💯KCM2324028; Maigizo
Tumejipata, Tunaachilia Breki.
#JumapiliYaMapumziko
Mwanamafanikio,
Mwaka huu wa mafanikio 2023-2024 tumejipata kwa kuchagua kuweka umakini wetu wote kwenye kitu kimoja mpaka kitupe matokeo makubwa.
Na tunaachilia breki kupitia kufanyia kazi maeneo sita; MALENGO, KUJIKUBALI, UWAJIBIKAJI, UBUNIFU, MAWASILIANO na UTULIVU ili kuweza kupiga hatua kubwa.

💯 Neno la leo; Maigizo.
Leo ikiwa ni #JumapiliYaMapumziko tunaangalia jinsi ambavyo tunapaswa kuitumia siku hii kuigiza maisha ya ndoto zetu.
Kwa mujibu wa mchakato wetu wa KISIMA CHA MAARIFA, jumapili siyo siku ya mapambano makubwa kama siku nyingine za wiki.
Jumapili ni siku ambayo hatuna ratiba kali na kubwa za kutekeleza. Ni siku ya mapumziko ambayo yanatupa nguvu ya kuendelea kwa ukubwa kwenye siku nyingine za wiki.
Kwa kuwa siku hii ya jumapili haina ratiba kali na za lazima kwa mtu, ni siku unayoweza kutumia kuigiza aina ya maisha unayotaka.
Huwa kuna maana tofauti tofauti za mafanikio kulingana na yale ambayo watu wanakuwa wanataka.
Lakini wengi wanakubaliana kwamba mafanikio ni kuweza kufanya kile unachotaka kufanya (nini/what), kwenye wakati unaopanga kufanya (lini/when), kwa namna unavyotaka wewe (vipi/how), mahali unapochagua (wapi/where) na kwa kushirikiana na watu uliowachagua (nani/who).
Unapokuwa unaanzia chini na bado hujajenga mafanikio makubwa, unakuwa hujafikia ngazi ya mafanikio ya kuweza kuchagua mambo hayo matano kwenye ufanyaji.
Utalazimika kufanya usiyopenda, ili kupiga hatua ambazo ni muhimu kwa kuwa zinakutoa chini unapokuwa.
Kwa bahati nzuri, una siku za jumapili ambazo huna mambo mengi ambayo ni lazima uyakamilishe.
Hivyo unaweza kuitumia siku hii kuigiza aina ya maisha unayotaka kuwa nayo pale unapokuwa umeshapata mafanikio makubwa unayoyataka.
Hapa haimaanishi kwa upande wa starehe au matumizi, bali kwa upande wa jinsi maisha yako kwa ujumla yatakavyokwenda.
Kwa kufanya zoezi hilo la kuyaigiza maisha yako ya mafanikio, kuna mengi sana utakayojifunza ambayo yataboresha safari yako nzima.
Usiache kufanya zoezi hili kwa kuona ni la kitoto au lisilokuwa na tija.
Huenda mafanikio unayoyapambania yasiwe na maana kama unavyodhani.
Kwa kuyaigiza maisha ya mafanikio kabla hujayafikia, ufajifunza na kuyaboresha zaidi.
Hilo litafanya mafanikio unayokuja kupata yawe na maana kubwa kwako na kwa wengine.
💯Hatua za kuchukua leo;
1. Leo ni siku ya mapumziko, wiki nzima umepambana kwa siku 6, siku hii ya 7 tenga muda wa kupumzika ili kukusanya nguvu za kuendelea na mapambano kwenye wiki nyingine.
2. Kamilisha mambo yako binafsi ambayo yalikwama kwa wiki nzima kutokana na kutingwa na shughuli zako za kikazi au kibiashara.
3. Tenga muda wa kupitia wiki unayomaliza na kupangilia wiki inayokwenda kuanza. Angalia yapi umefanya vyema na yapi ya kuboresha. Kisha panga matokeo unayotaka kuzalisha wiki inayofuata.
4. Fanya tathmini yako ya kazi/biashara kwa wiki uliyomaliza. Tathmini hii ihusishe namba muhimu ambazo unajipima nazo kwenye kile unachofanya. Tathmini inakuonyesha hatua ambazo umeshapiga na zile za kuendelea kupiga.
5. Tenga muda wa kutosha kwa watu muhimu kwako ili kujenga na kuimarisha mahusiano yako.
Makala ya ukurasa wa leo ni kuhusu kujifunza kushinda kupitia kushindwa. Isome, weka maoni na nenda kachukue hatua. Fungua hapa; https://www.kisimachamaarifa.co.tz/2023/11/26/3252
Ukawe na siku bora kabisa ya mapumziko leo, siku unayokwenda kuigiza aina ya maisha ya mafanikio unayoyajenga ili kuyaboresha zaidi kadiri unavyokwenda.
Kocha.
💯