💯KCM2324035; Nyumbani.

Tumejipata, Tunaachilia Breki.

#JumapiliYaMapumziko

Mwanamafanikio,

Mwaka huu wa mafanikio 2023-2024 tumejipata kwa kuchagua kuweka umakini wetu wote kwenye kitu kimoja mpaka kitupe matokeo makubwa.

Na tunaachilia breki kupitia kufanyia kazi maeneo sita; MALENGO, KUJIKUBALI, UWAJIBIKAJI, UBUNIFU, MAWASILIANO na UTULIVU ili kuweza kupiga hatua kubwa.



💯 Neno la leo; Nyumbani.

Leo ikiwa ni #JumapiliYaMapumziko tunaangalia jinsi ambavyo tunapaswa kuitumia siku hii kuwa zaidi nyumbani kuliko mahali pengine.

Kwa walio wengi, shughuli zao za kila siku zimekuwa zinawaweka mbali na nyumbani kwao.

Kwa wengi, hasa wanaoishi kwenye miji mikubwa ni kama wanaishi kwenye shughuli zao na kurudi kulala nyumbani.
Hiyo ni kwa sababu wanaondoka nyumbani asubuhi na mapema na kurudi usiku sana.

Kuna mazingira ambayo yanawabana watu kuwa na maisha ya aina hiyo na wanakuwa hawana namna katika kipindi hicho.
Lakini ni kitu ambacho hakipaswi kuruhusiwa kwenye siku zote za wiki.
Badala yake siku ya jumapili inapaswa kufanywa kuwa ya tofauti.

Siku ya jumapili inapaswa kuwa siku ya kutumia muda wako mwingi nyumbani.
Kwa sababu shughuli za wiki nzima zilikunyima fursa ya kuwa nyumbani, jumapili ni siku ya kufidia hilo.

Hivyo pangilia vizuri jumapili yako kuhakikisha huondoki nyumbani isipokuwa kwa mambo muhimu sana au ya dharura.
Itumie siku ya jumapili kuwa nyumbani ili kutekeleza mengi ambayo yamekwama kwa kukosekana kwako.

Uwepo wako nyumbani siku za jumapili pia ni sehemu ya kuimarisha mahusiano yako na familia yako.
Kwa sababu nyumbani siyo tu jengo la nyumba, bali na wale walio ndani yake.
Unapopatikana nyumbani unatoa pia nafasi kwa familia kuchangamana na wewe.

Siku sita za wiki fanya kazi zako kwa juhudi uwezavyo, hata kama itahusisha kukesha kwenye baadhi ya siku. Lakini siku moja ya wiki, hakikisha unaitofautisha na kazi na kuifanya kwa ajili ya mambo binafsi na ya kifamilia.
Ni kwa njia hiyo ndiyo utaweza kujenga mafanikio makubwa na ya kudumu kwenye maisha yako.

💯Hatua za kuchukua leo;
1. Leo ni siku ya mapumziko, wiki nzima umepambana kwa siku 6, siku hii ya 7 tenga muda wa kupumzika ili kukusanya nguvu za kuendelea na mapambano kwenye wiki nyingine.
2. Kamilisha mambo yako binafsi ambayo yalikwama kwa wiki nzima kutokana na kutingwa na shughuli zako za kikazi au kibiashara.
3. Tenga muda wa kupitia wiki unayomaliza na kupangilia wiki inayokwenda kuanza. Angalia yapi umefanya vyema na yapi ya kuboresha. Kisha panga matokeo unayotaka kuzalisha wiki inayofuata.
4. Fanya tathmini yako ya kazi/biashara kwa wiki uliyomaliza. Tathmini hii ihusishe namba muhimu ambazo unajipima nazo kwenye kile unachofanya. Tathmini inakuonyesha hatua ambazo umeshapiga na zile za kuendelea kupiga.
5. Tenga muda wa kutosha kwa watu muhimu kwako ili kujenga na kuimarisha mahusiano yako.

Makala ya ukurasa wa leo ni kuhusu akili ya kuvuka barabara. Isome, weka maoni na nenda kachukue hatua. Fungua hapa; https://www.kisimachamaarifa.co.tz/2023/12/03/3259

Ukawe na siku bora kabisa ya mapumziko leo, siku unayokwenda kutumia muda wako mwingi ukiwa nyumbani kuliko mihangaiko mingine.

Kocha.
💯