KCM2324021; Kutu
Tumejipata, Tunaachilia Breki.
#JumapiliYaMapumziko
Mwanamafanikio,
Mwaka huu wa mafanikio 2023-2024 tumejipata kwa kuchagua kuweka umakini wetu wote kwenye kitu kimoja mpaka kitupe matokeo makubwa.
Na tunaachilia breki kupitia kufanyia kazi maeneo sita; MALENGO, KUJIKUBALI, UWAJIBIKAJI, UBUNIFU, MAWASILIANO na UTULIVU ili kuweza kupiga hatua kubwa.

Neno la leo; Kutu.
Leo ikiwa ni #JumapiliYaMapumziko tunaangalia jinsi ambavyo tunapaswa kuitumia siku hii kuondoa kutu ya wiki nzima.
Kwenye siku za wiki kuna mambo mengi ambayo tunakuwa tumepanga na kudhamiria kufanya, lakini yanakosa nafasi.
Mambo hayo kushindwa kufanyika yanatengeneza kutu kwenye maisha yetu.
Kutu huwa inaharibu na kudhoofisha kitu na isipoondolewa huwa inakimaliza kabisa.
Kwenye maisha, baadhi ya mambo ambayo yamekuwa hayafanyiki kutokana na mtu kutingwa, yamekuwa yanafanya ubora wa maisha ya mtu kupungua.
Hiyo inakuwa inatokana na mambo hayo ambayo hayajafanyika kumpa mtu msongo wa aina mbalimbali.
Ili kuondoa kutu hizo ambazo zinajikusanya kidogo kidogo na kuleta madhara, tunapaswa kutenga siku za jumapili kwa ajili ya kukamilisha yale yaliyokwama kwenye wiki nzima.
Jumapili ni siku ya mapumziko ambayo haina ratiba yoyote maalumu ya kikazi.
Hivyo inaweza kutumika kukamilisha yale muhimu yaliyokwama kwenye wiki nzima, hasa yale ambayo ni binafsi.
Kwa kuitumia jumapili hivyo, unaondoa msongo ambao unakuwa unajijenga kwa mambo ambayo yanashindwa kukamilika kwenye nyakati ambazo yalipangwa.
Mkusanyiko wa mambo mengi ambayo yameshindwa kufanyika kama yalivyopangwa ndiyo chanzo cha msongo mkubwa kwa watu wengi na unaopelekea kupunguza ubora wa maisha ya mtu.
Wewe kuwa makini kwa kuzitumia siku za jumapili kuondoa hiyo misongo iliyopo kwa kutekeleza yale yaliyokwama kwa wiki nzima.
Hatua za kuchukua leo;
1. Leo ni siku ya mapumziko, wiki nzima umepambana kwa siku 6, siku hii ya 7 tenga muda wa kupumzika ili kukusanya nguvu za kuendelea na mapambano kwenye wiki nyingine.
2. Kamilisha mambo yako binafsi ambayo yalikwama kwa wiki nzima kutokana na kutingwa na shughuli zako za kikazi au kibiashara.
3. Tenga muda wa kupitia wiki unayomaliza na kupangilia wiki inayokwenda kuanza. Angalia yapi umefanya vyema na yapi ya kuboresha. Kisha panga matokeo unayotaka kuzalisha wiki inayofuata.
4. Fanya tathmini yako ya kazi/biashara kwa wiki uliyomaliza. Tathmini hii ihusishe namba muhimu ambazo unajipima nazo kwenye kile unachofanya. Tathmini inakuonyesha hatua ambazo umeshapiga na zile za kuendelea kupiga.
5. Tenga muda wa kutosha kwa watu muhimu kwako ili kujenga na kuimarisha mahusiano yako.
Makala ya ukurasa wa leo ni kuhusu kufanya mambo ya msingi kabla ya magumu. Isome, weka maoni na nenda kachukue hatua. Fungua hapa; https://www.kisimachamaarifa.co.tz/2023/11/19/3245
Ukawe na siku bora kabisa ya mapumziko leo, siku unayokwenda kuondoa kutu za wiki nzima ambazo zimetengenezwa na msongo wa kushindwa kukamilisha yale uliyokuwa umepanga.
Kocha.