KCM2324043; Kushindwa.
Tumejipata, Tunaachilia Breki.
#JumatatuYaMalengo
Mwanamafanikio,
Mwaka wa mafanikio 2023-2024 tumejipata kwa kuchagua kufanyia kazi kwa ukubwa kitu kimoja mpaka kitupe mafanikio makubwa tunayoyataka.
Tumeachilia breki kwa kufanyia kazi maeneo sita; MALENGO, KUJIKUBALI, UWAJIBIKAJI, UBUNIFU, MAWASILIANO na UTULIVU ili kujipa uhakika wa kufanya makubwa.

Neno la leo; Kushindwa.
Leo ikiwa ni #JumatatuYaMalengo tunaona jinsi ambavyo kushindwa siyo mwisho wa malengo, bali ni fursa ya kujipanga upya ili kuyafikia malengo kwa uhakika.
Karibu kila mtu huwa anaweka malengo kwenye maisha yake, hata kama ni kwa kusema tu.
Na wengi wanaoweka malengo, huwa wanaanza kabisa kuyafanyia kazi.
Lakini cha kushangaza, ni wachache sana ambao wanayafikia malengo waliyojiwekea.
Wengi sana wanaoweka malengo na kuanza kuyafanyia kazi, huwa wanaishia njiani.
Na shida kubwa huwa inaanzia pale wanapokutana na magumu na changamoto kwenye kufanyia kazi malengo yao.
Hapo ndipo huona kwamba malengo waliyojiwekea hayafai au hayawezekani na kisha kuachana nayo.
Rafiki, unachopaswa kujua ni kwamba kama uliweka malengo, basi ipo ndani ya uwezo wako kuyafikia.
Hata kama ni makubwa na yanaonekana ni magumu kiasi gani, kuna imani iliyo ndani yako ambayo ilikubali utaweza kuyafikia.
Sasa unapokutana na magumu na kuyaacha hayo malengo ni kujidharau wewe mwenyewe.
Na hata utakapoenda kwenye malengo mengine, nako utakutana na magumu na kwa kuwa umeshakuwa mkimbiaji, utayakimbia na hayo pia.
Rafiki, kuanzia sasa azimia kwamba ukishaweka malengo umeyaweka na hakuna kuyavunja au kuyaacha mpaka umeyafikia.
Pale unapokutana na magumu na hata kushindwa, siyo mwisho wa malengo uliyonayo.
Bali ni fursa kwako kujipanga upya na kurudi kwenye malengo hayo ukiwa na nguvu za kufanya makubwa zaidi.
Kwenye maisha, kushindwa siyo pale unapoanguka, bali kushindwa ni pale unapokata tamaa.
Kama umeanguka mara saba na ukainuka mara ya nane, bado wewe ni mshindi, ni swala la muda tu kuudhihirisha.
Jiwekee malengo makubwa kwenye maisha yako.
Na ukishayaweka, usiyaache kamwe mpaka umeyafikia.
Unapoanguka, inuka, jipange upya na endelea kuyapambania malengo yako.
Kamwe usibadili au kuyaacha malengo, badala yake badili mikakati na mbinu unazotumia kuyafikia malengo hayo.
Kutokuwa na malengo sahihi au kuwa nayo na kuyaacha pale unapokutana na magumu ni moja ya breki zinazowazuia wengi kufanikiwa.
Achilia breki hizo kwa kuweka malengo sahihi na kwa maandishi, kisha kuyageuza kuwa ahadi ya maisha yako ambayo unaiishi kila siku bila kuivunja.
Kwa njia hiyo utaweza kufanya makubwa sana.
Hatua za kuchukua leo;
1. Andika ahadi yako ya mwaka wa mafanikio 2023-2024 kwa mtiririko wa NINI, LINI, WAPI, KWA NINI, NANI, VIPI na HISIA kisha weka kwenye kundi.
2. Soma kurasa 10 za kitabu cha MJASIRIAMALI MJANJA na shirikisha uliyojifunza kwenye kundi.
3. Chukua hatua kwenye yale ambayo umeshajifunza na shirikisha kwenye kundi.
4. Matokeo unayopata yashirikishe kwenye kundi.
5. Kaa kwenye mchakato sahihi wa kile unachotaka kufikia na epuka usumbufu unaokuwa kikwazo kwako.
Makala ya ukurasa wa leo ni kuhusu mambo ya kuzingatia na mambo ya kuepuka ili kufanikiwa. Isome, weka maoni na nenda kachukue hatua. Fungua hapa; https://www.kisimachamaarifa.co.tz/2023/12/11/3267
Ukawe na siku bora kabisa ya leo, siku ya kuendelea kuyapambania malengo yako hata kama umeanguka mara nyingi kwenye malengo hayo.
Kocha.