💯KCM2324045; Kubadili.

Tumejipata, Tunaachilia Breki.

#JumatanoYaUwajibikaji

Mwanamafanikio,

Mwaka wa mafanikio 2023-2024 tumejipata kwa kuchagua kufanyia kazi kwa ukubwa kitu kimoja mpaka kitupe mafanikio makubwa tunayoyataka.

Tumeachilia breki kwa kufanyia kazi maeneo sita; MALENGO, KUJIKUBALI, UWAJIBIKAJI, UBUNIFU, MAWASILIANO na UTULIVU ili kujipa uhakika wa kufanya makubwa.

💯 Neno la leo; Kunadili.

Leo ikiwa ni #JumatanoYaUwajibikaji tunaona jinsi ambavyo unawajibika kwako mwenyewe kwa kubadilika wewe na siyo vitu vya nje.

Kuna vitu ambavyo ni dhahiri kabisa vinaweza kuwa vinakuzuia usipate kile unachotaka.

Familia uliyozaliwa na kukulia inaweza kuwa na changamoto ambazo zinakukwamisha, lakini huwezi kuibadili.

Msimu fulani unaokuwa unapitia unaweza kuwa unakukwamisha, lakini huwezi kuubadili msimu.

Hali ya uchumi inaweza kuwa inakukwamisha, lakini huwezi kuibadili hali ya uchumi.

Unaweza kuyalalamikia sana mambo hayo na mengine ya aina hiyo, lakini haitakusaidia wewe kupata kile unachotaka.

Kwa sababu unapolalamikia au kulaumu chochote, unakuwa umekipa nguvu ya kukubakisha pale ulipo.

Njia pekee ya kutoka pale ulipo na kufika mbali zaidi ni kwa kuwa na uwajibikaji binafsi.
Kwenye uwajibikaji binafsi unabadili kile ambacho kipo ndani ya uwezo wako kukibadili.
Na katika hali zote zinazokukwamisha, kitu pekee unachoweza kukibadili ni wewe mwenyewe.

Huwezi kubadili wengine, msimu au uchumi, lakini unaweza kubadilika wewe ili kuzitumia hali hizo zinazokukwamisha ili kupiga hatua zaidi.

Yaani kwa kushika hatamu na uwajibikaji binafsi, ukabadilika kulingana na hali zinazokuwa zinakukwamisha, unakuwa umegeuza mkwamo wowote unaopitia kuwa ndiyo njia ya kufanikiwa.

Unapobadilika wewe, vile ulivyokuwa unavilalamikia ni vikwazo kwako, unaona njia bora ya kuvifanya kuwa ndiyo njia ya mafanikio.

Kukosa uwajibikaji imekuwa breki inayowazuia wengi kufanikiwa. Kulalamika na kulaumu imekuwa rahisi kwa wengi, lakini imekuwa haileti manufaa. Haijalishi ni vikwazo gani unakutana navyo, ukichagua kubadilika wewe, utaweza kuvitumia vikwazo hivyo hivyo kufanikiwa.

Kumbuka wewe siyo mti kiasi kwamba ulazimike kubali pale ulipo.
Kama kuna kitu ambacho ni kikwazo kwako unapaswa kukibadili.
Na kama huwezi kukibadili, basi badilika wewe.
Ni rahisi kama hivyo na ina nyuvu ya kukujengea mafanikio makubwa.

💯Hatua za kuchukua leo;
1. Andika ahadi yako ya mwaka wa mafanikio 2023-2024 kwa mtiririko wa NINI, LINI, WAPI, KWA NINI, NANI, VIPI na HISIA kisha weka kwenye kundi.
2. Soma kurasa 10 za kitabu cha MJASIRIAMALI MJANJA na shirikisha uliyojifunza kwenye kundi.
3. Chukua hatua kwenye yale ambayo umeshajifunza na shirikisha kwenye kundi.
4. Matokeo unayopata yashirikishe kwenye kundi.
5. Kaa kwenye mchakato sahihi wa kile unachotaka kufikia na epuka usumbufu unaokuwa kikwazo kwako.

Makala ya ukurasa wa leo ni kuhusu usiwajengee kushindwa. Isome, weka maoni na nenda kachukue hatua. Fungua hapa; https://www.kisimachamaarifa.co.tz/2023/12/13/3269

Ukawe na siku bora kabisa ya leo, siku ya kuchukua uwajibikaji binafsi kwa kubadilika wewe mwenyewe pale unapokuwa kwenye hali ambazo huwezi kuzibadilisha.

Kocha.
💯