3180; Sitaki upate amani.

Rafiki yangu mpendwa,
Siku za karibuni nilikuwa nampigia mmoja wetu hapa simu.
Akaniambia nikiona simu yako nakosa amani.
Nikamwambia hivyo ni vizuri kabisa, kwa sababu hicho ni kiashiria kwamba programu inafanya kazi.

Japokuwa jina langu ni Amani, hicho ndiyo kitu ambacho sitataka ukipate kabisa.
Kwa sababu kupitia kujifunza kwa usomaji na hata kwa baadhi ya watu ambao wamepita kwenye hizi programu na kupotea, nimeona mlolongo ambao umekuwa unajirudia.

Mtu anaanza akiwa chini kabisa, anakuwa na msukumo mkubwa wa kujifunza. Anazingatia mafunzo yote na kuyafanyia kazi kwa uhakika.

Msukumo huo mkubwa wa kujifunza unawafanya waanze kupata ushindi. Kwa ushindi huo wanatoka chini walipokuwa na kuanza kupanda juu.

Ushindi wanaoanza kupata, unawafanya wawe na mazoea. Wanaona wameshajua kila kitu na hawahitaji tena kujifunza, au hakuna kipya cha kujifunza.
Hata uchukuaji wa hatua unabadilika, hawachukui tena kwa msukumo mkubwa, bali kwa mazoea.
Sifa wanazokuwa wanapata zinawapanda kichwani, kichwa kinakuwa kikubwa na hakisikilizi tena.

Mazoea na ujuaji vinapelekea mtu kushindwa na kujikuta anarudi kule alikotoka.
Pamoja na yeye mwenyewe kuwa amechangia kwenye hatua hiyo, bado hatakubali kwamba amekuwa na mchango.
Bali atatafuta sababu za kumfurahisha kwa nini ameshindwa.
Na hapo mwendo anakuwa ameumaliza.

Mfumo wa programu yetu wa kuhakikisha hupati amani mara zote ni wa kuanza na lengo kubwa. Kisha kupambana kwa kila namba kulifikia.
Kabla hujalifikia lengo hakuna kitu umefanya, hivyo unakuwa na msukumo mkubwa wa kulipambania.
Ukilifikia lengo tu, unapata pongezi, halafu hapo hapo lengo unalikuza mara mbili na hilo kuwa ndiyo lengo lako jipya.
Unarudi tena kwenye msukumo wa kufikia lengo kwa sababu unaona bado kuna kitu hujafikia.

Kama unajiuliza mwisho wa hili ni lini, kuna habari mbili;
Moja lengo tulilonalo ni kubwa, hivyo mapambano yake lazima yawe makubwa sana.
Mbili, hilo halitakuwa na mwisho, kwa sababu tunajua kwenye maisha kuna kwenda mbele au kurudi nyuma, hakuna kusimama.
Ukisimama, wakati dunia inaenda mbele, unakuwa unarudi nyuma.
Hivyo inabidi ukimbie mara mbili ili uende zaidi ya pale ulipo.

Hivyo basi, kwenye hii safari, sahau kuhusu amani. Amani utaipata ukifa.

Niliona kauli mahali inauliza kwa nini watu wakifa wanaambiwa wapumzike kwa amani (Rest In Peace) badala ya walio hai kuambiwa wakae kwa amani (Stay In Peace).
Na nadhani jibu lipo wazi, dunia haina amani, amani pekee utaipata ukifa.

Mpaka utakapofika huo wakati, ni kuendelea na mahangaiko bila amani.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe