💯KCM2324019; Usizunguke.
Tumejipata, Tunaachilia Breki.
#IjumaaYaMawasiliano
Mwanamafanikio,
Mwaka huu wa mafanikio 2023-2024 tumejipata kwa kuchagua kuweka umakini wetu wote kwenye kitu kimoja mpaka kitupe matokeo makubwa.
Na tunaachilia breki kupitia kufanyia kazi maeneo sita; MALENGO, KUJIKUBALI, UWAJIBIKAJI, UBUNIFU, MAWASILIANO na UTULIVU ili kuweza kupiga hatua kubwa.

💯 Neno la leo; Usizunguke.
Leo ikiwa ni #IjumaaYaMawasiliano tunaangalia jinsi kuzunguka kwenye mawasiliano kunavyowakwamisha wengi.
Kwa chochote unachotaka kupata kutoka kwa wengine, unapaswa kuwaambia moja kwa moja ni nini unataka kutoka kwao na unatakaje.
Haina haja ya kuzunguka kwenye mengine mengi halafu ndiyo uje kusema kile unachotaka.
Unapozunguka sana kwenye kujieleza, unajiweka kwenye hatari ya kutokueleweka vizuri na kuishia kukosa ulichotaka.
Umakini wa watu kwa sasa umeshuka sana. Wakati unakazana na maelezo mengi, wao wanakuwa wanafikiria vitu vingine tofauti kabisa.
Watu huwa wanatumia maelezo mengi na ya kuzunguka pale wanapokuwa wanataka kitu kutoka kwa wengine kwa hofu ya kukataliwa.
Kwa kuwa mtu anaweza kusema hapana kwenye kile anachoambiwa, wanaowaambia huwa wanatafuta njia ya kupunguza hayo makali ya kukataliwa.
Hivyo wanazunguka sana kama njia ya kuwalainisha watu kabla ya kuwaeleza kile wanachotaka.
Njia hiyo inaweza kuwa na nia njema.
Lakini kwa zama tulizopo sasa, hilo linakuwa kikwazo badala ya msaada.
Kwa watu kukosa umakini, kadiri unavyotumia muda mrefu kueleza kitu, ndivyo unavyozidi kuwapoteza.
Ili mawasiliano yaweze kuwa sahihi na yakamilike, waambie watu moja kwa moja na kwa uhakika kile unachotaka.
Ukishaeleza unachotaka, unawapa nafasi ya wao kukujibu.
Njia hii ina matokeo mazuri ikitumika.
Maana hata kama mtu atakataa, bado angekataa hata kama ungezunguka kiasi gani. Ila hapo unakuwa umeokoa muda na nguvu.
Usizunguke sana, nenda moja kwa moja kwenye kile unachotaka na kieleze kwa kugha rahisi kwa kila mtu kuelewa.
Hiyo itakupa matokeo mazuri.
Mawasiliano sahihi na yaliyokamilika, yaani ambayo watu wameelewana ni hitaji muhimu kwenye kuachilia breki na kupata mafanikio makubwa.
💯Hatua za kuchukua leo;
1. Andika ahadi yako ya mwaka wa mafanikio 2023-2024 kwa mtiririko wa NINI, LINI, WAPI, KWA NINI, NANI, VIPI na HISIA kisha weka kwenye kundi.
2. Soma kurasa 10 za kitabu cha MTAALA WA UTAJIRI na shirikisha uliyojifunza kwenye kundi.
3. Chukua hatua kwenye yale ambayo umeshajifunza na shirikisha kwenye kundi.
4. Matokeo unayopata yashirikishe kwenye kundi.
5. Kaa kwenye mchakato sahihi wa kile unachotaka kufikia na epuka usumbufu unaokuwa kikwazo kwako.
Makala ya ukurasa wa leo ni kuhusu vitu vinavyokupa ushindi. Isome, weka maoni na nenda kachukue hatua. Fungua hapa; https://www.kisimachamaarifa.co.tz/2023/11/17/3243
Ukawe na siku bora kabisa ya leo, siku ya kuweka picha kubwa ya mafanikio unayoyataka kwenye fikra zako.
Kocha.
💯