3166; Bakiza moja.

Rafiki yangu mpendwa,
Kwenye harakati za kujitafuta, nimewahi kufanya kilimo cha matikiti maji.
Nilishirikiana na rafiki yangu mmoja na tulijipanga vyema kuhakikisha tunapata matokeo mazuri.

Baada ya kuandaa shamba, kupanda na miche kuanza kutoa matunda, tulitafuta mtaalamu wa kilimo na kwenda naye shambani ili aangalie na kutushauri zaidi mambo ya kuzingatia ili tupate matokeo bora.

Mtaalamu alifika na kutushauri mambo mengi ya kuboresha. Jambo moja aliloshauri lilinishangaza na lilinipa somo kubwa ambalo nalikumbuka mpaka sasa na lina nguvu sana.
Alituambia kwa kila mche ambao umetoa tunda zaidi ya moja, tuondoe matunda yote ya ziada na kubakiza tunda moja tu.

Nilikuwa wa kwanza kupinga hilo, nikimwambia kwa nini tupunguze matunda hayo badala ya kuyaacha na kuwa na mavuno makubwa zaidi.
Alinijibu kwa utulivu kwamba kama tutaacha mche mmoja uwe na tunda zaidi ya moja, matunda yatakayotoka yatakuwa madogo madogo na sokoni tutapata bei ndogo.
Lakini kama tutaondoa matunda ya ziada na kubakiza tunda moja kwa kila mche, na kuhakikisha miche imepata maji ya kutosha, basi matunda yatakuwa makubwa na bei tutakayoipata sokoni itakuwa nzuri.

Ni kitu ambacho kilinipa funzo kubwa sana ambalo mpaka sasa nalitumia nje ya kilimo.

Huwa ni rahisi kujishawishi kwamba kadiri tunavyofanya mambo mengi kwa wakati mmoja ndivyo tunavyokuwa na uzalishaji na ufanisi mkubwa.
Lakini kwenye uhalisia mambo ni tofauti.
Tunapofanya mambo mengi, tunatawanya nguvu zetu na hatimaye kuishia kupata matokeo madogo madogo na yasiyokuwa na tija.
Kama tungepeleka nguvu zote kwenye kitu kimoja, matokeo ambayo tungepata yangekuwa makubwa na yenye tija zaidi.

Asili ina mifano mingi ya kutufunza kwenye hilo.
Hata mimea mingine, kadiri inavyokuwa na matawi mengi, ndivyo uzalishaji wake unakuwa madogo. Ndiyo maana mara kwa mara inatakiwa kupunguzwa matawi, ili yabaki machache ambayo yatazalisha vizuri.

Tukiliangalia jua pia linatupa funzo kubwa kwenye eneo hilo.
Mwanga wa jua ukitawanywa kwenye eneo kubwa, unaishia tu kuwa mwangaza.
Lakini mwanga huo huo ukielekezwa eneo moja kwa uhakika, huwa unakuwa moto mkali na unaochoma.

Kadhalika kwa mvua, matone mengi ya mvua yanaishia kulowesha eneo kubwa.
Lakini tone moja linaloanguka kwenye mwamba kwa muda mrefu bila kuacha, huwa linavunja kabisa huo mwamba.

Rafiki, yote hayo ni kutaka kukusisitiza kwa kuwa tumeshajipata, nguvu zetu zote tunaziweka kwenye kitu kimoja kwa wakati mmoja.
Kwenye kujenga biashara, tunaijenga moja peke yake kwanza.
Ni mpaka pale inapoweza kujiendesha bila kututegemea moja kwa moja ndiyo tunaweza kuiacha na kwenda kuanzisha au kufanya biashara nyingine.

Lakini kabla ya kufikia hatua hiyo ya biashara kuweza kujiendesha yenyewe, hatutafanya kitu kingine chochote cha kuingiza kipato isipokuwa biashara hiyo tu.
Tunajua zitaendelea kuja kwetu fursa nyingi zinazoonekana ni nzuri na zinazoweza kutupa matokeo makubwa na ya haraka.
Lakini tunajua vyema kwamba tukishatawanya tu nguvu, tunaishia kupata matokeo madogo kwenye maeneo yote.

Tunajua biashara moja tuliyochagua kufanya tukiipa umakini wote na kuiwekea juhudi kubwa, ina nguvu ya kutupa matokeo makubwa sana tunayoyataka.
Hivyo tunapaswa kusema HAPANA kwa mengine yote yanayotushawishi kufanya kwa sababu tunayaona ni rahisi au yatatupa matokeo makubwa.

Kwenye hatua hii ya kuwa tumejipata kwenye hii safari, futa shughuli nyingine zote unazofanya za kuingiza kipato na baki na moja pekee.
Hata kama hizo nyingine zinaonekana kuwa na fursa nzuri.
Chagua moja ambayo ukiiwekea kila kitu ulichonacho itakupa matokeo makubwa zaidi.
Halafu basi, muda wako wote, nguvu zako zote na umakini wako wote unaweka kwenye hicho kimoja ulichochagua.
Usijibanie kwa namna yoyote ile.
Fanya kwa namna ambayo hutakuwa na majuto kwamba kuna kitu hukufanya.

Na kama tunavyojua kwa uhakika kabisa kwamba hakuna juhudi zinazowekwa mahali na zikapotea bure.
Hivyo tuamini kwenye kitu hicho kimoja na kukiwekea juhudi zote kabisa.
Ni lazima tutapata matokeo bora kabisa.

Na kama kuna mengine ambayo unapenda kuyafanya, kwa sababu ndiyo ndoto au mapenzi yako, utakuja kuyafanya baadaye.
Kwanza simamisha kile kinachoweza kujiendesha chenyewe bila kukutegemea na hapo utakuwa huru kuendelea na vitu vingine.
Lakini kama hujaweza kusimamisha kitu kimoja kwa uhakika, hupaswi kuwa unahangaika na kitu kingine chochote isipokuwa hicho kimoja.

Umeshajipata, futa vyote ulivyokuwa unagangaika navyo na ubaki na kimoja.
Jenga hicho kimoja kwa mafanikio makubwa ndiyo uende kwenye vingine.
Usijidanganye kwamba una akili au ujanja kuliko asili.
Fuata asili kwenye hili na utapata matokeo bora kabisa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe