💯KCM2324030; Boksi.

Tumejipata, Tunaachilia Breki.

#JumanneYaKujikubali

Mwanamafanikio,

Mwaka wa mafanikio 2023-2024 tumejipata kwa kuchagua kufanyia kazi kwa ukubwa kitu kimoja mpaka kitupe mafanikio makubwa tunayoyataka.

Tumeachilia breki kwa kufanyia kazi maeneo sita; MALENGO, KUJIKUBALI, UWAJIBIKAJI, UBUNIFU, MAWASILIANO na UTULIVU ili kujipa uhakika wa kufanya makubwa.

Huu mkeka una hatua kwa hatua za kufuata ili kujenga biashara na kufanya uwekezaji kwa ngazi ya Ubilionea.



💯 Neno la leo; Boksi.

Leo ikiwa ni #JumanneYaKujikubali tunaona jinsi ambavyo dunia inakuweka ndani ya boksi na kukuzuia usitoke, kitu kinachokukwamisha kukua.

Dunia na hapo ikimaanisha watu wanaokuzunguka huwa wana tabia ya kukuweka ndani ya boksi la aina fulani, kisha kukutaka uende vile wanavyotaka wewe uende.

Pale unapojaribu kwenda tofauti na matarajio ya wale wanaokuzunguka, wanakukataza na kukutaka urudi kwenye matarajio ambayo wao wanayo kwako.

Unaweza kudhani wanakutaka ubaki kwenye matarajio hayo kwa sababu wanajali sana maslahi yako.
Lakini ukweli ni watu wanakutaka unaki kwenye matarajio waliyokuwekea kwa sababu ndivyo wanavyonufaika kupitia wewe.

Kwa sababu watu wananufaika pale unapobaki kwenye boksi ambalo wamekuweka, watafanya kila namna kuhakikisha hutoki kwenye boksi hilo.
Hiyo inahusisha kukutisha na kukujaza hofu kwamba ukijaribu tu kutoka kwenye boksi hilo basi umekwisha kabisa.

Hali hiyo ndiyo inayopelekea watu kutokujikubali na kujiamini na hivyo kuendelea kutumika kwa manufaa ya wengine.

Kitu unachopaswa kujua ni hakuna anayekujua wewe zaidi ya wewe mwenyewe.
Boksi lolote ambalo watu wamekuweka, kwa matarajio waliyoweka kwako ni kwa manufaa yao wenyewe.
Hivyo usikubali kamwe kunyamazishwa na yeyote.
Usikubali kuburuzwa kwa manufaa ya wengine.
Usipokee maelezo ya wengine wewe ni mtu wa aina gani na unaweza au huwezi kufanya nini.

Rudisha hatima ya maisha yako kwako mwenyewe.
Jielezee wewe mwenyewe.
Chagua aina ya maisha unayoyataka wewe.
Fanya yale unayotaka wewe, yanayokupeleka kule unakotaka kufika.
Puuza vitisho na hofu zote ambazo watu wanakujaza kwamba ukienda tofauti na wanavyokuambia basi utapotea.
Tayari umepotea kama unafuata ya wengine.

Jikubali, jiamini na fuata njia yako,
Hiyo ndiyo njia sahihi zaidi kwako.
Hata kama itaonekana kuwa ngumu,
Ndiyo njia itakayokupa matokeo makubwa.
Kumbuka, magumu yote huwa yanaweza kuvukwa.
Na matokeo yaliyo upande wa pili wa magumu huwa ni makubwa kuliko matokeo ya kufanya mazoea.

Kuamini wengine wapo sahihi zaidi kuhusu wewe kuliko wewe mwenyewe ni breki ambayo imewakwamisha wengi kupiga hatua kubwa kwenye maisha yao.
Achilia breki hiyo mara moja kwa kujiamini, kujikubali na kuchagua maisha unayotaka wewe na siyo unayopangiwa na wengine.
Huwezi kushindwa kwa kuchagua kuwa wewe na kuweka rasilimali zako zote kwenye kufanikisha hilo.

💯Hatua za kuchukua leo;
1. Andika ahadi yako ya mwaka wa mafanikio 2023-2024 kwa mtiririko wa NINI, LINI, WAPI, KWA NINI, NANI, VIPI na HISIA kisha weka kwenye kundi.
2. Soma kurasa 10 za kitabu cha MTAALA WA UTAJIRI na shirikisha uliyojifunza kwenye kundi.
3. Chukua hatua kwenye yale ambayo umeshajifunza na shirikisha kwenye kundi.
4. Matokeo unayopata yashirikishe kwenye kundi.
5. Kaa kwenye mchakato sahihi wa kile unachotaka kufikia na epuka usumbufu unaokuwa kikwazo kwako.

Makala ya ukurasa wa leo ni kuhusu kazi feki zinazokukwamisha usipige hatua. Isome, weka maoni na nenda kachukue hatua. Fungua hapa; https://www.kisimachamaarifa.co.tz/2023/11/28/3254

Ukawe na siku bora kabisa ya leo, siku ya kujikubali, kujiamini na kuchagua kuyaishi maisha unayotaka wewe mwenyewe na siyo unayopangiwa na wengine.

Kocha.
💯