💯KCM2324047; Kinachoendelea.
Tumejipata, Tunaachilia Breki.
#IjumaaYaMawasiliano
Mwanamafanikio,
Mwaka wa mafanikio 2023-2024 tumejipata kwa kuchagua kufanyia kazi kwa ukubwa kitu kimoja mpaka kitupe mafanikio makubwa tunayoyataka.
Tumeachilia breki kwa kufanyia kazi maeneo sita; MALENGO, KUJIKUBALI, UWAJIBIKAJI, UBUNIFU, MAWASILIANO na UTULIVU ili kujipa uhakika wa kufanya makubwa.

💯 Neno la leo; Kinachoendelea.
Leo ikiwa ni #IjumaaYaMawasiliano tunaona jinsi ambavyo mawasiliano sahihi ndiyo njia bora ya kujua kinachoendelea kwa mtu.
Sisi binadamu bado hatujafikia uwezo wa kusoma kinachoendelea kwenye fikra za watu.
Tunaweza kubashiri tu kulingana na yale ambayo mtu anayaonyesha kwa nje, lakini siyo kwa usahihi.
Njia sahihi ya kujua kile kinachoendelea ndani ya mtu ni kwa wao wenyewe kutueleza, kwa mawasiliano sahihi.
Utaweza kuelewa fikra, hisia na uzoefu vilivyo ndani ya mtu kama tu atachukua muda wa kukueleza ukaelewa.
Kadhalika na wewe utaweza kueleweka na wengine kama utajieleza vizuri.
Mawasiliano sahihi ni muhimu sana kwenye kujenga mahusiano mazuri na ushirikiano mzuri na wengine.
Mara zote eleza kwa usahihi kile kinachoendelea ndani yako na unachotaka wengine wajue.
Usikae kimya ukidhani wengine watakuelewa, watu hawawezi kusoka kilicho ndani yako.
Pia epuka sana kubadili tabia fulani kama kuwaonyesha watu ishara ya kinachoendelea ndani yako. Kwa mfano pale mtu anapochagua kununa pale ambapo hajafurahishwa na kitu.
Ananuna kama sehemu ya kufikisha ujumbe kwa wengine, lakini ni mara chache sana wanaolengwa kuupata ujumbe huo.
Hivyo kinachotokea ni mtoa ujumbe kuzidi kuumia huku mlengwa wa ujumbe akiwa anaendelea na maisha yake bila kujali.
Njia sahihi ya kueleweka na wengine ni kuwaeleza kwa usahihi kile kinachoendelea ndani yako.
Eleza kwa usahihi ili ueleweke na kufikisha kile ulichotaka kifike.
Usitumie mafumbo au kubadili tabia, utavunja mawasiliano na kupoteza muda.
Kukosekana kwa mawasiliano sahihi ni moja ya breki zinazowazuia wengi kufanikiwa.
Wewe achilia breki hizo kwa kujieleza kwa usahihi ili kutoa kila kilicho ndani yako. Pia kuwa msikilizaji makini ili uweze kuwaelewa vizuri wengine.
💯Hatua za kuchukua leo;
1. Andika ahadi yako ya mwaka wa mafanikio 2023-2024 kwa mtiririko wa NINI, LINI, WAPI, KWA NINI, NANI, VIPI na HISIA kisha weka kwenye kundi.
2. Soma kurasa 10 za kitabu cha MJASIRIAMALI MJANJA na shirikisha uliyojifunza kwenye kundi.
3. Chukua hatua kwenye yale ambayo umeshajifunza na shirikisha kwenye kundi.
4. Matokeo unayopata yashirikishe kwenye kundi.
5. Kaa kwenye mchakato sahihi wa kile unachotaka kufikia na epuka usumbufu unaokuwa kikwazo kwako.
Makala ya ukurasa wa leo ni kuhusu ahadi hewa. Isome, weka maoni na nenda kachukue hatua. Fungua hapa; https://www.kisimachamaarifa.co.tz/2023/12/15/3271
Ukawe na siku bora kabisa ya leo, siku ya kujieleza kwa usahihi ili kuweza kutoa kile kinachoendelea ndani yako na kukamilisha mawasiliano na wengine kwa usahihi.
Kocha.
💯