lenge figa moja.
Na wengi sana wamekwama hapo, licha ya kuwa na mawazo mazuri na ya tofauti.

Ili biashara iweze kuwa na mafanikio makubwa, inahitaji watu tofauti kwenye vipengele hivyo vitatu.
Biashara inakuwa inahitaji mafiga matatu ili kupika mafanikio.

Sehemu ya kwanza ni kuwa na mtu au watu wanaokuja na mawazo tofauti ya kibiashara. Hapo panafanyiwa kazi na uongozi wa biashara.
Mmiliki wa biashara pamoja na timu yake ya uongozi ndiyo inakuja na mawazo ya bora yanayoitofautisha biashara na washindani.

Sehemu ya pili ni kuwa na timu ya watu wanaotekeleza mawazo hayo, kwa kuyaweka kwenye matendo na kuzalisha matokeo. Hapa ndipo wafanyakazi wote wa biashara wanapoingia na matokeo makubwa wanayopimwa nayo ni mapato yanayoingia kwenye biashara.

Sehemu ya tatu ni kuwa na mtu au watu ambao wanasukuma sehemu hizo mbili kufanya kwa ukubwa na utofauti.
Kwa kuwa mazoea huwa ni rahisi kuingia kwenye mchakato wowote ule, sehemu ya tatu inavunja hayo mazoea kwa kuusukuma kila upande kwenda kabisa nje ya mazoea.
Sehemu hiyo ya tatu ndiyo ina makocha na washauri mbalimbali.

Mpaka hapo nadhani unapata picha jinsi tunavyokwenda hapa.

Wewe kama mmiliki wa biashara kazi yako ni kuja na mawazo ya kuiboresha zaidi biashara yako, iweze kukua na kuepuka ushindani.
Unapaswa kuielewa biashara yako na soko kwa kina ili kwenda vizuri na vyote.

Unapaswa kuwa na timu ambayo inatekeleza mawazo ya kibiashara unayokuja nayo.
Timu inapaswa kugeuza mawazo kuwa uhalisia.

Halafu mimi kama Kocha wako nipo kukusukuma wewe na timu yako.
Nakusukuma uje na mawazo bora kabisa ya kuikuza biashara, kwa kukutaka uwe na malengo makubwa kuliko ulivyozoea.
Na pia naisukuma timu yako itekeleze mawazo hayo kwa imani na kujituma zaidi mpaka yageuke kuwa unalisia.
Kama kocha sipaswi kuruhusu mazoea yoyote yatawale kwenye biashara. Kila wakati napaswa kusukuma zaidi kila upande ili matokeo bora na ya tofauti yazalishwe kwenye biashara.

Tukijenge vizuri mzunguko huu wa mafiga matatu, tutaweza kupika kitu kikubwa sana ndani ya biashara yako, ambacho watu hawataweza kuamini kimewezekanaje.

Je umejitoa kiasi gani kuhakikisha huu mpango wa mafiga matatu (WAZO, UTEKELEZAJI na MSUKUMO) unakwenda kufanya kazi kwa uhakika kabisa kwako?
Karibu ushirikishe kwenye maoni hapo chini.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe