💯KCM2324018; Picha.
Tumejipata, Tunaachilia Breki.
#AlhamisiYaUbunifu
Mwanamafanikio,
Mwaka huu wa mafanikio 2023-2024 tumejipata kwa kuchagua kuweka umakini wetu wote kwenye kitu kimoja mpaka kitupe matokeo makubwa.
Na tunaachilia breki kupitia kufanyia kazi maeneo sita; MALENGO, KUJIKUBALI, UWAJIBIKAJI, UBUNIFU, MAWASILIANO na UTULIVU ili kuweza kupiga hatua kubwa.

💯 Neno la leo; Picha.
Leo ikiwa ni #AlhamisiYaUbunifu tunaangalia jinsi kutengeneza picha ya kifikra ya kile unachotaka ilivyo na nguvu kwenye kukipata.
Huwa kuna kauli inayosema picha moja ni sawa na maneno elfu moja.
Akili zetu huwa zinaelewa picha haraka kuliko maelezo.
Na hata kwenye maelezo, akili huwa inayageuza picha ndiyo iweze kuyaelewa.
Ndiyo maana chochote ambacho mtu unakitaka, kinapaswa kuanzia kwenye picha ya kifikra kwenye akili.
Hatua ya kwanza na muhimu ni akili kupata picha ya kile unachotaka.
Akili haijali sana kama kitu kinawezekana au hakiwezekani.
Yenyewe inapokea maelekezo kama ambavyo inapewa.
Pale picha fulani inapowekwa kwenye akili na kwa muda mrefu, ndivyo inavyokuwa na nguvu ya kuweza kufikiwa.
Wote walioweza kufanya makubwa, walianza na picha kubwa kwenye fikra zao na kwenda nayo bila kuyumba.
Picha hizo zinakuwa ni za vitu ambavyo havipo kabisa, lakini mtu unaamini vinapaswa kuwepo.
Kitendo cha kuweka kwenye fikra picha ya kitu ambacho bado hakipo ndiyo ubunifu.
Na ni kupitia ubunifu ndiyo watu wanaweza kuachilia breki na kuzalisha matokeo makubwa.
Usijizuie kwa sababu picha uliyonayo kwenye fikra zako haijawahi kuwepo kwenye uhalisia.
Wewe ipambanie hiyo picha mpaka iwe uhalisia na hapo utapata matokeo mapya na makubwa yanayokupa mafanikio.
Jenga picha kubwa kwenye akili yako ya kile unachotaka, kisha fanyia kazi picha hiyo ili kuweza kuigeuza kuwa uhalisia.
💯Hatua za kuchukua leo;
1. Andika ahadi yako ya mwaka wa mafanikio 2023-2024 kwa mtiririko wa NINI, LINI, WAPI, KWA NINI, NANI, VIPI na HISIA kisha weka kwenye kundi.
2. Soma kurasa 10 za kitabu cha MTAALA WA UTAJIRI na shirikisha uliyojifunza kwenye kundi.
3. Chukua hatua kwenye yale ambayo umeshajifunza na shirikisha kwenye kundi.
4. Matokeo unayopata yashirikishe kwenye kundi.
5. Kaa kwenye mchakato sahihi wa kile unachotaka kufikia na epuka usumbufu unaokuwa kikwazo kwako.
Makala ya ukurasa wa leo ni kuhusu kujitoa ili kupata unachotaka. Isome, weka maoni na nenda kachukue hatua. Fungua hapa; https://www.kisimachamaarifa.co.tz/2023/11/16/3242
Ukawe na siku bora kabisa ya leo, siku ya kuweka picha kubwa ya mafanikio unayoyataka kwenye fikra zako.
Kocha.
💯