Barua ya XXI; Kuhusu Sifa ambazo falsafa ya Ustoa inatupatia.
Rafiki yangu Mstoa,
Sisi binadamu huwa tunapenda kuwa na sifa fulani mbele ya wengine.
Huwa tunapenda umaarufu kupitia yale tunayofanya au tunayokuwa nayo kwenye maisha.
Na tamaa hiyo ya sifa na umaarufu ndiyo inawasukuma wengi kufanya hata mambo yasiyo sahihi ili tu kutimiza haja yao.
Tamaa ya sifa na umaarufu imekuwepo tangu enzi na enzi na mwanafalsafa Seneca aliona hilo kwenye mawasiliano yake na rafiki yake Lucilius.
Kwenye barua hii ya 21 ya mfululizo wa barua ambazo Seneca alimwandikia Lucilius, amemweleza jinsi ambavyo maandiko yake yatampa sifa na umaarufu wa kudumu.
Kwenye barua hii tunakwenda kujifunza jinsi na sisi tunavyoweza kuitumia falsafa hii ya Ustoa kujijengea sifa na umaarufu wa kudumu bila ya kufanya mambo yasiyokuwa sahihi.
Kabla hatujaingia kwenye barua na kujifunza, nataka kwanza nikuonyeshe kwa nini barua hii ni muhimu zaidi leo kuliko ilivyokuwa miaka zaidi ya elfu 2 iliyopita ambapo ndiyo iliandikwa.
Sote tunajua jinsi ambavyo mitandao ya kijamii imekuwa na uraibu kwa watu wengi kwenye zama hizi.
Ukiangalia ni faida ipi kubwa ambayo mitandao hiyo inawapa watu, huoni.
Lakini bado watu wanatumia mitandao hiyo kwa muda mrefu kuliko wanavyotaka.
Hiyo ni kwa sababu mitandao ya kijamii inawapa watu mtego wa kupata sifa na umaarufu wanaotaka.
Kupitia mitandao hiyo watu wamejifunza wakiweka vitu vya aina fulani wanapata wafuasi wengi.
Hilo ndiyo limepelekea watu kuweka mambo yasiyo sahihi kwenye mitandao ya kijamii, ili tu kupata sifa na umaarufu.
Wapo ambao wanaweka picha za uchi na wapo ambao wanaweka habari za uongo na uzushi. Wapo wengine ambao wanadhalilisha watu, yote hayo kwa lengo la kupata sifa na umaarufu.
Kwa kuweka mambo yasiyo sahihi kwenye mitandao ya kijamii, watu wamekuwa wanapata umaarufu ndani ya mitandao hiyo, kwa kuwa na wafuasi wengi.
Lakini umekuwa ni umaarufu usiokuwa na tija, kwani hauwi na manufaa yoyote kwa mtu nje ya mitandao hiyo.
Ili tuweze kupata sifa na umaarufu ambao utakuwa na tija kwetu, tunapaswa kuiishi misingi ya falsafa ya Ustoa kama ambavyo tumekuwa tunajifunza.
Na kupitia barua hii ya 21, tunakwenda kuona jinsi kuiishi misingi hiyo ya Ustoa kunatupa sifa na umaarufu.
Karibu tujifunze.
1. Wewe ndiye kikwazo kwako mwenyewe.
Lucilius alikuwa amemwandikia Seneca akimweleza kuna watu wanamwekea ugumu kwenye mambo yake.
Seneca anamjibu kwamba hakuna yeyote anayemwekea ugumu isipokuwa yeye mwenyewe.
Anamweleza wazi kabisa kwamba yeye ndiye kikwazo kwake mwenyewe.
Anaendelea kumfafanulia kwamba anakuwa kikwazo kwake mwenyewe kwa sababu hajui nini hasa anachotaka.
Anamweleza yuko vizuri kwenye kuelekeza njia sahihi kuliko kuifuata njia hiyo yeye mwenyewe.
Anamwambia anajua kabisa wapi furaha ya kweli ipo, lakini hana ujasiri wa kuipata furaha hiyo.
Anamsisitizia kwamba kinachomkwamisha ni kutokuwa tayari kuyaacha maisha aliyo nayo sasa ili kupata maisha bora zaidi.
Na ndiyo maana anabaki amekwama pale pale.
Seneca ameweka wazi hapo kwamba kama kuna kikwazo chochote kwenye maisha yetu, basi kinaanzia ndani yetu wenyewe na siyo nje.
Na sababu kubwa ni kutokujua kwa hakika nini tunachotaka na kukiendea na hivyo kubaki tumekwama pale tulipo.
Hatua ya kuchukua;
Amua sasa nini hasa unachotaka kwenye maisha yako, jua njia ya kukipata kisha kuwa na ujasiri wa kukiendea bila kujikwamisha wewe mwenyewe.
Jua kabisa hakuna kinachoweza kukukwamisha ila wewe mwenyewe.
Ukiweza kuvuka kikwazo cha ndani yako mwenyewe, utaweza kupata chochote unachokitaka kwenye maisha yako.
Nukuu;
“Your greatest difficulty is with yourself; for you are your own stumbling-block. You do not know what you want.” – Seneca
“Ugumu mkubwa upo ndani yako mwenyewe; kwa sababu wewe ndiyo kikwazo kwako mwenyewe. Hujui nini hasa unachotaka.” – Seneca
2. Kujifunza kutakufanya kuwa bora.
Seneca anaendelea kumweleza Lucilius kwamba kupitia kujifunza ndiyo kutampa mwanga na kumwezesha kuwa bora zaidi.
Anamweleza jinsi ambavyo watu waliojihusisha na waandishi bora wa zama za nyuma walivyoweza kupata sifa na umaarufu wa muda mrefu.
Seneca anamwonyesha kwamba kupitia kujifunza na kujihusisha na watu wanaofanya makubwa, jina lako halitafutika haraka kwenye uso wa dunia.
Na hili limekuwa kwa vitendo kwa Lucilius mwenyewe, sababu pekee ya sisi kumjua leo ni kwa sababu Seneca alikuwa akimtaja kwenye barua zake.
Watu wengi wanapita hapa duniani ila baada ya vifo vyao wanasahaulika kabisa.
Wanaweza kuwa walipata sifa na umaarufu kwenye baadhi ya mambo wakati wa uhai wao.
Lakini sifa na umaarufu wao havikudumu kwa muda mrefu baada ya vifo vyao.
Hiyo ni kwa sababu havikujengwa kwenye msingi imara.
Anachotuambia Seneca hapa ni kuhakikisha tunajihusisha na watu wanaofanya mambo yanayodumu vizazi na vizazi ili majina yetu yadumu pia.
Hatua ya kuchukua;
Una bahati kubwa ya kuwa kwenye jamii ya tofauti tunayoijenga ya KISIMA CHA MAARIFA na programu ya Bilionea Mafunzoni. Kama utakaa kwenye hii jamii na ukafanya yale unayopaswa kufanya, kwa hakika jina lako litaingia kwenye historia itakayodumu vizazi kwa vizazi.
Utakuwa sehemu ya mapinduzi makubwa yanayokwenda kutokea kwenye jamii zetu. Hivyo wajibu wako ni kuhakikisha unapambana kupata nafasi ya kuendelea kubaki kwenye jamii hii na utajenga sifa na umaarufu wa kudumu.
Nukuu;
“The deep flood of time will roll over us; some few great men will raise their heads above it, and, though destined at the last to depart into the same realms of silence, will battle against oblivion and maintain their ground for long.” – Seneca
“Mafuriko makubwa ya muda yatatufunika; baadhi ya watu wakuu watanyanyua vichwa vyao juu ya mafuriko hayo, na japo watakabiliwa na nguvu ya ukimya na kusahaulika, watapambana na kulinda sifa na umaarufu wao kwa muda mrefu.” – Seneca
3. Kaa kwenye nafasi yako.
Seneca anaendelea kumwambia rafiki yake Lucilius kwamba kujihusisha na watu wakuu kunampa mtu nafasi ya kukumbukwa kwa muda mrefu, lakini hilo siyo uhakika, kwani bado mtu anawajibika kutunza sifa aliyoipata kwa kukaa kwenye nafasi yake.
Hapa ndipo inapokuwa muhimu mtu kuiishi misingi sahihi ambayo imemkutanisha na watu wakuu.
Kwani pale mtu anapoiacha misingi hiyo, anapoteza nafasi aliyoipata.
Hatua ya kuchukua;
Kuna sifa zimekupa nafasi ya kuwa ndani ya jamii hii ya tofauti, lakini kupata nafasi haimaanishi ni ya milele kwako.
Bali unapaswa kuendelea kuipambania nafasi hiyo kwa kuendelea kuiishi misingi sahihi ya jamii hii ya tofauti.
Siku utakayoacha kuiishi misingi ya jamii hii ndiyo siku unapoteza sifa za kuwa sehemu ya jamii hii na hivyo jina lako kufutika kwenye ukuu.
Nukuu;
“Whenever men have been thrust forward by fortune, whenever they have become part and parcel of another’s influence, they have found abundant favour, their houses have been thronged, only so long as they themselves have kept their position; when they themselves have left it, they have slipped at once from the memory of men.” – Seneca
“Pale watu wanapopata sifa na umaarufu kupitia kujihusisha na watu wakuu, wataendelea kukumbukwa kama tu wataendelea kubaki kwenye nafasi hizo; wanapoziacha nafasi hizo, wanapotea kwenye kumbukumbu za watu.” – Seneca
4. Kupata chochote unachotaka, ondoa tamaa.
Seneca anamnukuu Epicurus ambaye alisema kama unataka kumfanya mtu kuwa tajiri, usimwongezee fedha, bali mwondolee tamaa.
Seneca anasema wazo hilo liko wazi kabisa na halihitaji ufafanuzi wa ziada.
Pia linaeleweka vizuri, halihitaji msisitizo mkubwa.
Seneca anasema wazo hilo halifanyi kazi kwenye utajiri pekee, bali linafanya kazi kwenye mambo yote kwenye maisha.
Kwa kitu chochote ambacho mtu anataka kupata, anapaswa kuondoa tamaa kwanza.
Seneca anaendelea kutoa mifano kama;
Ukitaka mtu aheshimike, usimwongezee heshima, bali mwondolee tamaa.
Ukitaka mtu awe na raha, usimwongezee raha, bali mwondolee tamaa.
Kwa mifano hiyo tunaona wazi kwamba tamaa ndiyo kikwazo kikubwa kwenye chochote tunachotaka.
Kwani tunapokuwa na tamaa sana na kitu, huwa tunajizuia kukipata.
Na hata ikitokea tumekipata, huwa hatukifurahii kwa sababu tamaa inahama.
Lakini tunapoondoa tamaa, tunafanya mambo kwa usahihi na hivyo kupata kile tunachotaka kupata.
Na hata tunapokipata, tunakifurahia kwa sababu kinakuwa kinatutosheleza.
Hatua ya kuchukua;
Kwa kila unachotaka kupata kwenye maisha yako, anza kwa kuondoa tamaa, maana hiyo ndiyo imekuwa kikwazo kikubwa kwako.
Fanya mambo yako kwa mpango sahihi uliouweka kwa fikra sahihi na siyo kwa kusukumwa na tamaa.
Nukuu;
“If you wish, to make Pythocles rich, do not add to his store of money, but subtract from his desires.” – Epicurus
“Kama unataka kumfanya Pythocles kuwa tajiri, usiongeze kwenye akiba yake ya fedha, bali ondoa tamaa kwake.” – Epicurus
5. Tamaa za kupuuza na za kuhadaa.
Seneca anaeleza kwamba tamaa za miili yetu huwa hazilingani, kuna tamaa ambazo tunaweza kuzipuuza na maisha yetu yakaenda vizuri kabisa.
Halafu kuna tamaa ambazo hatuwezi kuzipuuza, kwani zitaendelea kuusumbua mwili mpaka tuweze kuzitimiza.
Lakini hilo halimaanishi tutawaliwe na tamaa hizo, kwa kuzipa kila tulichonacho.
Badala yake tunapaswa kuzihadaa kwa kuzipa kiasi kidogo ili ziweze kutulia na kutupa uhuru wa kuendelea na mambo yetu.
Moja ya tamaa hizo ni njaa.
Seneca anasema tumbo likiwa na njaa huwa halisikii kitu chochote mpaka lipate chakula.
Huwezi kuipuuza njaa kwa muda mrefu.
Lakini pia haimaanishi ule kwa ulafi kwa sababu unaweza kupata chakula.
Badala yake unapaswa kula kwa kiasi kuituliza njaa kisha kuendelea na mambo yako mengine.
Kama watu wangekuwa wanakula kwa namna hii, tusingekuwa na magonjwa mengi ya uzito uliopitiliza ambayo watu wanahangaika nayo sasa.
Watu wamekuwa wanakula kupitiliza kwa ajili ya tamaa na kutaka kuikomesha njaa, kitu ambacho hawakiwezi.
Kitu chochote ambacho utahitajika kukifanya kwa uendelevu, usishindane nacho, kitakupoteza.
Fanya kwa kiasi kutimiza hitaji kisha endelea na mengine muhimu.
Hatua ya kuchukua;
Zijue tamaa ulizonazo ambazo unaweza kuzipuuza, hizi ni za vitu vyote vya nje kama kutamani vitu ambavyo wengine wanavyo, usihangaike nazo kabisa.
Pia zijue tamaa ambazo huwezi kuzipuuza, ambazo zinatokana na mahitaji ya mwili wako ambayo lazima yatimizwe.
Kwa tamaa hizo, timiza kwa kiasi badala ya kutaka kutosheleza kabisa tamaa iliyopo.
Nukuu;
“The belly will not listen to advice; it makes demands, it importunes. And yet it is not a troublesome creditor; you can send it away at small cost, provided only that you give it what you owe, not merely all you are able to give.” – Seneca
“Tumbo likiwa na njaa huwa halisikilizi ushauri, bali linataka kushibishwa kwa namna yoyote ile. Lakini tumbo siyo mdai msumbufu, ni rahisi kumhadaa kwa gharama kidogo; kwa kulipa kile ambacho linakudai na siyo kulipa vyote unavyoweza kutoa.” – Seneca
Muhimu ni kula kutuliza njaa uliyonayo na siyo ule kushiba kupitiliza. Kula hakuna mwisho, hata ukishiba sana leo, kesho utakuwa na njaa tena.
Ukiwa unakula kukomoa, utaishia kujikomoa wewe mwenyewe.
Rafiki yangu Mstoa, barua hii imetufunza mengi sana kuhusu kujenga sifa na heshima ya kudumu.
Pia imetupa funzo juu ya kupata tunachotaka kwa kuondoa tamaa badala ya kuongeza tunachotaka.
Na kwa tamaa ambazo hatuwezi kuziondoa, tunapaswa kuzituliza tu na siyo kushindana nazo.
Kama Wastoa, wajibu wetu ni kuweka kwenye matendo haya yote tuliyojifunza ili tuweze kuwa na maisha bora.
Kutoka kwa Mstoa mwenzako,
Kocha Dr Makirita Amani.
Asante Kocha,
Kwenye hii barua nimejikumbusha tamaa (greed) isipodhibitiwa tunakosa kujali masilahi ya wengine jambo linalopelekea kukosa mafanikio kwenye shughuli tunazo paswa kushirikiana na wengine.
LikeLike
Hiyo ni kweli.
LikeLike
Asante sana kocha, hakika hizi Falsafa zinatujenga na kutuimarisha.
•wewe(mimi) ndiye kikwazo wa maisha yangu mwenyewe
•kujifunza kunatufanya kuwa bora zaidi,
LikeLike
Tuyafanyie kazi haya tunayojifunza ili kuwa bora zaidi.
LikeLike
Seneca alizungumza mambo muhimu mno maelfu ya miaka iliyopita, imenishangaza kwamba hata mambo ya diet Seneca aliyazungumza miaka mingi sana iliyopita.
Hili la tamaa limenipa mwanga zaidi.
LikeLike
Hakika,
Ndiyo maana kuna kauli kwamba hakuna jipya chini ya jua.
Ni yale yale yanarudiwa kwa namna tofauti.
Tunaona wengi wanavyosumbuliwa na ulaji uliopitiliza ambao unakuwa mzigo kwao.
Tukizingatia hili la kudhibiti tamaa kwenye ulaji, tunaenda vizuri sana.
LikeLike
Hakika ukiondoa tamaa utakuwa na maisha Bora
Asante sana
LikeLike
Ndiyo.
LikeLike
Kuishinda tamaa ,ku jifunza, kuwa na kiasi
LikeLike
Ndiyo
LikeLike