3187; Siyo ngumu kihivyo.

Rafiki yangu mpendwa,
Watu wengi wamekuwa wanalalamika maisha ni magumu na kuna ukweli fulani kwenye hilo.
Lakini bado tukiangalia kwenye uhalisia, maisha siyo magumu kihivyo, bali watu wenyewe wamekuwa wanazidisha ugumu wa maisha kwa mambo wanayofanya.

Kwa mfano kwa walio wengi, kuamka asubuhi na mapema ili kuianza siku kwa ushindi ni kitu kinachoonekana kuwa kigumu sana.
Lakini ukiangalia kwenye uhalisia, siyo vigumu kuamka asubuhi na mapema kama mtu amelala mapema.
Kumbe basi watu wanashindwa kuamka mapema kwa sababu wanachelewa kulala.
Sasa ukiwauliza nini kinawafanya wachelewe kulala, majibu utakayoyapata na ukalinganisha na malengo waliyonayo, vinakuwa havina uhusiano kabisa.

Mchekeshaji mmoja amewahi kusema hakuna kitu cha maana kwenye maisha yake kimewahi kutokea baada ya saa nne usiku. Hivyo alikuwa amejiwekea kanuni ya kuwa amelala muda huo.

Miaka mingi iliyopita, Benjamin Franklin alikuwa akiishi kwa kanuni hii; kuwahi kulala na kuwahi kuamka kunampa mtu afya, utajiri na hekima.
Unadhani nini kimebadilika hapo?
Hakuna. Kama unataka kuwahi kuamka, wahi kulala. Kuna ugumu gani kwenye hilo?

Labda umekuwa unajiambia wewe ni mtu wa kukesha zaidi.
Fanya zoezi hili rahisi kisha tumia matokeo yake kuchukua hatua sahihi.
Ni fursa ngapi nzuri umewahi kuzikosa kwa kuwahi kulala?
Na ni fursa ngapi nzuri umewahi kuzikosa kwa kuchelewa kuamka?
Majibu utakayopata yatumie kuboresha muda wako wa kulala na wa kuamka.

Tuendelee, ni jambo gani jingine ambalo watu wanalalamika ni gumu?
Yapo mengi, kama kuweka akiba, watu wanazidisha ugumu wake kwa kuanza na matumizi kabla ya akiba, mwisho wanakuwa wamemaliza fedha na hakuna cha kuweka akiba.
Akiba inatakiwa ianze kabla ya matumizi na hapo utalazimika kujibana kwenye kiasi kinachobaki.

Waambie watu wasome kitabu na watakuambia hawawezi, ila wape udaku na watasoma kurasa kwa kurasa.
Tatizo nini? Jibu lipo wazi, kufanya usomaji kuwa mgumu kuliko unavyopaswa kuwa.
Mtu akiona kitabu kikubwa anachoka hapo hapo.
Wakati angepanga kusoma kurasa 10 tu kila siku, ndani ya mwezi amemaliza kitabu na ndani ya mwaka vitabu zaidi ya 10.
Mtu yeyote anayesoma vitabu zaidi ya 10 kwa mwaka anakuwa bora sana kuliko wengine wengi anaoshindana nao.

Hiyo ilikuwa kwenye maisha na jinsi watu wanayazidishia ugumu.
Sasa twende kwenye safari ya mafanikio, ambayo inaonekana kuwa ndiyo ngumu zaidi kwa walio wengi.
Bado watu wamekuwa wanaongeza ugumu usio wa msingi kwenye safari yao.

Kwa mfano watu wengi wamekuwa wanashindwa kwenye maisha huku wakiwa wamejaribu vitu vingi tofauti tofauti.
Lakini kanuni ya mafanikio kwenye jambo lolote ipo wazi, fanya kitu kimoja kwa muda mrefu zaidi na lazima utapata ushindi.
Ukiacha kutawanya nguvu zako kwenye mambo mengi na kuzikusanya kwenye kitu kimoja, kwa muda mrefu na kwa msimamo, lazima utapata matokeo mazuri.
Ni vile wengi hawana subira na hivyo kujaribu kuharakisha kitu kinachopelekea waharibu kabisa.

Nikukumbushe hadithi ya kijana aliyetaka kusomea utawa ambaye alienda kwa mwalimu wa utawa na kumuuliza itamchukua muda gani kufikia ngazi ya utawa, mwalimu akamjibu miaka 10.
Kijana akamwambia yupo tayari kufanya kazi usiku na mchana, je hapo itamchukua muda gani? Mwalimu akamjibu, miaka 20.

Tunaona hapo kuna vitu ukitafuta tu njia ya mkato ndiyo unazidi kupotea.
Moja ya vitu hivyo ni mafanikio kwenye maisha.

Namna nyingine tunavyoongeza ugumu kwenye safari yetu ya mafanikio ni kujaribu kufanya vipya na vigumu wakati kuna vitu vya kawaida na vya msingi ambavyo hatujavikamilisha bado.
Kabla ya kuhangaika na mambo mapya na magumu, hakikisha kwanza yale ya msingi kabisa unayafanya kwa msimamo wa hali ya juu.
Utapata matokeo mazuri kwa kufanya mambo ya msingi kwa msimamo kuliko kuhangaika na mambo mapya kila wakati.

Kama safari yoyote uliyopo inakuwa ngumu kuliko ulivyotegemea au inachukua muda mrefu zaidi ya ilivyozoeleka, kuna namna unaongeza ugumu kwenye mchakato wako.
Jitathmini ili uweze kuuona ugumu huo na kuuondoa ili upate matokeo unayoyatarajia.

Kama ambavyo tumeona kwenye mifano tofauti tofauti hapa, huhitaji kuwa na akili nyingi sana ndiyo ufanikiwe, bali unachohitaji ni kufanya mambo ya msingi kwa muda mrefu zaidi ya ulivyozoea.
Acha kuhangaika na mambo mapya kila wakati na peleka juhudi zako zote kwenye yale ya msingi na utaweza kurahisisha mafanikio kwako.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe