3168; Lugha pekee tunayoielewa hapa.

Rafiki yangu mpendwa,
Kuna lugha nyingi ambazo huwa zinaongelewa na wengi.
Lakini hapa kwenye programu yetu ya Bilionea Mafunzoni, tunaielewa lugha moja pekee.

Ni lugha ambayo sote tumeikubali na ndiyo tunaipambania katika mambo yote tunayoyafanya.
Ni lugha ambayo inatuwajibisha kwenye kila kitu tunachokifanya kwenye hii safari.

Ndiyo lugha ambayo tunahukumu nayo kila kitu kwenye maisha yetu.
Hatua zote tunazochukua tunazipima kwa hiyo lugha na kupambana kuboresha matokeo tunayoyapata.

Lugha ninayoiongelea ni ushindi.
Hiyo ndiyo lugha pekee tunayozungumza na kuielewa hapa.
Kila siku yetu tunaipima kwa ushindi kiasi gani tumepata.
Kwa sababu kila siku ni siku ya ushindi.
Na ushindi kwenye maisha ni mkusanyiko wa siku nyingi za ushindi.

Tunajua hakuna siku moja tutakayoamka na kujikuta tumepata ushindi mkubwa.
Bali ushindi tunakuwa tunautengeneza kila siku hatua kwa hatua.
Kila tunachofanya kwenye kila saa na kila dakika ya kila siku yako inaathiri ushindi wako.

Ni muhimu sana kuanzia hapo ili kuweza kujenga ushindi mkubwa kwenye maisha yetu.
Kwa kwenda hatua kwa hatua,
Tukikusanya ushindi kila siku.

Yote niliyoeleza hapa hakuna ambacho ni kipya na kisichoeleweka.
Lakini bado wengi sana sivyo tunavyoziendea siku zetu.
Bado ndani yetu tunaamini kuna mahali ushindi umejificha.
Mahali pa siri ambapo tukipagundua basi tutapata ushindi mkubwa na wa haraka.

Ni huo ubishi wa watu ndiyo umepelekea wengi kutapeliwa, kuibiwa na kupoteza muda na fedha nyingi.
Hayo huwa yanatokea pale tunapojikuta tumefuata mkumbo wa kundi la wengi ambao wanatafuta ushindi rahisi na wa haraka.
Kitu ambacho hakijawahi kuwepo.

Mambo ya msingi ya kufanya ili kupata ushindi ni yale yale.
Kinachohitajika ni kuyarudia rudia kwa msimamo kila siku bila kuyachoka.
Wengi huwa wanachoka haraka sana kwenye kurudia mambo yale yale.
Hivyo hunasa kwa haraka sana kwenye mambo mapya na ya kusisimua mara zote.

Na hapo ndipo mimi ninapoingia.
Wajibu wangu ni kukupa wewe ushindi.
Nimejitoa kuhakikisha wewe unakaa kwenye mchakato sahihi wa kukusanya ushindi wako wa kila siku.
Ili uweze kukusanya siku nyingi za ushindi (kila siku) ambazo ndiyo zitajenga maisha ya ushindi.

Na ili kuhakikisha hilo linatokea bila ya shaka yoyote, nipo tayari kufanya kila kinachopaswa kufanyika ili upate ushindi wako.

Nahakikisha mara zote unapata maarifa sahihi ya kukuwezesha kufanya maamuzi bora.

Nahakikisha mara zote unafanya maamuzi yaliyo bora.

Nahakikisha unatekeleza maamuzi yote uliyoyafanya kwa msimamo bila ya kuacha.

Nahakikisha unakaa kwenye mchakato bila ya kuyumbishwa na mengi yanayokuzunguka.

Nahakikisha unashirikiana vizuri na wengine katika mchakato mzima.

Ili kuhakikisha yote hayo yanatimia, nipo tayari kukuzingua kwa namna yoyote ile pale unapokwenda tofauti na lugha yetu kuu ya ushindi.

Nakukatalia pale unapotaka kuutoroka mchakato kwa sababu zozote zile.

Nakukatalia pale unapojipa sababu kwa nini mchakato unakushinda.

Nakukatalia pale unapofanya kwa mazoea na kukubali matokeo ya kawaida.

Kama utapenda hili itakuwa vyema, safari itakuwa rahisi.
Na hata kama hutalipenda, angalau uliheshimu na kufanyia kazi.
Kama utakuwa na tamaa kwenye hili itapendeza.
Lakini hata kama utakosa tamaa, hofu inatosha.

Hata kama hupendi, heshimu.
Hata kama hutamani, hofia.
Kwa namna hiyo tutaweza kuvuka mitego ambayo imewakwakisha wengi sana kwenye hii safari.
Kama unataka kuwa vile unavyotaka kuwa na usibabaishwe na yeyote, tayari hii safari kwa huu mpango inakuwa imekushinda moja kwa moja.

Tumekuwa tunajadiliana haya kila siku.
Tumekuwa tunapeana yote tunayopaswa kuyafanya na kwa namna ya kuyafanya.
Lakini bado kuna ambao wanajichagulia kufanya yale wanayojisikia kufanya wao.
Wanaamua ni yapi ya kimchakato watayafanya na yapi hawatayafanya.

Wanataka kuendelea na majaribio ambayo yameshashindwa kwenye maisha yao.
Kwa kipindi kirefu cha hayo maisha wamekuwa wanahangaika na mengi.
Na hakuna hatua kubwa walizopiga.
Wamepoteza muda mwingi na hawana cha kuonyesha.
Lakini kutulia kwenye mchakato kamili na sahihi kwa muda wanaona kama wanapoteza muda.
Na kwenda kuhangaika na vitu vipya na vya kusisimua.

Hiyo ndiyo kitu ambayo ninaikataa kwa kila namna kwenye huu mchakato wetu.
Ni tunaufuata mchakato kama ulivyo kwa ukamilifu wake.
Au tunaachana nao moja kwa moja.
Hakuna njia ya kati.
Hakuna uvuguvugu.
Unazama ndani mazima au unatoka nje.
Unayaoga maji au unaachana nayo.
Unainywa dawa au unaachana nayo.
Hakuna kupoteza muda kwa majaribio ambayo yameshashindwa.
Tupo kwenye safari ya uhakika na tunakaa kwenye hiyo kwa kila namna.

Ninachotaka na nilichodhamiria ni kukupa ushindi.
Ushindi wa uhakika.
Kwa kufanya kila kinachopaswa kufanyika.
Ili upate ushindi.
Lakini kama hujautaka hasa ushindi.
Kama hujajitoa hasa ili kuupata ushindi.
Kama unapenda kutoa sababu.
Huu mpango hautafanya kazi kwako.
Unapoteza tu muda wako.

Ili huu mpango ufanye kazi vizuri.
Ni unafuata mchakato mzima kama tulivuouweka.
Au unafanya kile kilicho bora zaidi ya mchakato uliopo.
Chini ya hapo, haitafanya kazi.
Hatuna haja ya kudanganyana kwenye hilo.

Je wewe umejitoa kiasi gani kuhakikisha kweli kila siku inakuwa ya ushindi kwako kwenye huu mchakato tuliouchagua?
Upo tayari kutoa ushirikiano kiasi gani kwangu katika kuhakikisha natimiza wajibu niliojipa wa kukupa wewe ushindi?
Jibu kwenye sehemu ya maoni hapo chini.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe