3177; Nidhamu na hamasa.

Rafiki yangu mpendwa,
Watu wengi kwenye maisha wamekuwa wanahangaika sana na hamasa.
Wamekuwa wanatafuta vitu vya kuwapa hamasa ili kuendelea na safari yao ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa.

Kwa bahati mbaya sana, hamasa haijawahi kuwa na manufaa makubwa kwa mtu, hasa kwenye safari ya mafanikio makubwa.

Hiyo ni kwa sababu hamasa ni hisia na hisia huwa zina tabia ya kuyumba yumba kila mara.
Kama unasubiri uongozwe na hisia, kuna wakati utajisikia kufanya na kuna wakati hutajisikia.

Hamasa ni nzuri kwenye kuanza kitu chochote, ni kama kuwasha kitu.
Lakini ili kuendelea kufanya mpaka matokeo makubwa yapatikane, hamasa pekee haitoshi.
Badala yake unahitaji nidhamu.

Nidhamu ndiyo ufunguo mkuu wa mafanikio.
Nidhamu ni kuweza kujisukuma kufanya kile ulichopanga kufanya iwe unajisikia kufanya au la.

Sehemu kubwa ya mafanikio ambayo watu wanayapata kwenye maisha yao, yanatokana na nidhamu kali wanayokuwa nayo.
Pale mtu anapojijengea nidhamu kali ya kupanga na kufanya bila kuacha, ndiyo unajua mtu wa aina hiyo amedhamiria kweli na lazima atafanikiwa.

Wale wanaokimbizana na hamasa kila wakati, hakuna makubwa wanayofanya.
Hiyo ni kwa sababu wanakuwa wanatumia muda mwingi kwenye kuhangaika na hamasa kuliko kufanya.
Wanakuwa na mlolongo wa vitu vingi vya kutimiza ndiyo waweze kufanya wanachopaswa kufanya.

Lakini kwa upande wa pili wa watu wenye nidhamu kali, kipaumbele chao cha kwanza ni kufanya.
Wanakuwa hawana milolongo mirefu. Wanapanga na kutikiza kama walivyopanga.

Hamasa kwa sehemu kubwa ipo kwenye maneno.
Wakati nidhamu kwa sehemu kubwa ipo kwenye vitendo.
Unaweza kuelezea hamasa vyovyote utakavyo.
Lakini inapokuja kwenye nidhamu, unahitaji kuonyesha.

Kwa sababu kusema ni rahisi na kufanya ni vigumu, nenda na ugumu.
Unapopanga kufanya kitu kwenye muda fulani, na muda huo unafika na ukawa hujisikii kukifanya, hupaswi kwenda na hizo hisia.
Bali unapaswa kwenda na nidhamu.
Ulipanga utafanya, basi fanya kama ulivyopanga bila kuangalia ni hisia gani unazo juu ya kitu.

Hamasa inaweza kufundishwa, ndiyo maana kumekuwa na mafunzo mengi sana kuhusu hamasa, ambayo pia bado yamekuwa hayana uhakika.
Nidhamu haiwezi kufundishwa, ni kitu ambacho mtu anakijenga ndani yake mwenyewe.

Hamasa inaanza na matamanio, hasa ya nje, yanayochochewa na wengine.
Lakini nidhamu inaanza na hasira ambazo mtu anakuwa nazo, kwa mabadiliko yanayotakiwa kufanyiwa kazi.

Nidhamu huwa inajengwa kwa matendo madogo madogo yasiyokuwa na madhara yoyote.
Kadiri unavyokuwa unafanya kwa juhudi kubwa chochote unachokuwa umepanga, ndivyo unavyozidi kuimarisha nidhamu yao ya ufanyaji.

Mwisho ni kupoteza kuna nguvu ya kumjengea mtu nidhamu kali kuliko kupata.
Kwa mfano pale kitu kinapokuwa kimefikia ukomo, watu huwa wanafanya kwa nidhamu kali hata kama hawajisikii kufanya.
Hivyo basi, kama umekuwa na tatizo la kukosa nidhamu, chagua kuwa na mtu atakayehakikisha kuna kitu kikubwa unachopoteza kama hutafanya kama ulivyopanga kufanya.
Kwa kuwa na mtu anayekuwajibisha, ambaye hatasikiliza sababu na visingizio vyako, utaweza kujenga nidhamu kali ya kufanya kwa msimamo bila kuacha.

Ukipanga, fanya.
Wakati wa kufanya unapofika na ukawa hujisikii kufanya, hapo hapo anza kufanya.
Ukiahidi, timiza.
Wakati wa kutekeleza unapofika na ukawa unatafuta sababu na visingizio, hapo hapo anza utekelezaji.
Ukiweza kujenga nidhamu kali ya kuamua na kufanya kwa msimamo bila kuacha, hakuna kitakachoweza kukuzuia usipate chochote unachotaka.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe