KCM2324036; Usipoteze.

Tumejipata, Tunaachilia Breki.

#JumatatuYaMalengo

Mwanamafanikio,

Mwaka wa mafanikio 2023-2024 tumejipata kwa kuchagua kufanyia kazi kwa ukubwa kitu kimoja mpaka kitupe mafanikio makubwa tunayoyataka.

Tumeachilia breki kwa kufanyia kazi maeneo sita; MALENGO, KUJIKUBALI, UWAJIBIKAJI, UBUNIFU, MAWASILIANO na UTULIVU ili kujipa uhakika wa kufanya makubwa.

 Neno la leo; Usipoteze.

Leo ikiwa ni #JumatatuYaMalengo tunaona jinsi ambavyo hatupaswi kupoteza kazi yoyote ambayo tumeshafanya kwa kuhakikisha tunaweka misingi sahihi.

Kuna wakati mtu unajikuta umeshafanya mambo mengi na makubwa, lakini hukuwa umeanza na msingi sahihi.
Kwa kukosa msingi huo sahihi, unakuwa umejiweka kwenye hatari ya kupoteza kila kitu.

Hali kama hiyo huwa inawaweka watu kwenye wasiwasi mkubwa na wasijue nini cha kufanya.
Wanaendelea kwenda kama walivyokuwa wanaenda mpaka pale inapotokea hali inayowapelekea kupoteza kila kitu.

Hilo hupaswi litokee kwako, unapaswa kulinda matokeo yoyote mazuri ambayo umeyazalisha.
Kama unajikuta umejenga nyumba bila ya msingi imara, badala ya kutamani tetemeko lisitokee ili isibomoke, unapaswa kuanza kujenga msingi ili kuilinda.

Kila unapogundua udhaifu uliopo kwenye kile unachofanya, ufanyie kazi mara moja kabla haujawa na madhara ya wewe kupoteza kila ambacho umeshakijenga.

Kama uliianza safari yako bila ya malengo, yaani umejikuta unajiendea tu, anza kwa kuweka malengo ambayo yataendeleza matokeo mazuri ambayo tayari unayapata.

Kila unachofanya hakikisha kimejengwa kwenye misingi sahihi ya kukuhakikishia matokeo mazuri na makubwa.
Kama kuna namna yoyote inayoweza kupelekea upoteze kile ambacho umeshajenga, chukua hatua mara moja kuzuia hilo.

Usipoteze chochote ambacho umeshajenga kwa namna yoyote ile. Hakikisha unajenga misingi sahihi inayolinda vyote ambavyo umeshapata.

Kuwa na malengo sahihi ni msingi muhimu ambao kila mtu anapaswa kuwa nao ili asipoteze juhudi kubwa anazoweka kwenye yale anayofanya.
Hakikisha unayo malengo sahihi kwenye kila unachofanya ili uweze kupata matokeo makubwa na ya uhakika.

Hatua za kuchukua leo;
1. Andika ahadi yako ya mwaka wa mafanikio 2023-2024 kwa mtiririko wa NINI, LINI, WAPI, KWA NINI, NANI, VIPI na HISIA kisha weka kwenye kundi.
2. Soma kurasa 10 za kitabu cha MTAALA WA UTAJIRI na shirikisha uliyojifunza kwenye kundi.
3. Chukua hatua kwenye yale ambayo umeshajifunza na shirikisha kwenye kundi.
4. Matokeo unayopata yashirikishe kwenye kundi.
5. Kaa kwenye mchakato sahihi wa kile unachotaka kufikia na epuka usumbufu unaokuwa kikwazo kwako.

Makala ya ukurasa wa leo ni kuhusu matokeo na muda, mkazo unapowekwa. Isome, weka maoni na nenda kachukue hatua. Fungua hapa; https://www.kisimachamaarifa.co.tz/2023/12/04/3260

Ukawe na siku bora kabisa ya leo, siku ya kujenga msingi imara kwenye kila unachofanya ili usipoteze matokeo ambayo tayari umeshayajenga.

Kocha.