3173; Ufunguliwe au uvunje.

Rafiki yangu mpendwa,
Kama unapita mahali usiku, ambapo pana wanyama hatari na ghafla ukasikia mnyama mkali anakujia.
Ukakimbia mpaka ukakutana na nyumba, ambayo mlango umefungwa.
Unadhani ni nini utafanya ili uweze kujitoa kwenye hatari uliyopo?

Bila shaka ni utagonga huo mlango ili uweze kufunguliwa na uondokane na hatari inayokuwa inakukabili.
Na vipi kama unagonga ila hakuna anayefungua, huku mnyama mkali akizidi kukusogelea?
Hapo itabidi uvunje huo mlango na kuingia ndani.

Ukweli ni kwamba kama utagonga mlango bila kuchoka, kuna mtu ataufungua au la mlango huo utavunjika.
Lakini sivyo mambo yanavyokuwa kwa walio wengi.
Kwani wanapogonga mlango mara chache na usifunguliwe, wanaachana nao na kwenda kwenye mlango mwingine.
Na pale huo mwingine nao unakataa, wanauacha na kwenda pengine tena.

Hivyo ndivyo watu wanakuja kushtuka wamegusa vitu vingi juu juu na hakuna chochote ambacho wamezama ndani mpaka wakapata matokeo bora na ya tofauti.
Na hilo ndiyo limekuwa linawakwamisha wengi kufanikiwa.

Watu wengi wamekuwa wanaona kwamba hawafanikiwi kwa sababu mambo ni magumu.
Lakini ukweli ni kwamba hawafanikiwi kwa sahahu wanakata tamaa haraka.
Hawajitoi vya kutosha na kwa muda mrefu.
Hawadhamirii kwenye kitu kimoja mpaka watakapopata kile wanachotaka.

Mwenendo wa wengi ni kama mvua, matone mengi yaliyosambaa kwenye eneo kubwa, ambayo yanaishia kulowesha.
Lakini kama tone moja litadondoka kwenye mwamba kwa kujirudia rudia, mwamba huo utavunjika.

Kama umechagua kuweka nguvu mahali, jitoe hasa kuhakikisha nguvu hizo unaziweka kwa msimamo na kwa muda mrefu mpaka zizalishe matokeo ya tofauti.
Kama hujapata matokeo unayotaka, siyo kwa sababu matokeo hayo hayawezekani, bali kwa sababu hujayapambania vya kutosha.

Mapambano ni mpaka upate kile unachotaka na siyo chini ya hapo.
Mapambano ni kufanya kila kinachopaswa kufanyika na siyo tu kufanya kilicho ndani ya uwezo wako.

Wakati mwingine watu wanashindwa kwa sababu hawana hatari kubwa ambayo inawakabili kama watashindwa.
Kwa maneno mengine watu wanakuwa kwenye eneo la faraja kwao, ambalo halina hatari yoyote kwao.
Ndiyo maana wanakuwa na anasa ya kuhama kutoka eneo moja kwenda jingine.
Unapokuwa unakabiliwa na hatari kubwa, utajitoa hasa kwenye kile ambacho ndiyo ukombozi wa hatari hiyo kwako.

Kama umeshajigundua umekuwa mtu wa kuhangaika na mambo mengi kwa juu juu bila kuzama ndani na kupata matokeo makubwa na ya tofauti, unapaswa kujiweka kwenye hatari itakayokulazimisha ukae kwenye jambo moja kwa muda mrefu mpaka upate matokeo unayoyataka.

Unapojitoa kweli kweli ili ukipate kitu, ni lazima utakipata.
Dunia haiwezi kumzuia mtu aliyedhamiria hasa kupata kile anachokitaka.
Hakikisha unapata kile unachotaka kwa kuweka dhamira ya kweli na kujiweka kwenye hatari ambayo huwezi kutoroka.
Hakuna njia nyingine ya uhakika zaidi ya hiyo.

Gonga mlango mpaka ufunguliwe.
Na usipofunguliwa kabisa, uvunje.
Unachotaka ni kuingia ndani.
Hakuna kinachopaswa kukuzuia.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe