💯KCM2324010; Uwezekano.
Tumejipata, Tunaachilia Breki.
#JumatanoYaUwajibikaji
Mwanamafanikio,
Mwaka huu wa mafanikio 2023-2024 tumejipata kwa kuchagua kuweka umakini wetu wote kwenye kitu kimoja mpaka kitupe matokeo makubwa.
Na tunaachilia breki kupitia kufanyia kazi maeneo sita; MALENGO, KUJIKUBALI, UWAJIBIKAJI, UBUNIFU, MAWASILIANO na UTULIVU ili kuweza kupiga hatua kubwa.

💯 Neno la leo; Uwezekano
Leo ikiwa ni #JumatanoYaUwajibikaji tunaangalia umuhimu wa kuangalia zaidi uwezekano wa kitu badala ya kuangalia vikwazo.
Uzuri mmoja wa maisha ni kwamba huwa tunapata kile tunachokitafuta sana.
Kama unatafuta mtu wa kumlaumu kutokana na yale unayopitia, basi utampata.
Na kama unatafuta sababu za kuwajibika na maisha yako pia utazipata.
Huwa kuna usemi kwamba wazazi wapo kwa ajili ya kuwalaumu.
Kwamba kama maisha yamekupiga kisawasawa, hata kama ni kwa uzembe wako binafsi, huwezi kukosa sababu za kuwalaumu wazazi wako.
Kadhalika serikali, nayo inaingia kwenye hilo kundi la kutokukosa cha kulaumiwa.
Lakini huwezi kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa kulaumu wengine, au kulalamika.
Hakujawahi kujengwa mnara wa mlalamikaji bora.
Kulalamika na kulaumu wengine ni breki kubwa kwenye mafanikio ya wengi.
Njia pekee ya kuachilia breki hiyo ni kuchukua uwajibikaji wa kila kitu kwenye maisha yako.
Vile ulivyo sasa ni matokeo ya yale uliyofanya au kushindwa kufanya.
Huna mwingine wa kumlaumu.
Inawezekana kuna nafasi na fursa nzuri ulishindwa kuzitumia huko nyuma, lakini kujilaumu kwa hilo haitasaidia.
Badala yake linapaswa kukupa msukumo wa kufanya zaidi sasa.
Kwenye kila unachofanya, mbele yako unaweza kuona uwezekano au kuona vikwazo.
Vyote tayari vipo, ni wewe tu kuchagua unataka kutumia nini kati ya hivyo.
Ili kupiga hatua na kupata mafanikio unayoyataka, mara zote ona uwezekano.
Hata pale unapoona vikwazo vikubwa, tafuta uwezekano ndani yake.
Upo na ukiweza kuutumia, utafanya makubwa.
💯Hatua za kuchukua leo;
1. Andika ahadi yako ya mwaka wa mafanikio 2023-2024 kwa mtiririko wa NINI, LINI, WAPI, KWA NINI, NANI, VIPI na HISIA kisha weka kwenye kundi.
2. Soma kurasa 10 za kitabu cha MTAALA WA UTAJIRI na shirikisha uliyojifunza kwenye kundi.
3. Chukua hatua kwenye yale ambayo umeshajifunza na shirikisha kwenye kundi.
4. Matokeo unayopata yashirikishe kwenye kundi.
5. Kaa kwenye mchakato sahihi wa kile unachotaka kufikia na epuka usumbufu unaokuwa kikwazo kwako.
Makala ya ukurasa wa leo ni kuhusu hamasa na nidhamu na uhitaji wake kwenye mafanikio. Isome, weka maoni na nenda kachukue hatua. Fungua hapa; https://www.kisimachamaarifa.co.tz/2023/11/08/3234
Ukawe na siku bora kabisa ya leo, siku unayokwenda kushika hatamu ya maisha yako na kuifanya kuwa ya kipekee kabisa kwako.
Kocha.
💯