3172; Uhuru na Raha.

Rafiki yangu mpendwa,
Watu wengi huwa wanachagua kuingia kwenye biashara na ujasiriamali ili kupata uhuru na raha.
Wanataka uhuru wa kuyaendesha maisha yao kwa namna wanavyotaka wao na raha ya kufanya mambo yao kwa namna wanavyojisikia.

Kitu ambacho wanakuwa hawakijui ni kwamba uhuru na raha huwa haviendi pamoja.
Kufanya biashara au ujasiriamali ni kuchagua kupata uhuru kwa kukosa raha.
Yaani ili uwe huru, ni lazima uachane na kutaka raha.

Hiyo ni kwa sababu uhuru huwa unakuja na uwajibikaji mkubwa.
Kuna mambo mengi ambayo unajikuta ukiwajibika kuyafanya ili uwe huru.
Mambo hayo yanaweza yasikupe raha, lakini lazima yafanyike.

Watu wengi wanapokuwa wanaanza biashara zao huwa wanajituma sana.
Kitu ambacho kinawaletea mafanikio kiasi fulani.
Kwa mafanikio hayo, watu hao wanaona ni wakati wa kuacha kujitesa kwa hizo juhudi walizoweka na kuanza kupata raha.
Na hapo ndipo anguko kubwa sana linapoanzia.

Pale watu wanapoanza kujipa tu raha, kwa kuachana na juhudi kubwa zilizowafikisha kwenye ngazi fulani ya mafanikio, ndiyo anguko linapoanza na hatimaye kupoteza uhuru.

Kuendesha biashara yenye mafanikio ni sawa na kuendesha baiskeli.
Unapoanza kuendesha baiskeli huwa inayumba yumba, kisha inakaa sawa.
Na ili iendelee kuwa sawa, lazima iendelee kuchochewa pia. Kadiri inavyokuwa kwenye mwendo, ndivyo inavyokuwa imara.
Lakini baiskeli inapoachwa kuchochewa inaanza kuyumba na hatimaye kuanguka.
Hivyo ndivyo biashara pia zilivyo.
Haijalishi umepiga hatua kiasi gani, juhudi zaidi zinaendelea kuhitajika.
Huwezi tu kujiamulia kufanya vile unavyojisikia wewe.

Kinachoua biashara nyingi ni kujisahau kwa wamiliki wa biashara.
Pale wanapotaka kupata raha baada ya kufikia uhuru fulani, ndiyo wanaanza kuanguka.

Kama umechagua maisha ya kupata uhuru na mafanikio makubwa, jua wazi kwamba umeamua kuachana na raha.
Siyo kwamba maisha yako yote yatakuwa ya mateso, bali ni hakuna wakati utafika na kuona umeshamaliza kila kitu.
Kwani kwa kila hatua unayofikia, juhudi zaidi zinakuwa zinahitajika ili kuendelea kubaki kwenye kilele cha mafanikio unayokuwa umefikia na hata kusonga mbele zaidi.

Huwezi kupata uhuru na mafanikio makubwa kama hautakubali kuachana na raha ya mazoea.
Ukishachagua maisha ya uhuru na mafanikio maana yake umechagua mapambano yasiyo na mwisho.
Kama mwezi mmoja mambo yameenda vizuri, haimaanishi na mwezi unaofuata mambo pia yataenda vizuri yenyewe.
Bali unahitajika kujipanga na kuweka juhudi kubwa zaidi ili mwezi unaofuata matokeo yaendelee vizuri.

Anguko kwa wengi huanzia pale wanapodhani wakishafika hatua fulani basi ndiyo wamefika, hawawezi kuipoteza.
Kitu ambacho siyo kweli.
Kila hatua ni ya kupambania kombe.
Ukizubaa tu umelipoteza kombe na kunyang’anywa ushindi.

Kwenye hii safari ya mafanikio pia, kujiona mjanja ni hatari kubwa sana.
Kuona labda una upekee fulani ambao unakupa faida dhidi ya wengine ambao hawana ni kujiandaa na anguko.
Ni kweli unahitaji kuwa na kitu cha tofauti na wengine, lakini lazima ukifanyie kazi kwa uhakika ndiyo uweze kunufaika nacho.

Changamoto kubwa ya sisi binadamu ni kuzoea vitu haraka.
Wakati tunaanza tunakuwa na msukumo mkubwa.
Tukishafika ngazi fulani ya mafanikio tunazoea na kutaka kupata raha.
Tunaanza kupunguza juhudi za kazi tulizokuwa tunaweka.
Tunaanza kuwa na matumizi makubwa ambayo yanatutoa kabisa kwenye ufanyaji.
Tunajiona tunayastahili mafanikio tuliyoyapata, ni yetu milele.
Na hapo ndipo anguko kubwa sana linapojitokeza na watu kupotea kabisa kwenye ramani ya mafanikio.

Kwenye safari ya mafanikio kwenye maisha, kupitia kuanzisha na kukuza biashara, hakuna kipindi ambacho juhudi hazihitajiki tena.
Hakuna taji la milele.
Kila wakati ni wa kupambania kombe.
Kila hatua ni ya kuweka juhudi kubwa zaidi ili hata tu kubaki pale mtu unapokuwa.

Usilete mazoea kwenye hii safari.
Usitake raha.
Kama umechagua kupata uhuru, jua umechagua kuachana na raha.
Endelea na mapambano kila wakati.
Na juhudi unazoweka ndiyo zinazoendelea kukuweka huru.
Jichunge sana kwenye kazi na matumizi.
Kila wakati weka kazi kubwa zaidi badala ya kuwa na matumizi zaidi.

Kama kujua haya kumekuumiza.
Kama ulikuwa kwenye hii safari ukiamini baada ya haya mateso basi ni raha mustarehe kama inavyokuwaga kwenye hadithi na simulizi nyingi.
Basi jua umepotea njia.
Amua sasa kuchagu uhuru kwa kuachana na raha.
Au kama unachotaka ni raha, basi kubali kutokupata uhuru mkubwa.
Rudi kufanya kazi chini ya mwingine ili kutokuwajibika kw viwango vikubwa.

Kupata uhuru na mafanikio makubwa, lazima uendeshe mapambano makubwa na yasiyo na ukomo.
Watu huwa wanachanganya uhuru wa mafanikio na kutokufanya.
Kwamba pale wanapokuwa wamefikia uhuru wa kifedha na kibiashara basi wanaacha kufanya.
Kitu ambacho kinakaribisha anguko kubwa.

Kufanya ni zoezi endelevu kama unataka uhuru na mafanikio makubwa.
Kubali hilo na mambo yako yatakwenda vizuri.
Lakini ukianza kukimbizana na raha, utakuwa umekaribisha matatizo makubwa wewe mwenyewe.

Kila wakati ni wa kupambania kombe.
Ukileta tu mazoea na kutaka raha, unakuwa umepoteza kila ulichokuwa umekipata.
Kamwe usiruhusu hilo.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe