Barua ya XIX; Kuhusu mambo ya kidunia na kustaafu.
Rafiki yangu Mstoa,
Maisha yetu hapa duniani ni ya mahangaiko, tangu tunazaliwa mpaka tunakufa.
Kwenye kila hatua ya maisha kunakuwa na mambo ambayo tunayahangaikia.
Na hilo limekuwa halina mwisho.
Kwa watu wengi wasiokuwa na uelewa au falsafa wanayoiishi, maisha yao yote huwa ya mahangaiko.
Hata pale wanapopambana na kupata walichotaka, bado hawawezi kutulia, kwani wanajikuta wakitaka zaidi.
Mwanafalsafa Seneca aliliona hilo kwa wengi na kwenye barua yake ya 19 kwa rafiki yake Lucilius alieleza kwa kina kuhusu kustaafu.
Alimweleza umuhimu wa kufikia hatua ya kuridhika na yale ambayo mtu ameshafanikisha na kuwa na mwisho wa maisha wenye utulivu mkubwa.
Karibu tujifunze kuhusu hilo la kustaafu na mambo mengine ya kuzingatia ili kuwa na maisha bora na yenye mafanikio na utulivu.
1. Unapofika wakati wa kustaafu, fanya kwa utulivu.
Seneca anamwambia rafiki yake kwamba baada ya mahangaiko mengi ya maisha, unafika wakati ambapo mtu anahitaji kupumzika.
Huo unakuwa ni wakati ambao hawezi tena kuendelea na mikiki mikiki aliyokuwa nayo kwa kipindi chote cha maisha yake.
Lakini pia wengi wanapofikia hatua ya kustaafu huwa wanafanya hivyo kwa kelele nyingi. Wakichukulia kama ni tukio kubwa na kila mtu anapaswa kujua hivyo.
Seneca anaeleza siyo mpango mzuri kufanya kustaafu kwako kuwa tukio ambalo kila mtu analijua.
Badala yake unapaswa tu kupunguza mambo yanayokupa usumbufu mkubwa kwenye maisha yako.
Yaani watu wanatakiwa wajue tu kwa kuwa umri wako umeenda basi kuna mambo hawawezi kukutegemea tena kama awali.
Kwa njia hiyo kustaafu kwako kunakuwa kwa kawaida badala ya kuwa kwa usumbufu kwa wengine.
Hatua ya kuchukua;
Kwetu sisi tumechagua kufanya kile tunachofanya kwa kipindi chote cha maisha yetu.
Lakini kadiri muda unavyokwenda ndivyo tunavyoendelea kupunguza mengi yasiyokuwa na umuhimu.
Tunabaki na yale muhimu tu, ambayo pia tunafurahia kuyafanya.
Na huko ndiyo kustaafu kwetu, kubaki tukifanya yale tu tunayofurahia kuyafanya.
Hatupigi kelele na mtu kwamba tumestaafu, wao wanatuona tu tukihamishia umakini wetu kwenye mambo machache ya msingi.
Nukuu;
“Surely there is nothing in this that men can begrudge us. We have spent our lives on the high seas; let us die in harbour.” – Seneca
“Kwa hakika hakuna chochote ambacho watu wanaweza kutuchukia nacho kwenye hili [kustaafu]. Tumetumia maisha yetu baharibi; wacha tufie bandarini.” – Seneca
2. Unaoona huwezi kuwaacha, wapo tayari kukuacha muda wowote.
Seneca anaendelea kueleza kwamba kinachowafanya wengi wasiwe tayari kustaafu ni kuona kwamba bado wanahitajika na kutegemewa na wengine.
Wanaona kuna watu ambao hawawezi kuwaacha na hivyo kuendelea kufanya shughuli zao, hasa wasizozipenda na kwa umri ambao umeshaenda sana.
Seneca anatukumbusha kwamba wale tunaoona hatuwezi kuwaacha, huwa wapo tayari kutuacha muda wowote.
Anaeleza kwamba watu wapo na wewe siyo kwa sababu yako, ila kwa sababu zao wenyewe.
Yaani watu wengi wanaoambatana na wewe ni kwa sababu ya maslahi yao binafsi. Siku ambayo hawapati maslahi hayo, wataachana na wewe mara moja, bila ya kujali umejitoa kiasi gani kwa ajili yao.
Hapa kuna funzo kubwa sana ambalo Seneca anatukumbusha, tunaweza kujitesa sana kwenye maisha yetu kwa ajili ya watu wengine. Tukidhani na wao wanajitoa kwa ajili yetu pia.
Ni mpaka pale tunapokuwa na uhitaji mkubwa kutoka kwao ndiyo tunaujua ukweli, kwamba walikuwa nasi kwa manufaa yao binafsi.
Seneca anatoa mfano kwamba hata muuzaji anayempitia mteja kila siku kumuuzia, siku akikuta hayupo anaenda kwa mteja mwingine.
Hivyo ndivyo maisha yalivyo, tunapaswa kuweka kipaumbele cha kwanza kwetu wenyewe, kwa sababu ndivyo wengine pia wanavyofanya.
Tusije kujitesa kwenye maisha yetu kwa ajili ya wengine, kwa kutegemea nao wajitese kwa ajili yetu.
Hatua ya kuchukua;
Kipaumbele cha kwanza kwenye maisha yako kinapaswa kuwa kwako wewe mwenyewe. Shirikiana vizuri na wengine, wape yale unayochagua kuwapa, lakini usije ukajisahau kwamba watu wapo kwa maslahi hao binafsi. Na hakuna ubaya wowote kwenye hilo, ni wewe tu usijisahau na baadaye kuja kuumia.
Nukuu;
“For what will you leave behind you that you can imagine yourself reluctant to leave? Your clients? But none of these men courts you for yourself; they merely court something from you.” – Seneca
“Kwani ni kitu gani ambacho hutaki kukiacha nyuma? Wateja wako? Hakuna kati yao aliye na wewe kwa sababu yako; bali wapo na wewe kwa maslahi yao binafsi.” – Seneca
3. Vitu vikubwa vina gharama kubwa.
Kila kitu kwenye maisha huwa kina gharama ambayo tunaingia ili kukipata.
Na kadiri kitu kinavyokuwa kikubwa na muhimu, ndivyo gharama yake inavyokuwa kubwa pia.
Kwenye dhana ya kustaafu, Seneca anaeleza jinsi inavyokuja na gharama kubwa.
Kwa sababu ya mambo mengi ambayo mtu unakuwa umeyafanya, unaona ugumu kuyaacha, kwa sababu ni kama unakuwa umepoteza.
Huenda ni fursa fulani kubwa unayokuwa umeipata au wadhifa fulani.
Pale unapolazimika kuachana na yale yanayokusumbua, unaweza kuona ni gharama kubwa kwako kuacha hayo uliyoyapambania kwa muda mrefu.
Kuvuka hilo, Seneca anatutaka tujiulize kama tupo tayari kupoteza nafsi zetu au kupoteza hivyo ambavyo tumepata.
Hapo ndipo sasa unapochagua gharama ya kulipa.
Kama upoteze ulivyopata ila uokoe nafsi yako.
Au upoteze nafsi yako ila ubaki na ulivyopata.
Kwa sababu mwisho wa siku hakuna utakachoondoka nacho, kuwa tayari kulipa gharama ya kupoteza baadhi ya vitu ulivyopata ili uweze kubaki na utulivu wa nafsi yako.
Hatua ya kuchukua;
Inapofika hatua ya kuchagua kati ya nafsi yako na vile ulivyopata, mara zote chagua nafsi yako. Kwa kuweka kipaumbele kwenye nafsi utabaki na maisha tulivu, hata kama utapoteza vingine.
Lakini ukichagua kupoteza nafsi ili kubaki na vitu, hutaweza kuvifurahia kwa sababu utakosa utulivu.
Nukuu;
“Great things cannot be bought for small sums; so reckon up whether it is preferable to leave your own true self, or merely some of your belongings.” – Seneca
“Vitu vikuu haviwezi kununuliwa kwa gharama ndogo; piga hesabu kama utachagua kupoteza nafsi yako au baadhi ya vitu ulivyonavyo.” – Seneca
4. Matamanio hayana mwisho.
Kutamani kupata zaidi au kwenda ngazi z juu zaidi ni sababu nyingine inayowazuia watu wengi wasiwe tayari kustaafu.
Hiyo ni kwa sababu wanajiona wakiwa karibu zaidi na kupata kile walichokitaka sana.
Wasijue kwamba hata wakishakipata, bado watakuwa na matamanio mengine.
Hivyo dawa siyo kusubiri mpaka usiwe na matamanio kabisa, hilo halitatokea.
Bali unapaswa kufika mahali na kusema imetosha ili uweze kuacha kukimbizana na hayo matamanio yasiyokuwa na mwisho.
Seneca anasisitiza ni muhimu mtu kufikia hatua ambayo unaridhika na pale ulipofika kwa sababu ndiyo njia pekee ya kuwaridhisha wengine pia.
Anaeleza kwamba tunapochagua kustaafu, tunaachana na mambo mengi na kubaki na mambo machache, lakini yanayoturidhisha, badala ya kuhangaika na mengi yanayotusumbua.
Hatua ya kuchukua;
Kumbuka matamanio hayana mwisho. Unapofika hatua ya kupunguza mambo, jiambie imetosha na chukua hatua.
Ukijiambia unasubiri mpaka ukamilishe vitu fulani, jua hutafanya.
Nukuu;
“Prosperity is not only greedy, but it also lies exposed to the greed of others. And as long as nothing satisfies you, you yourself cannot satisfy others.” – Seneca
“Mafanikio siyo tu yanaleta tamaa, lakini pia yanatuweka kwenye tamaa za wengine. Na kama hujaridhika wewe mwenyewe, huwezi kuwaridhisha wengine.” – Seneca
5. Changamoto zipo hata kwenye ngazi z juu.
Huwa tunadhani kwamba mtu anapopanda ngazi za juu basi anakuwa hana tena changamoto.
Ukweli ni kwamba hata mtu upande juu kiasi gani, changamoto huwa haziishi, bali zinabadilika.
Kadiri unavyokwenda juu zaidi, ndivyo changamoto pia zinavyokuwa kubwa zaidi.
Seneca anamnukuu mwanafalsafa Maecenas ambaye anafananisha changamoto kwenye maisha na mlima, kwenye kilele cha mlima kuna hewa safi, lakini pia kunakuwa na radi kali.
Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye maisha, tunapokuwa na changamoto fulani, tunakazana kwenda juu zaidi tukidhani tutakuwa tumezikwepa kabisa changamoto.
Lakini matokeo yake tunakuwa tumezalisha changamoto nyingine mpya kabisa.
Hatua ya kuchukua;
Kumbuka changamoto za maisha hazina mwisho. Unapotatua changamoto za chini na kupanda juu, unakuwa umekaribisha changamoto nyingine za juu zaidi.
Nukuu;
“There’s thunder even on the loftiest peaks.” – Maecenas
“Huwa kuna radi hata kwenye vilele vya juu zaidi.” – Maecenas
6. Chagua marafiki kwa usahihi.
Seneca anamalizia barua hii kama ambavyo huwa anamalizia barua zake kwa kumnukuu mwanafalsafa Epicurus.
Kwenye nukuu ya barua hii Epicurus anasisitiza umuhimu wa kuchagua marafiki kwa usahihi.
Anasema ni muhimu kuchagua kwa usahihi watu unaokula nao kuliko unavyochagua nini ule.
Kwa sababu kula nyama bila ya marafiki sahihi ni sawa na maisha ya simba au mbwa mwitu.
Seneca anasema wakati pekee wa kupata marafiki sahihi ni pale unapokuwa umeachana na mambo mengi yanayokusumbua.
Kwani wakati upo kwenye mapambano, utakutana na wengi, lakini haitakuwa rahisi kujua wapo kwa ajili ya urafiki au kwa maslahi yao binafsi.
Hatua ya kuchukua;
Jenga marafiki sahihi ili uweze kuwa na maisha bora. Kwa sababu ni kupitia marafiki wa kweli ndiyo unaweza kuwa na maisha bora na tulivu, yasiyokuwa na upweke.
Nukuu;
“You must reflect carefully beforehand with whom you are to eat and drink, rather than what you are to eat and drink. For a dinner of meats without the company of a friend is like the life of a lion or a wolf.” – Epicurus
“Unapaswa kutafakari kwa umakini nani unakula na kunywa naye kuliko nini unakula na kunywa. Kwa sababu chakula bila ya marafiki sahihi ni kama maisha ya simba au mbwa mwitu.
7. Urafiki haununuliwi.
Seneca anahitimisha barua hii kwa kusisitiza jambo muhimu sana kwenye urafiki, ambalo wengi hulipuuza na kuwagharimu.
Anasema urafiki hauwezi kununuliwa kwa kitu chochote kile.
Anaeleza kwamba watu walio ‘bize’ na shughuli zao huwa wanadhani wale wanaowazunguka ni marafiki zao, wakati wao wenyewe hawawachukulii kama marafiki.
Wanadhani kwa kuwa wanawasaidia watu basi ni marafiki zao.
Seneca anasisitiza hakuna kitu kinaua urafiki kama misaada.
Yaani pale unapowasaidia sana watu kwa namna ambayo hawawezi kukulipa, wanaishia kukuchukia ndani yao.
Nje wataonekana kukupenda na kukuthamini, kwa kuwa ni tegemezi kwako, ila ndani yao watakuwa wanakuchukia kwa sababu wanajiona wakiwa na deni kwako na ambalo hawawezi kulilipa.
Hivyo ili kujenga urafiki sahihi, weka pembeni mambo ya kusaidiana kifedha na mali ambayo yanajenga zaidi utegemezi.
Urafiki unakuwa mzuri pale kila upande unapokuwa huru na kufurahia mahusiano hayo na siyo upande mmoja kuwa unatoa na mwingine kuwa unapokea mara zote.
Kuwa na marafiki ambao wote mnaweza kujitegemea na mnahusiana na kushirikiana kwa uhuru badala ya utegemezi wa lazima.
Hatua ya kuchukua;
Jenga urafiki na watu ambao mnaheshimiana na kushirikiana kwa usawa. Usinunua urafiki kwa kuwa mtu wa kutoa zaidi na wala usinunuliwe kirafiki kwa kuwa tegemezi kwa wengine. Hilo litajenga mahusiano yasiyo bora na urafiki kukosa maana nzima.
Nukuu;
“In the case of certain men, the more they owe, the more they hate. A trifling debt makes a man your debtor; a large one makes him an enemy.” – Seneca
“Kwa baadhi ya watu, kadiri wanavyodaiwa ndivyo wanavyochukia. Deni dogo linamfanya mtu kuwa mdaiwa; deni kubwa linamfanya mtu kuwa adui.” – Seneca
Kitu cha nyongeza tunachoondoka nacho hapa ni kutokuwakopesha fedha marafiki. Kwa sababu hiyo ni njia ya haraka ya kuua urafiki, kutokana na chuki na uadui unaojengeka pale mahusiano yanapogeuka kuwa ya mdai na mdaiwa.
Rafiki yangu Mstoa, umejifunza mengi kwenye barua hii kuhusu kustaafu kwa kupunguza mambo ya kufanya kadiri muda unavyokwenda ili kuzidi kuwa na utulivu.
Lakini pia umejifunza kujenga urafiki sahihi na kuepuka kosa kubwa linaloua urafiki, pale utegemezi wa moja kwa moja unapotengenezwa.
Tuyazingatie haya tuliyojifunza ili tuweze kujenga maisha bora ya mafanikio na yenye utulivu mkubwa.
Kutoka kwa Mstoa mwenzako,
Kocha Dr Makirita Amani.
Asante sana,
Nimewahi poteza mrafiki kwaajili ya kukopeshana na mara moja huyu rafiki alikuwa katika wakati mgumu sana na alitaka kufungwa, ;akini ule mkopo ulifanya urafiki wetu ukome mpaka leo sijui yupo wapi.
LikeLike
Haya mambo hayadanganyi.
LikeLike
Madeni yanaua urafiki.
LikeLike
Ndiyo
LikeLike
Asante sana Hilo ni kweli kabisa kumkopesha fedha rafiki ni kutafuta kutoelewana kabisa na rafiki huyo na kujenga uadui
Asante sana
LikeLike
Ndivyo ilivyo.
LikeLike
Asante sana kocha kwa barua hii. Imenifunza mengi sana.
LikeLike
Karibu.
LikeLike
Asante Kocha,
” Unaoona huwezi kuwaacha, wako tayari kukuacha wakati wowote”. Ninalenga kufanya yale sahihi yanayonifurahisha, siyo kuwafurahisha wengine kwa kuwa ninaamini siwezi kuwafurahisha watu wote.
LikeLike
Kila la kheri
LikeLike
Nje wataonekana kukupenda na kukuthamini kwa kuwa ni tegemezi kwako, ila ndani yao watakuwa wanakuchukia kwa sababu watajiona wana deni kwako na ambalo hawawezi kulilipa.
LikeLike
Huo ndiyo ukweli mchungu.
LikeLike
Asante kocha,Inabidi kujenga urafiki wa kweli sio wa utegemezi wa kukopeshana fedha,na fedha zinaharibu urafiki wakati wa kudaiana.
LikeLike
Hakika
LikeLike