💯KCM2324017; Akili.
Tumejipata, Tunaachilia Breki.
#JumatanoYaUwajibikaji
Mwanamafanikio,
Mwaka huu wa mafanikio 2023-2024 tumejipata kwa kuchagua kuweka umakini wetu wote kwenye kitu kimoja mpaka kitupe matokeo makubwa.
Na tunaachilia breki kupitia kufanyia kazi maeneo sita; MALENGO, KUJIKUBALI, UWAJIBIKAJI, UBUNIFU, MAWASILIANO na UTULIVU ili kuweza kupiga hatua kubwa.

💯 Neno la leo; Akili.
Leo ikiwa ni #JumatanoYaUwajibikaji tunaangalia akili inavyotokana na uwajibikaji wa yajayo na siyo kukumbuka yaliyopita.
Huwa tunapenda kuangalia yakiyopita na kujisifia nayo kama ni mazuri au kuyalaumu kama ni mabaya.
Lakini hakuna mwenye nguvu kwenye mambo yaliyopita, hakuna namna unaweza kuyaathiri yaliyokwishapita.
Mabadiliko yapo kwenye yale yajayo ambayo bado hayajafanyiwa kazi.
Hayo ndiyo yana fursa kubwa ya kuleta mabadiliko kwenye maisha yako.
Akili siyo kukumbuka ya nyuma, bali kuwajibika na yajayo.
Akili ni kushika hatamu kwenye kile unachofanya, ukijua wewe ndiye unayehusika na kila kitu.
Angalia vitu unavyoweza kuvibadili na kuzalisha matokeo unayotaka badala ya kuhangaika na vitu ambavyo huwezi kuviathiri.
Kama kila mtu angechukua hatua kwenye yale yaliyo ndani ya uwezo wake, kwa kuwajibika na siyo kulalamika, hatua kubwa sana zingepigwa.
Wengi wanakwama kupiga hatua kwa sababu hawataki kuwajibika, bali wanataka kulalamika.
Na kwenye haya maisha, mafanikio makubwa yanaenda kwa wanaowajibika na siyo wanaolaumu na kulalamika.
Kuwajibika kwa kila jambo kwenye maisha yako ni moja ya njia za kuachilia breki kwenye mafanikio unayoyataka.
Ili uwajibike vizuri, weka mkazo kwenye yale unayoweza kuyaathiri moja kwa moja na siyo ambayo huwezi.
Kuwa na akili, fikiria zaidi yale yajayo kuliko unavyofikiria yaliyopita.
Hata kwenye gari, kioo cha kuangalia mbele ni kikubwa kuliko cha kuangalia nyuma.
Tuangalie mbele zaidi kuliko tunavyoangalia nyuma.
💯Hatua za kuchukua leo;
1. Andika ahadi yako ya mwaka wa mafanikio 2023-2024 kwa mtiririko wa NINI, LINI, WAPI, KWA NINI, NANI, VIPI na HISIA kisha weka kwenye kundi.
2. Soma kurasa 10 za kitabu cha MTAALA WA UTAJIRI na shirikisha uliyojifunza kwenye kundi.
3. Chukua hatua kwenye yale ambayo umeshajifunza na shirikisha kwenye kundi.
4. Matokeo unayopata yashirikishe kwenye kundi.
5. Kaa kwenye mchakato sahihi wa kile unachotaka kufikia na epuka usumbufu unaokuwa kikwazo kwako.
Makala ya ukurasa wa leo ni kuhusu ukuaji na changamoto. Isome, weka maoni na nenda kachukue hatua. Fungua hapa; https://www.kisimachamaarifa.co.tz/2023/11/15/3241
Ukawe na siku bora kabisa ya leo, siku unayokwenda kuwajibika kwa kuyaangalia yajayo badala ya kukwamishwa na yaliyopita.
Kocha.
💯