💯KCM2324029; Leo.

Tumejipata, Tunaachilia Breki.

#JumatatuYaMalengo

Mwanamafanikio,

Mwaka wa mafanikio 2023-2024 tumejipata kwa kuchagua kufanyia kazi kwa ukubwa kitu kimoja mpaka kitupe mafanikio makubwa tunayoyataka.

Tumeachilia breki kwa kufanyia kazi maeneo sita; MALENGO, KUJIKUBALI, UWAJIBIKAJI, UBUNIFU, MAWASILIANO na UTULIVU ili kujipa uhakika wa kufanya makubwa.

Utajiri ni mzuri na unauhitaji sana kwenye maisha yako. Jipatie nakala yako ya kitabu cha MTAALA WA UTAJIRI leo, tumia mawasiliano 0752 977 170.



💯 Neno la leo; Leo.

Leo ikiwa ni #JumatatuYaMalengo tunaona jinsi ambavyo siku ya leo ndiyo siku sahihi ya kuanza.

Huwa kuna kauli inasema wakati sahihi wa kupanda mti ulikuwa ni miaka 20 iliyopita.
Wakati mwingine sahihi wa kupanda mti ni sasa.

Kauli hiyo ina maana kubwa sana kwenye kuanza kufanya kitu chochote chenye manufaa kwako.

Kwa hapo ulipo sasa, kuna vitu unatamani ungekuwa navyo sasa, ambavyo ungepaswa kuwa ulivifanyia kazi kipindi cha nyuma.
Lakini hukuweza kufanya hivyo.
Unaweza kujilaumu kwa nini hukufanya hivyo wakati ilikuwa kabisa ndani ya uwezo wako.
Lakini haitakuwa na maana kama utajilaumu na kuishia hapo.
Badala yake unapaswa kuanza kufanya sasa ili kesho usijilaumu tena.

Hakuna siku bora ya kuanza kufanya kile unachopaswa kufanya kama leo.
Ndiyo, leo hii ndiyo bora kabisa kwako kuanza kufanya chochote unachotaka kwenye maisha yako.
Haijalishi kitachukua muda mrefu kiasi gani kukupa matokeo unayotaka, kilicho muhimu ni wewe kuanza kufanya.

Watu wengi wanajua nini wanataka.
Na wanajua nini wanapaswa kufanya ili kupata wanachotaka.
Tatizo linakuja kwenye kuanza kufanya.
Wengi hutaka mpaka kila kitu kiwe sawa ndiyo waanze kufanya.
Lakini wote tunajua kwamba kila kitu hakijawahi kuwa sawa.
Hata tukiahirisha kuanza kwa muda mrefu kiasi gani, bado kuna vitu vitakuwa havijakaa sawa.

Hivyo dawa ya hilo ni kuanza kufanya mara moja.
Na kufanya kwa mwendelezo bila kuacha.
Unaanza kufanya na unaendelea kufanya bila kuacha.
Unaenda ukiboresha ufanyaji wako lakini kamwe huachi.
Hivyo ndivyo unavyoweza kufanya makubwa kwenye maisha yako.

KWA CHOCHOTE UNACHOPANGA KUFANYA, SIKU NZURI YA KUANZA KUKIFANYA NI LEO.
Siyo kesho, wiki inayo, mwezi ujao au mwaka ujao, bali ni leo.
Kama utashindwa kuanza kufanya leo, jua hata hiyo siku unayojiambia utaanza hutaweza kuanza.
Mwaka mmoja kutoka sasa, utatamani sana kama ungekuwa umeanza leo.
Ili wewe uepuke majuto hayo, hebu anza kufanya leo hii.

Ni kitu gani muhimu sana umekuwa unapanga kuanza kufanya ila umekuwa unakisogeza mbele?
Anza kukifanya leo hii.
Wewe anza tu, hata kama kuna mengi unaona bado hayajakaa sawa.
Ni kupitia kuanza ndiyo utajua mengi ambayo hukuwa umeyajua.
Na ukishaanza, kinachofuata ni kuendelea kufanya bila kukoma.

Kuwa na malengo unayoyafanyia kazi kila siku ni njia muhimu ya kuachilia breki zinazokuzuia kufanikiwa.
Kuchelewa kuanza ni kushikilia breki, kuanza kufanya ni kuachilia breki.
Anza kufanya leo na utakuwa umeachilia breki ambazo zimekuzuia kwa muda mrefu.

💯Hatua za kuchukua leo;
1. Andika ahadi yako ya mwaka wa mafanikio 2023-2024 kwa mtiririko wa NINI, LINI, WAPI, KWA NINI, NANI, VIPI na HISIA kisha weka kwenye kundi.
2. Soma kurasa 10 za kitabu cha MTAALA WA UTAJIRI na shirikisha uliyojifunza kwenye kundi.
3. Chukua hatua kwenye yale ambayo umeshajifunza na shirikisha kwenye kundi.
4. Matokeo unayopata yashirikishe kwenye kundi.
5. Kaa kwenye mchakato sahihi wa kile unachotaka kufikia na epuka usumbufu unaokuwa kikwazo kwako.

Makala ya ukurasa wa leo ni kuhusu kubobea ya msingi kabla ya kuhangaika na magumu. Isome, weka maoni na nenda kachukue hatua. Fungua hapa; https://www.kisimachamaarifa.co.tz/2023/11/27/3253

Ukawe na siku bora kabisa ya leo, siku ya kuanza kufanya yale ya muhimu ambayo umekuwa unayaahirisha kwa muda mrefu.

Kocha.
💯