💯KCM2324022; Wanajua.
Tumejipata, Tunaachilia Breki.
#JumatatuYaMalengo
Mwanamafanikio,
Mwaka wa mafanikio 2023-2024 tumejipata kwa kuchagua kufanyia kazi kwa ukubwa kitu kimoja mpaka kitupe mafanikio makubwa tunayoyataka.
Tumeachilia breki kwa kufanyia kazi maeneo sita; MALENGO, KUJIKUBALI, UWAJIBIKAJI, UBUNIFU, MAWASILIANO na UTULIVU ili kujipa uhakika wa kufanya makubwa.

💯 Neno la leo; Wanajua.
Leo ikiwa ni #JumatatuYaMalengo tunaona jinsi ambavyo watu wanaofanikiwa huwa wanajua watafanikiwa, kwa sababu ya malengo wanayokuwa wamejiwekea.
Safari yoyote ile kwenye maisha huwa inaanzia sehemu fulani.
Lakini tayari ikiwa na mwisho wa hiyo safari na njia ya kupita ili kuufikia mwisho huo.
Mwisho wa safari huwa ndiyo lengo kuu la safari.
Hatua ya kwanza ya mtu yeyote kufika kwenye safari aliyonayo, ni lazima ajue wapi anakoenda.
Bila kujua anakotaka kufika, mtu hawezi kuwa na uhakika wa safari.
Kama utajiandaa kwa safari na kwenda kwenye kituo cha mabasi, utapokelewa vizuri sana na wauzaji wa tiketi za mabasi mbalimbali.
Wataanza kwa kukuambia karibu sana, kisha swali la kwanza ni wapi unaenda.
Ukiwajibu hujui unakoenda, utawapa mshangao mkubwa. Hiyo ni kwa sababu wanajua tangu umetoka nyumbani kwako ulipaswa kuwa unajua wapi unataka kufika.
Ukikutana na wenye tamaa ya kuuza tiketi, watakuuzia tiketi ya popote na hivyo hutajua wapi unaenda na hata ukifika hutajua ufanye nini.
Hivyo ndivyo watu wengi wanayaendesha maisha yao kwa kukosa malengo.
Wanakuwa wanajiendea tu kwa mazoea na kufuata mkumbo wa wengine.
Kwa sababu hawajui wapi wanaenda, hawafiki popote.
Hivyo miaka inaenda, lakini wanajikuta wamebaki pale pale bila ya kupiga hatua zozote.
WATU WENYE MALENGO WANAFANIKIWA KWA SABABU WANAJUA NI WAPI WANAENDA.
Hilo ndilo hitaji la kwanza na la msingi kwenye mafanikio.
Nini hasa unachotaka kupata? Wapi hasa unakotaka kufika?
Ukishindwa kujibu swali hilo la msingi kwa uhakika, utazurura hapa duniani kwa maisha yako yote.
Utachoka sana, lakini yote utakayokuwa umehangaika nayo yanaishia kuwa ni kazi bure.
Kukosa malengo ni moja ya breki ambazo zinawazuia watu kufanikiwa.
Wataonekana wanahangaika sana, lakini hawapigi hatua.
Mahangaiko yao yote yanapotea kwa sababu yanakuwa hayajaelekezwa kwenye kitu chochote cha uhakika.
Hata ile hali ya watu kuhangaika na mambo mengi na kubadilika kila mara, ni kwa sababu wanakosa malengo ya uhakika.
Malengo yako ya uhakika ni kitu unachopaswa kuanza nacho kwenye kila siku yako.
Anza kila siku yako kwa kuyaandika malengo yako, kwa mfumo wa ahadi unayojiwekea kwa kuhusa maeneo saba muhimu.
Kisha kwenye siku yako, weka kipaumbele kwenye yale yanayochangia kwenye malengo yako na kupuuza mengine yote yasiyohusika.
Zingatia hili na litakuwa mwongozo mzuri na wa uhakika kwako.
💯Hatua za kuchukua leo;
1. Andika ahadi yako ya mwaka wa mafanikio 2023-2024 kwa mtiririko wa NINI, LINI, WAPI, KWA NINI, NANI, VIPI na HISIA kisha weka kwenye kundi.
2. Soma kurasa 10 za kitabu cha MTAALA WA UTAJIRI na shirikisha uliyojifunza kwenye kundi.
3. Chukua hatua kwenye yale ambayo umeshajifunza na shirikisha kwenye kundi.
4. Matokeo unayopata yashirikishe kwenye kundi.
5. Kaa kwenye mchakato sahihi wa kile unachotaka kufikia na epuka usumbufu unaokuwa kikwazo kwako.
Makala ya ukurasa wa leo ni kuhusu vitu vitakavyokupa ushindi unaoutaka. Isome, weka maoni na nenda kachukue hatua. Fungua hapa; https://www.kisimachamaarifa.co.tz/2023/11/20/3246
Ukawe na siku bora kabisa ya leo, kuongozwa na malengo makubwa uliyonayo ili kuwa na uhakika wa mafanikio kwenye maisha yako.
Kocha.
💯