3163; Mazoea na Kujisahau.

Rafiki yangu mpendwa,
Sisi binadamu tumeumbiwa kusahau.
Kusahau kumekuwa na manufaa makubwa sana kwetu kwani kumewezesha kuendelea na maisha licha ya mambo mbalimbali tunayoyapitia.

Kama tungekuwa tunakumbuka kila ambacho tumepitia kwenye maisha, tusingeweza kuwa na maisha tulivu.
Uzito wa kumbukumbu tunazokuwa nazo ungetuelemea sana kiasi cha kushindwa kufanya maamuzi sahihi kwetu.

Kusahau huko ambako kumekuwa na manufaa makubwa kwetu, kumekuwa pia na hasara.
Na hasara kubwa ya kusahau ni kujisahau kupitia mazoea ambayo mtu anakuwa amejijengea.

Kuna watu ambao unakuwa ulianza kushirikiana nao wakiwa kwenye hali fulani ya chini sana.
Hali hiyo ikawa inawasukuma sana kujituma kwenye kutekeleza wajibu wao.
Lakini kadiri muda unavyokwenda, watu hao wakawa wanabadilika.
Wanaacha kuweka juhudi kubwa ambazo walikuwa wanaweka tangu awali.

Kinachopelekea mabadiliko hayo kinakuwa ni mazoea na kujisahau.
Mazoea yanapotawala mtu anaacha kufanya kwa msukumo mkubwa aliokuwa nao awali, badala yake anafanya kwa sababu ndivyo amekuwa anafanya.
Na kujisahau kunamfanya mtu akose ile hofu ya kukosa au kupoteza aliyokuwa nayo awali na kuona hakuna kinachoweza kumsumbua.

Pale maamuzi yenye madhara kwa mtu yanapochukuliwa kwa mtu kwa sababu ya mazoea na kusahau kwake, anashangazwa sana na hilo.
Kwani anakuwa hakutegemea maamuzi ya aina hiyo yangeweza kufanyika.
Kwenye fikra zake anaona kila kitu kipo sawa kabisa, mpaka pale maamuzi yanapofanyika.

Unaweza kudhani kama mtu huyo angekumbushwa mara kwa mara basi angechukua hatua bora zaidi.
Lakini hilo siyo kweli, kwani mazoea na kusahau ni vitu vyenye nguvu kubwa sana. Hata ufanye nini, huwezi kuvivunja kwa nje ya mtu. Hayo ni lazima yaanzie ndani ya mtu mwenyewe.

Lakini pia unaweza kushawishika kwamba mtu amejifunza kwa maamuzi yenye madhara kwake yaliyofanyika. Hasa pale mtu anapoonekana kuumia na maamuzi yaliyofanyika, ambayo hakuwa anayategemea.
Unaweza kuona mtu amejifunza na hivyo kutengua maamuzi yaliyofanyika awali.
Lakini mambo huwa hayapo hivyo.
Mazoea na kujisahau ni hatua ya hatari sana kwenye maisha ya mtu.
Ni hatua ambayo mtu akishaifikia, ni vigumu sana kurudi nyuma.
Kwa sababu pamoja na changamoto anazokuwa nazo mtu, bado ataona tatizo siyo lake.
Ataona ni kama haeleweki hivi.
Na hivyo hata akipewa tena nafasi, atarudia yale yale aliyokuwa anafanya mpaka maamuzi yakafanyika juu yake.

Unapojiridhisha kwamba mtu hawezi tena kuendelea na kitu kwa sababu ya mazoea na kujisahau anakokuwa nako, simamia hilo.
Kwa sababu ndiyo lililo sahihi.
Unapofanya maamuzi halafu ukarudi tena kuyabadili, unachokuwa umeonyesha ni kwamba mtu huyo yupo sahihi na wewe ndiye uliyekosea.
Ndiyo maana haitamchukua mtu muda kurudi kwenye yale yale aliyokuwa anayafanya.

Unaweza kuwa unatamani sana kuendelea na mtu kwa muda mrefu. Lakini kama mazoea na kujisahau kumeshaingia ndani yake, hakuna kitu utakachoweza kukifanya kumbadili.
Mtu wa kubadilika huwa anaanza kubadilika ndani yake mwenyewe kupitia mwenendo wake mwenyewe anaokuwa anauona.
Kama inabidi mtu alazimishwe kutoka nje ndiyo abadilike, anakuwa hajawa tayari kwa mabadiliko na hivyo mabadiliko atakayoyafanya hayatadumu.
Bado ataendelea kuamini yeye ndiye yuko sahihi na wengine ndiyo wanaokosea.

Tumaini pekee unaloweza kuwa nalo kwa watu unaoshirikiana nao ni kuwakumbusha mara kwa mara na kuwasukuma wasiingie kwenye mazoea.
Lakini wakidhajisahau au kufanya kwa mazoea, huna tena namna ya kuwatoa kwenye hilo shimo.
Mazoea na kujisahau ni ugonjwa ambao mtu akishaupata ni hawezi tena kupona.
Unaweza kukingika, lakini kutibika huwa ni vigumu.

Jikumbushe sana hili muhimu kwako binafsi na kwa wote unaoshirikiana nao.
Hangaika sana na kinga kwa kukumbusha kila mara na kuvunja mazoea.
Lakini kujisahau na mazoea vikishaingia, umekwisha, hakuna tena unachoweza kufanya.

Kwenye changamoto hiyo ya mazoea na kujisahau, kinga ndiyo tiba yenyewe.
Kama kinga itashindwa kufanya kazi, hakuna tena tiba zaidi ya kifo.
Na kwa kifo ni kuchukua maamuzi magumu ambayo yataumiza pande zote, ila pia yatakuwa na manufaa kwa pande zote.

Kila wakati, kila mtu anapaswa kuwa anajisukuma kufanya vitu vipya na tofauti ili kuendelea kupiga hatua.
Lakini pia anatakiwa kuwa na hofu ya kupoteza, ambayo inamfanya akipambanie kitu kwa ukubwa zaidi.
Mtu akishakosa vitu hivyo viwili, hakuna namna anaweza tena kusaidiwa kuvipata.
Zingatia sana mambo hayo mawili kwako binafsi na kwa wote unaojihusisha nao ili kuweza kufanya makubwa unayotaka kuyafanya.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe