3193; Ndiyo sababu ya kufanya.

Rafiki yangu mpendwa,
Karibu kila mtu anajua nini hasa anachotaka kwenye maisha yake.
Na pia wengi wanajua nini wanapaswa kufanya ili kupata wanachotaka.
Lakini cha kushangaza, inapokuja kwenye kufanya, wengi huwa hawachukui hatua.

Tunaweza kushangaa kwa nje, iweje watu washindwe kufanya kile wanachojua kabisa kwamba wanapaswa kufanya ili wapate wanachotaka.
Lakini kuna mengi yanayokuwa yanaendelea ndani ya mtu ambayo hatuaezi kuyajua.

Inapokuja kwa mtu mwenyewe, ambaye anajua kabisa anachopaswa kufanya ili kupata anachotaka, lakini anakwama kufanya, kile kinachomkwamisha ndiyo kinapaswa kuwa sababu ya yeye kufanya.
Yaani kile ambacho kinamzuia asifanye, ndiyo hicho hicho anapaswa kukitumia kama sababu ya kufanya, kimpe msukumo wa kufanya.

Kwa wengi kinachowazuia kufanya ni hofu. Hofu huwa zipo mbalimbali kama hofu ya kushindwa na hata hofu ya kufanikiwa.
Wengi huwa wanaingiwa na hofu kama watafanya halafu wakashindwa, wanaona watakuwa wamepoteza sana. Au kama watafanya wakafanikiwa, watakuwa wamejiongezea majukumu zaidi.
Kama mtu anakwamishwa kufanya na hofu, anatakiwa kuigeuza hofu hiyo kama sababu ya kufanya.
Yaani pale mtu anapopata hofu ya kufanya, ndiyo hapo hapo anatakiwa afanye.
Hiyo ni kwa sababu hofu ni kiashiria cha kutoka nje ya mazoea.
Huwezi kupata hofu pale unapofanya vitu ulivyozoea kufanya.
Ni pale unapotaka kufanya kitu kipya na cha tofauti ndiyo hofu kubwa huwa inakuingia.
Na hiyo ndiyo sababu kwa nini unapaswa kufanya kile unachohofia kufanya, kwa sababu ndiyo njia ya kutoka pale ulipokwama sasa.
Hivyo ukipatwa na hofu, badala ya kuacha, itumie hofu hiyo kama kichocheo cha kuanza kufanya mara moja.

Kitu kingine kinachowazuia wengi wasichukue hatua ni kujifanya ni wastaarabu kupitiliza.
Hapa watu wanaacha kufanya kwa sababu hawataki kuonekana ni wasumbufu kwa wengine.
Watu wanakuwa wanataka waonekane ni wastaarabu na hawana tatizo lolote.
Lakini pia huu ni mtego ambao unapaswa kuuvuka kama unataka kupiga hatua.
Inapokuja kwenye kupata kile hasa unachotaka, unaweza kukipata au unaweza kujifanya mstaarabu, huwezi kuwa navyo vyote kwa pamoja.
Ili uweze kupata chochote kile unachotaka, lazima uwasumbue watu wengi.
Hivyo basi, kama kinachokuzuia kufanya ni kutokutaka kuwasumbua wengine, hiyo ndiyo sababu kwa nini unatakiwa kufanya.
Kwa sababu ni kupitia kuwasumbua watu ndiyo wanakukumbuka kwa muda mrefu na kukufikiria wewe pale wanapokuwa na uhitaji.
Kwa chochote kile unachofanya, kama hakuna mtu yeyote amewahi kukuambia unamsumbua, maana yake ni hujafanya kwa ukubwa wa kutosha kukupa mafanikio unayotaka.
Unapokuwa unajikwamisha kufanya kwa sababu unataka uonekane mstaarabu, hapo hapo ndiyo unapaswa kuanza kufanya, tena kufanya kwa ukubwa ambao utawagusa wengi.

Kwenye maisha ni bora kuchukiwa kuliko kupuuzwa. Wanaokuchuki watakuwa wanakujua na wanakufikiria kwa muda mrefu, wakati wanaokupuuza hawajui hata kama upo, hivyo hakuna namna unaweza kunufaika nao.
Fanya kile unachopaswa kufanya, kwa sababu hata usipofanya, unakuwa hujatatua tatizo kuu ulilonalo.
Tatizo lolote unalokuwa nalo, litaweza kutatuliwa kwa wewe kufanya kile kinachohusisha eneo hilo.

Inapokuja kwa wewe kufanya unachopaswa kufanya ili kupata unachotaka, jua unapaswa kufanya hasa.
Na chochote kile kinachokuzuia usifanye, hicho hicho ndiyo kinakuwa sababu ya wewe kufanya.
Kila kikwazo kinachokuzuia, unapaswa kukigeuza kuwa njia ya kufika kule unakotaka.
Hatupaswi kuruhusu chochote kituzuie kupata kile hasa tunachotaka.
Ipo ndani ya uwezo wa kila mmoja wetu kuweza kupata chochote kile anachotaka.
Kinachohitajika ni mtu kuwa tayari kuendelea kufanya bila ya kuruhusu kumwamishwa na chochote kile.
Kama utafanya kilicho sahihi na ukakifanya kwa muda mrefu zaidi, lazima utafanikiwa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe