KCM2324025; Ujasiri.
Tumejipata, Tunaachilia Breki.
#AlhamisiYaUbunifu
Mwanamafanikio,
Mwaka wa mafanikio 2023-2024 tumejipata kwa kuchagua kufanyia kazi kwa ukubwa kitu kimoja mpaka kitupe mafanikio makubwa tunayoyataka.
Tumeachilia breki kwa kufanyia kazi maeneo sita; MALENGO, KUJIKUBALI, UWAJIBIKAJI, UBUNIFU, MAWASILIANO na UTULIVU ili kujipa uhakika wa kufanya makubwa.

Neno la leo; Ujasiri.
Leo ikiwa ni #AlhamisiYaUbunifu tunaona jinsi ambavyo watu hawakosi ubunifu bali wanakosa ujasiri.
Ubunifu unahitajika sana kwenye safari ya kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha.
Wengi wamekuwa wanajiwekea breki kwa kujiambia wao siyo wabunifu.
Lakini huo siyo ukweli.
Kila mtu ni mbunifu.
Na ukitaka kuthibitisha hilo, angalia jinsi watu wanavyopangilia mavazi yao, hata kama hawana mengi.
Pia angalia pale watu wanapotaka kuwahi mahali fulani wanavyotumia njia za mkato.
Wanachokosa watu siyo ubunifu, bali ujasiri.
Kila mtu huwa anayapata mawazo ya kibunifu, lakini wanaotekeleza mawazo hayo ni wale wenye ujasiri wa kuchukua hatua.
Tuangalie mfano mwingine, ni mara ngapi umepata wazo fulani zuri na kujiambia ukiwa tayari utalifanyia kazi.
Haipiti muda unakuja kukuta mtu anafanyia kazi wazo lile lile na kwenye eneo lile lile.
Ubunifu unahitaji ujasiri kwa sababu unapaswa kuchukua hatua mara moja pale unapopata wazo, hata kama hujawa tayari.
Watu wanaosubiri mpaka wawe tayarj, ndiyo ambao wanaishia kushindwa vibaya.
Wakati wenye ujasiri wa kuchukua hatua mara moja, licha ya kukutana na magumu, huwa wanapiga hatua kubwa.
Usijiambie wewe siyo mbunifu, bali jijengee ujasiri wa kuchukua hatua kwenye kila wazo zuri unalopata bila kusubiri mpaka uwe tayari.
Achilia breki ulizojiwekea kwenye eneo la ubunifu kwa kuwa na ujasiri wa kufanya bila ya kuhofia au kusubiri uwe tayari.
Hatua za kuchukua leo;
1. Andika ahadi yako ya mwaka wa mafanikio 2023-2024 kwa mtiririko wa NINI, LINI, WAPI, KWA NINI, NANI, VIPI na HISIA kisha weka kwenye kundi.
2. Soma kurasa 10 za kitabu cha MTAALA WA UTAJIRI na shirikisha uliyojifunza kwenye kundi.
3. Chukua hatua kwenye yale ambayo umeshajifunza na shirikisha kwenye kundi.
4. Matokeo unayopata yashirikishe kwenye kundi.
5. Kaa kwenye mchakato sahihi wa kile unachotaka kufikia na epuka usumbufu unaokuwa kikwazo kwako.
Makala ya ukurasa wa leo ni kuhusu kuendelea kufanya licha ya ugumu wa mwanzo. Isome, weka maoni na nenda kachukue hatua. Fungua hapa; https://www.kisimachamaarifa.co.tz/2023/11/23/3249
Ukawe na siku bora kabisa ya leo, siku ya kuwa na ujasiri wa kuchukua hatua bila ya kusubiri kuwa tayari.
Kocha.