3185; Mateso unayoyafurahia.

Rafiki yangu mpendwa,
Huwa kuna kauli inayosema watu waliofanikiwa wanakuwa wamefanya vitu ambavyo wasiofanikiwa hawapendi kuvifanya. Pia ni vitu ambavyo wao wenyewe hawapendi kuvifanya, ila wanakuwa hawana namna bali kuvifanya.

Ukweli ni kwamba huwezi kupata mafanikio makubwa kwa kufanya yale ambayo kila mtu anayafanya, tena kwa namna ambavyo anayafanya.
Kile ambacho kinafanywa na wengi huwa hakina mafanikio makubwa.

Ukiwaangalia watu wote walioweza kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yao, kuna namna wanakuwa wamepata mateso wanayoyafurahia.
Kuna vitu wanavyokuwa wanafanya kwa mapenzi makubwa, licha ya kuwa ni vitu ambavyo ni mateso kwa kila mtu.

Mateso ya vitu hivyo yanaweza kutokana na ugumu wa kitu au uchoshi wake.
Vitu vigumu ni vile ambavyo mtu anakuwa anavifanya kwa mara ya kwanza hivyo anakosea kuvifanya. Wengi hukata tamaa na kuacha kufanya. Lakini wanaofanikiwa sana huwa wanaendelea kufanya bila kuacha.

Vitu vyenye uchoshi ni vile ambavyo ni vya kawaida kabisa ila inabidi virudiwe rudiwe kufanywa kwa msimamo kila kuacha. Ni katika kurudia rudia huko kufanya ndiyo matokeo makubwa na mazuri yanazalishwa.
Walio wengi huwa wanapenda kufanya vitu vinavyowapa msisimko kila wakati kutokana na upya wake au mvuto wake kwa nje.
Lakini vitu vyenye mafanikio makubwa ni vile vya kawaida kabisa ambapo inabidi virudiwe rudiwe kufanywa kwa muda mrefu bila kuachwa.

Wasiofanikiwa huwa ni rahisi kuyumbishwa na vitu vipya na vya kusisimua vinavyowajia kila wakati.
Na huko kuyumbishwa kirahisi ndiyo kunakuwa kikwazo kwao kufanikiwa kwa kiasi kikubwa.

Wasiofanikiwa huwa wanatamani sana kuyaona maisha ya waliofanikiwa kwa undani, wakiamini kuna siri fulani wanakuwa nazo.
Lakini pale wanapopata nafasi ya kuyaangalia maisha ya waliofanikiwa kwa karibu ndivyo wanavyojionea hakuna jipya.
Wanashangaa jinsi ambavyo wale waliofanikiwa kuliko wao wanavyofurahia kufanya mambo ambayo wao hawataki hata kuyaona.

Unajua kabisa kwamba unachotaka ni mafanikio makubwa.
Na unajua ili kuyapata ni lazima ufanye vitu ambavyo unaweza usiwe unapenda kufanya.
Lakini inabidi uvifanye, iwe unapenda au hupendi, unajisikia kufanya au hujisikii.

Baraka kubwa kabisa kwenye maisha ni kupata mateso ambayo unafurahia kuyafanya.
Ukiweza kufanya kitu licha ya kwamba kinakutesa, unakuwa umewazidi wengine wengi ambao wanaacha kufanya kwa sababu wameshindwa kuyavumia mateso yaliyopo kwenye kitu hicho.

Unapaswa kuujua mchakato wa msingi kabisa unaopaswa kuutekeleza kila siku bila ya kuacha na kisha kuutekeleza kweli.
Ni msimamo wako kwenye utekelezaji wa mchakato wa msingi kila siku bila kuacha ndiyo unaokupa mafanikio makubwa.

Kitu kimoja tunachoendelea kukiona ni jinsi ambavyo mafanikio na mateso haviwezi kutengana.
Na hapo pia tunaona jinsi ambavyo wale wanaofanikiwa sana kuna namna akili zao zinakuwa za tofauti na ambao hawafanikiwi.
Kwa sababu ni mtu wa aina gani ambaye atakuwa tayari kuyafurahia mateso?
Kwa hakika lazima awe mtu wa ajabu, kwa vipimo vya kawaida na kulinganisha na wengine.

Kwenye safari ya mafanikio makubwa hufanyi kwa kuangalia wengine au unajisikiaje wewe.
Bali unafanya kwa kuziangalia namba zinakuletea matokeo gani.
Unaenda ukiboresha yale yanayokuletea matokeo unayoyataka.
Na hivyo ndivyo watu wanavyoweza kupiga hatua kubwa kwenye maisha yao.

Namba hazijali sana wewe unajisikiaje au unataka nini.
Bali zinatokana na juhudi zinazokuwa zimewekwa.
Kwa juhudi kuongezwa, namba nazo zinakuwa bora zaidi.

Ni mateso gani ambayo wewe unafurahia kuyafanya?
Vitu gani ambavyo wengine wanakwepa kuvifanya ila wewe upo tayari kuvifanya mara zote?
Karibu ushirikishe kwenye maoni hapo chini.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe